HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 20, 2023

MRADI WA FUNGUO WATANGAZA WASHINDI 17, KUPATA BILIONI 1.2 KUSAIDIA KAMPUNI CHANGA ZA KIBUNIFU

 Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
WASHINDI 17 wa dirisha la pili la Mradi wa Funguo wakabidhiwa kitita cha shilingi Bilioni 1.2 kupitia Mradi uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania pamoja na Umoja wa Mataifa.

Meneja mradi wa Funguo Joseph Evarist Manelukiza akizungumza mara baada ya  kuwatangaza washindi hao amesema kuwa ni kutoka katika kampuni changa za kibunifu za Kitanzania ambapo wataboresha Mazingira ya Biashara, Ukuaji na Ubunifu na kuwawezesha wabunifu ambao wanaanza ili waweze kuendesha biashara zao na ziweze kusonga mbele.

Amesema jukumu kubwa la Mradi wa Funguo ni kuwezesha makampuni machanga ya Wabunifu wanaoibukia kwa kutoa mitaji wezeshi ili waweze kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine.

Amesema kuwa wale wengine waliokosa wataunganishwa na taasisi nyingine ili waweze kupata mitaji kama walivyodhamilia kutoka katika taasisi mbalimbali zinazotoa mitaji kwa vijana wajasiriamali.

Amesema kuwa awamu ya kwanza waliomba na kupata mtaji ni 26 na awamu ya pili wamepata 17 ambapo wamepata jumla ya shilingi bilioni 3.8.

Akizungumzia vigezo ambavyo vimewawazesha kupata washindi 17 kwa awamu ya pili amesema kuwa ilikuwa ni lazima kuonesha kampuni inaubunifu ndani yake, kampuni inauwezo wa kukua, kuonesha kuwa italeta matokeo chanya, kutoa ajira kwa watu wengine pamoja na kuonesha timu ambayo inaendesha biashara.

Maombi ya awamu ya pili yalitoka katika mikoa 22 kote nchini na kujumuisha sekta muhimu zikiwemo kilimo, nishati, uvuvi, huduma za afya, elimu na masuluhisho yanayoendeshwa na teknolojia.

Kwa Upande wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Mazingira ya Biashara, Wizara ya Uwekezaji na Mipango, Baraka Aligaesha akiwasilisha mada katika majadiliano amesema, “Kama Serikali, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaboresha michakato ya udhibiti, kupunguza urasimu, na kutekeleza sera zinazohimiza ujasiriamali.

Amesema malengo ni kurahisisha biashara ili kubadili mazingira ya biashara kuwa mazuri kwa kuwekeza katika miundombinu, elimu, na ukuzaji wa ujuzi ili kuhakikisha msingi thabiti wa uvumbuzi inashamili kupitia ubia wa kimkakati na sekta binafsi.

Naibu kamishna mkuu wa ubalozi wa Uingereza, Rick Shearn amesema kuwa Serikali ya Tanzania inawekeza katika vipaji, uwezo na fursa kwa mustakabali wa Tanzania. “Ninawaomba wadau wote kushirikiana nasi na kuoanisha juhudi zetu kuelekea kufungua uwezo wa vijana wetu. Fursa zilizo mbele yao ni kubwa sana, lakini wanahitaji uwekezaji ili kufadhiliwa kikamilifu. Kwa kuwekeza kwa vijana, tunawekeza katika mustakabali wa Tanzania.” Amesema

“Tunajitahidi kuweka mazingira rafiki ya kibiashara ambayo yanavutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.” ameongeza.

Akizungumzia kuhusiana na Mipango ya Tume ya Tehama, Mkurugenzi wa Tume ya Tehama, Kundwe Mwasaga amesema serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na wabia mbalimbali nchini ili kuwawezesha vijana na waweze kuanzisha kampuni zao kuhakikisha kwamba vijana wanapata fursa.

“Serikali imetenga fedha katika tume ya Tehama nchini ili kujenga vituo ambavyo vitakuwa na kazi ya kuibua biashara za kibunifu katika mikoa yote.”

Pia amesema Serikali inajenga vituo sita vya Tehama hapa nchini katika mikoa ya Arusha, Mbeya, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Tanga na Zanzibar ili kuhakikisha kwamba wajasiriamali wadogo wanapata mafunzo na wanapata mtaji ambao utasaidia kampuni zao kukua.

“Serikali ya awamu ya sita imeweka mkazo katika sekta zote lakini kwa kutumia teknolojia ambazo takakuwa zikichagiza maendeleo hapa nchini.

Meneja mradi wa Funguo Joseph Evarist Manelukiza akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 20, 2023 mara baada ya kutambulisha washindi 17 waliokuwa wakiwani bilioni 1.2 zilizotolewa na UNDP wakishirikiana na Umoja wa Mataifa.
Mkurugenzi wa Tume ya Tehama, Kundwe Mwasaga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 20, 2023 mara baada ya kutambulishwa kwa washindi 17 waliokuwa wakiwani bilioni 1.2 zilizotolewa na UNDP wakishirikiana na Umoja wa Mataifa.
Naibu kamishna mkuu wa ubalozi wa Uingereza, Rick Shearn akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 20, 2023 mara baada ya kutambulishwa kwa washindi 17 waliokuwa wakiwani bilioni 1.2 zilizotolewa na UNDP wakishirikiana na Umoja wa Mataifa.
Mmoja wa wanufaika wa Mradi huo kizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 20, 2023.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad