HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 24, 2023

ITA WAASWA KUFANYA TAFITI ZINAZOTATUA CHANGAMOTO ZA MIFUMO YA UKUSANYAJI KODI


 Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, akizungumza wakati wa Mahafali ya 16 ya Chuo Cha Kodi(ITA) yaliyofanyika leo Novemba 24, 2023 jijini Dar es Salaam.


NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande (Mb), amekiagiza Chuo cha Kodi (ITA) kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitatoa suluhisho la ya changamoto zinazoukabili mfumo wa ukusanyaji kodi hapa nchini.

Ameyasema hayo leo Novemba 24, 2023 wakati wa mahafali ya Chuo Cha Kodi ya 16 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, amesema tafiti hizo pia ziibue vyanzo vipya vya mapato, namna bora ya kudhibiti ukwepaji kodi pamoja na kurahisisha ulipaji kodi uwe rahisi na rafiki kwa kuzingatia teknolojia za kisasa zilizopo duniani.

Chande amesema utozaji kodi na ukusanyaji wa mapato ni mambo yanayohusu wadau wengi, kuanzia watunga sera, watozaji kodi hadi walipakodi wenyewe.

“Hivyo Mamlaka ya Mapato ina wajibu wa kukisaidia Chuo kupanua wigo wa kutoa mafunzo kwa wadau wengine ili nchi ipate wataalamu waadilifu wa kutosha wa masuala ya kodi na ipate walipakodi wazalendo ambao wanatambua wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi sahihi, kwa hiari na kwa wakati.” Amesema Chande.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inathamini mchango ambao TRA inaoutoa katika juhudi za Serikali za kukuza mapato ya ndani na iko tayari kusaidia ili TRA ikiwezeshe Chuo kufanikisha majukumu na malengo yake.

Aidha, amewasihi kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kuweza kubadilishana ujuzi, uzoefu na taarifa katika nyanja za forodha, kodi na tafiti mbalimbali za maeneo haya.

Chande amewapongeza wahitimu 508, ambao 293 ni wa kiume na 215 ni wa kike waliotunukiwa vyeti mbalimbali chuoni hapo na kuwasihi kutumia ujuzi na maarifa waliyopata kwa faida ya Taifa kwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa kodi au kwa kuwasaidia walipakodi watimize wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo cha Kodi, Prof. Isaya Jairo, amesema kuwa udahili kwa wanafunzi ambao ni wafanyakazi wa TRA umekuwa ukiongezeka kila mwaka tangu Chuo kipate Ithibati mwaka 2007 udahili wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania umeongezeka kutoka wanafunzi 974 mwaka 2008/2009 hadi kufikia wanafunzi 1,766 mwaka 2022/2023.

Ameongeza kuwa Chuo kimendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, ambapo kimehuisha makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Kodi-International Bureau of Fiscal Documentation (IBFD), na kuendeleza ushirikiano na Mtandao wa Kimataifa wa Vyuo Vikuu vinavyotoa mafunzo ya Forodha.

Akiipongeza Serikali Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Cha Kodi, Dkt. Samwel Werema, amema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya elimu nchini na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi.

Dkt. Werema amesema kuwa Katika muktadha huo, Chuo kitaendelea kubuni mafunzo mbalimbali kwa ajili ya wadau wa Mamlaka ambayo yanaendana na matarajio ya Serikali pamoja na mabadiliko ya kiuchumi Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande pia aliwatunuku vyeti wahitimu hao pamoja na kugawa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi ya wengine.


Baadhi ya wahitimu wa Mahafali ya 16.
Picha ya Pamoja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad