HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 27, 2023

UWT KUFANYA VIKAO VYAKE VISIWANI ZANZIBAR, WAANDAA TUKIO KUBWA KUMPONGEZA RAIS MWINYI

*Kamati ya Utekelezaji wabariki Serikali kusaini uendelezaji bandari Dar

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania( UWT) Jokate Mwegelo amesema kwa mara ya kwanza vikao vya UWT Taifa vinatarajia kufanyika Visiwani Zanzibar.

Mbali ya kufanyika vikao hivyo pia Novemba 4 mwaka huu watarajia kufanya tukio kubwa la kihistoria la kumpongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa na nzuri ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

Jokate amesema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na wana UWT kuhusu ziara iliyofanywa na Kamati ya Utekelezaji chini ya Mwenyekiti wa UWT Mary Chatanda ya ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mikoa mbalimbali nchini.

"Jumuiya ya Wanawake Tanzania tunatarajia kwenda kufanya vikao vyetu visiwani Zanzibar na Novemba 4 mwaka huu tutakuwa na tukio kubwa la kihistoria kwa ajili ya kumpongeza Rais Dk.Mwinyi kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

"Tunawakaribisha wanawake wote kushiriki katika tukio hilo ambalo litahusisha makundi ya wanawake mbalimbali.Pia tutakuwa na wasanii watakaonogesha siku hiyo wakiongozwa na mwanadada Zuchu."

Jokate amesema katika uongozi wa miaka mitatu ya Rais Dk.Mwinyi wote ni mashahidi kazi kubwa imefanyika na hiyo inatokana na uongozi mzuri wake mzuri.

Aidha Jokate ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba UWT wanaipongeza Serikali kwa hatua ya kusaini mikataba ya uendeshaji na uwekezaji wa bandari kwa kuamini ni yenye tija na italeta matokeo makubwa kwenye uchumi.

"Tunaipongeza Serikali kwa kusaini mkataba wa uendeshaji bandari ya Dar es Salaam , tunaamini mikataba hiyo itasaidia nchi kukua kiuchumi, kijamii, kibiashara na kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri ya Tanzania nan chi za Falme za Kiarabu, " amesema Jokate.

Amesisitiza Kamati ya utekelezaji UWT imepongeza hatua za Serikali ya awamu ya sita kwa kusaini mikataba ya uendeshaji na uwekezaji wa bandari tunaamini ni yenye tija na italeta maendeleo makubwa ya kukua katika sekta ya uchumi.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa WUT amesema Kamati ya utekelezaji imeendelea kuhimiza wanawake na wananchi kwa ujumla walionufaika na mikopo ya asilimia 10 ya fedha zilizotengwa na Halmashauri za Wilaya kuirejesha kwa wakati ili kutoa fursa kwa walengwa wengine kunufaika.

Aidha amesema Kamati ya utekelezaji inawakumbusha wazazi na walezi kuwajibika katika malezi bora kwa watoto kwa lengo la kukabiliana na mmomonyoko wa maadili hususani ukatili kwa wanawake na watoto ambayo imekuwa changamoto kubwa katika jamii ya Watanzania

Pia Jokate amesema UWT inawahamasisha wanachama na wananchi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ili muda utakapofika wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Kuhusu ziara iliyofanywa na jumuiya hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Mary Chatanda, Jokae amesema imeleta mafanikio makubwa kwa UWT kwani kupitia ziara hiyo imeongeza wanachama wapya 514,032.

Ameongeza kupitia ziara hiyo jumla ya mikutano ya hadhara 737 iliyofanyika katika Wilaya 62 na miradi 1,284 imekaguliwa katika mikoa 10 huku akifafanua katika ziara hiyo wamebaini changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya vijiji kutofikiwa na huduma za umeme.

Changamoto nyingine ni baadhi ya miradi kutokamilika kwa wakati hususani shule na zahanati, upungufu wa watumishi katika baadhi ya sekta kama elimu na afyana uhaba wa maji safi na salama kwa baadhi ya vijiji.

Kutokana na changamoto ambazo wameziona Kamati ya Utekelezaji UWT chini ya Mwenyekiti wake Mary Chatanda imeielekeza sekta ya nishati kuhakikisha vijiji ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa wakati ili kukuza na kuendeleza shughuli za uchumi katika maeneo husika.

"Kamati ya utekelezaji UWT inaelekeza viongozi wote wasimamizi katika sekta zenye changamoto husika kushughulikia kwa haraka katika kutatua changamoto hizo."

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad