Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo
******
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa, Askari mgambo pamoja na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum mkoani Mara hususani katika kanda maalum ya Tarime Rorya kwenye bonde la mto Mara.
Operesheni hii, iliyofanyika kuanzia tarehe 02 hadi 08 Oktoba, 2023, imefanikisha uteketezaji wa jumla ya hekari 807 za mashamba ya bangi, ukamataji wa gunia 507 za bangi kavu iliyo tayari kusafirishwa, gunia 50 za mbegu za bangi pamoja na kuteketeza viwanda viwili vidogo vilivyokuwa vikitumika kuchakata na kufunga bangi kabla ya kusafirishwa ambapo watuhumiwa 11 wanashikiliwa kuhusika na dawa hizo.
Akizungumzia tukio hilo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, wakazi wa eneo hilo wamelifanya bonde la mto Mara kama eneo maalum kwa ajili ya kilimo cha bangi na kujimilikisha kwa kutoruhusu mtu yeyote asiye mkazi kuingia kwenye bonde kama sehemu ya kuficha uharifu wao na wametishia kumdhuru yoyote atakayeingia ndani ya bonde hilo bila ridhaa yao. Pia, wamediriki kufunga ofisi ya kijiji wakimtuhumu mtendaji wa kijiji cha Nkerege kutounga mkono kilimo cha bangi.
‘‘Kitendo kinachofanywa na wananchi waliopo katika eneo la mto Mara ni kinyume kabisa na sheria, viongozi wa serikali na wananchi ambao sio wakazi wa hapa hawaruhusiwi kabisa kuingia eneo la bonde. Uwepo wa daraja lililopo katika moja wapo ya vijito vinavyopeleka maji mto Mara, linatumika kama kizuizi cha watu kwenda kwenye hifadhi ya bonde la mto maeneo yanayolimwa bangi. Ili mtu avuke anatakiwa kujieleza nia na madhumuni ya kuvuka kuelekea upande wa pili, na wahusika wasiporidhika na maelezo hawakuruhusu kuendelea na safari’’ ,amesema Lyimo.
Ameongeza kuwa, baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa vijiji vinavyopakana na bonde hilo pamoja na wananchi waliojimilikisha bonde hilo muhimu kwa uchumi wa taifa, wamekuwa wakikodisha na kuuza mashamba ya kulima bangi ndani ya hifadhi ya bonde hilo.
Aidha, kutokana na mto Mara kuwa muhimu sana katika ikolojia ya mbuga ya Serengeti, Kamishna Jenerali Lyimo ameomba Wizara zinazohusika kushirikiana na Mamlaka kutokomeza kilimo cha bangi katika eneo hilo, kwani mbali na operesheni iliyofanyika bado mashamba ya bangi ni mengi pembezoni mwa mto na wananchi wamekuwa wakitumia maji ya mto kumwagilia.
‘‘Tukiacha kilimo cha bangi kiendelee hivi, na kuwaacha wananchi waendelee kuchepusha maji ya mto kumwagilia bangi mwisho wa siku itaharibu ikolojia katika mbuga ya Serengeti na mto kwa ujumla. Ni vema tukashirikiana kuhakikisha eneo hili linasimamiwa vema ili kufanikisha kusitishwa kwa kilimo cha bangi”, amesisitiza Lyimo.
Sambamba na hilo, amewataka viongozi wa serikali za mitaa waliotoroka kuwa sehemu ya mapambano ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha kwamba, wanakomesha kilimo cha bangi watakaporejea.
Pia, Kamishna Lyimo amesema, Mamlaka kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mara na uongozi wa wilaya ya Tarime, watafanya mikutano ya hadhara na kufikiria kuwa na mipango kabambe kuona ni namna gani bonde litalindwa dhidi ya kilimo cha bangi na uhalifu mwingine.
‘‘Sisi kama Mamlaka tutafanya operesheni endelevu katika maeneo haya kuhakikisha kilimo cha bangi kinaisha. Bonde hili lina rutuba nyingi na linakubali mazao ya aina zote, hivyo tumekubaliana na mkuu wa mkoa wa Mara kuwa na mikakati ya kusimamia bonde ili kumaliza kilimo cha bangi na kutafutwa kwa shughuli nyingine ambayo itakuwa rafiki’,’ amesema Lyimo.
Naye diwani wa kata ya Tulwa Mheshimiwa Chacha Machugu amesema, viongozi wa serikali za mitaa wanaosaidia kuendelea kwa kilimo cha bangi wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine. Aidha, amewaomba viongozi wa dini kusaidia kuwaambia waumini wao kuwa dawa za kulevya hazitakiwi.
‘‘Tutashirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha bangi hailimwi Tarime na yeyote atakaye kiuka miongozo na sheria za nchi atawajibishwa kwani sote tunaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.
Magreth Ally mkazi wa Tarime amesema kuwa, vijana wengi wanalima bangi kwa madai ya kupata fedha kwa haraka. Hivyo, ameiomba serikali kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kuelekeza na kuwezesha kilimo cha mazao mbadala ili kuepusha kurithishana kilimo cha bangi kama njia pekee ya kujipatia kipato kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Akizungumzia operesheni iliyofanyika, Isaya Banda mkazi wa Tarime, ameiomba serikali kufanya operesheni endelevu katika maeneo yote ili kutokomeza bangi kwani vijana wengi wameathirika na matumizi ya dawa hizo. Pia, amewaomba wananchi kuwafichua wanaojihusisha na kilimo na biashara ya bangi.
Kwa upande mwingine Chacha Michael mkazi wa kijiji cha Nkerege ambako operesheni hii imefanyika, ametoa msimamo wake juu ya kilimo cha bangi kwa kusema; “Hili zao linatuharibia sana vijana wetu, wanaacha kusoma wanaenda kuvuta bangi, vilevile tunauomba uongozi wa mama Samia zoezi hili liwe endelevu kwa sababu hapa mto Mara kilimo cha bangi kimekithiri sana. Kuna mazao mengi ya kulima ukapata hela kila zao linakubali hapa Tarime lakini wengi wamekimbilia bangi, mimi sikubaliani nalo kabisa”, amebainisha Chacha.
Operesheni iliyofanyika mkoani Mara ni mwendelezo wa operesheni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini kama moja ya hatua za muhimu katika kupunguza upatikanaji na usambazaji wa dawa za kulevya hapa Nchini.
No comments:
Post a Comment