HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 17, 2023

CMSA YAIDHINISHA MAUZO YA HISA ZA UPENDELEO ZA TCCIA INVESTMENT PLC, KUKUSANYA BILIONI 10.58/-

 

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imefungua Mauzo ya hisa za upendeleo za TCCIA Investment Plc kwenye soko la awali ambapo TCCIA Investment Plc inatarajia kukusanya kiasi cha Sh.bilioni 10.58.

Aidha Mamlaka hiyo imeeleza fedha zitakazopatikana kupitia mauzo hayo zitaiwezesha TCCIA Investment Plc kukuza uwekezaji wake katika dhamana mbalimbali za masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika hisa za kampuni, hatifungani na vipande katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja hapa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC).

Hayo yamesemwa Novemba 16, 2023 jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya uzinduzi wa mauzo ya hisa za upendeleo za kampuni ya TCCIA Investment Plc.

Wakati anaanza kuzungumza CPA Mkama amewaambia wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo kuwa mauzo ya hisa za upendeleo za kampuni ya TCCIA Investment Plc ni muhimu katika maendeleo na ustawi wa kampuni ya TCCIA Plc, sekta ya fedha na uchumi hapa nchini.

"Kuhudhuria kwenu ni uthibitisho kwamba kampuni ya TCCIA ina wadau wengi wanaounga mkono juhudi za kukuza mtaji na shughuli za kampuni, na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha hususani masoko ya mitaji, na uchumi kwa ujumla hapa nchini.

"Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ina jukumu la kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji ili kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharamia shughuli za maendeleo."

Amefafanua kadri Taifa letu linavyosonga mbele katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/2026 wenye dhima ya kujenga Uchumi Shindani kwa Maendeleo ya Watu, mahitaji ya rasilimali fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo na miundombinu yanaongezeka.

Amesema ili kufanikisha azma hiyo kunahitajika uwepo wa bidhaa bunifu ambazo zinaleta anuwai katika masoko ya fedha, ikiwa ni pamoja na hisa za upendeleo kama hizi za TCCIA Investment Plc.

Aidha, uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya mitaji unachangia utekelezaji wa Sera za Fedha katika Uchumi na Sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuongezeka kwa akiba hapa nchini, kupanuka kwa uwekezaji unaoleta ongezeko la ajira, Mapato kwa njia ya kodi kwa Serikali na kuinua kipato cha watanzania kwa ujumla.

"Novemba 3, 2023 CMSA) iliidhinisha Waraka wa Matarajio wa TCCIA Investment Plc kuuza hisa za upendeleo 72,957,660 kwa wanahisa wake kwa bei ya Shilingi 145 kwa kila hisa katika uwiano wa hisa moja mpya kwa kila hisa moja aliyonayo mwekezaji kwa sasa.

"Idhini imetolewa na CMSA baada ya TCCIA Investment Plc kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hisa za Upendeleo yaani “Capital Markets and Securities (The Capitalisation and Right Issues), Regulations 2000”.

"Kwa mantiki hii mauzo ya hisa za upendeleo za TCCIA Investment Plc yamekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Masoko ya Mitaji.Mchakato wa kuidhinisha mauzo ya hisa unahusisha taasisi na wataalam mbalimbali."

CPA Mkama amesema kazi hiyo haikuwa ndogo na rahisi lakini wameweza kufanya kazi yao vizuri na kufanikisha hatua hii kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa, na hivyo kupata idhini kutoka CMSA.

Akifafanua zaidi amesema masoko ya mitaji huchochea maendeleo ya uchumi kwa kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha na kuimarisha utawala bora na hivyo kuleta tija kwa kampuni na taasisi.

Ameongeza CMSA itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuuza hisa kwa umma, hatifungani za miundombinu.

Pia hatifungani rafiki wa mazingira, hatifungani za bluu, hatifungani za jamii na hatifungani za taasisi za Serikali huku akitoa rai kwa kampuni na taasisi katika sekta binafsi na umma kutumia fursa katika masoko ya mitaji kupata fedha za kugharamia shughuli za kibiashara na miradi ya maendeleo.

Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA Nicodemus Mkama (kulia) akizindua mauzo ya hisa za upendeleo za kampuni ya TCCIA Investment Plc. kwenye hafla iliyofanyika jana jijini Dar es SalaamNo comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad