HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 11, 2023

Waziri Gwajima: Wajasiriamali wanawake na vijana changamkieni fursa za IMBEJU

Dar es Salaam. Tarehe 11 Septemba 2023: Akizindua Maonesho ya Imbeju ya Wajasiriamali Ilala 2023, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima amewahimiza wafanyabiashara wadogo nchini hasa wanawake na vijana kuchangamkia fursa ya mafunzo, ushauri, na mitaji wezeshi inayotolewa na CRDB Bank Foundation kupitia program ya IMBEJU.

Waziri Gwajima amesema wanawake na vijana ndio injini ya uchumi wa taifa kwani ni kundi lenye uwezo mkubwa wa kuchangia mafanikio ya kijamii na kiuchumi. Hata ripoti ya Sensa na Makazi ya mwaka 2022, amesema inadhihirisha hilo ikibainisha kuwa asilimia 51 ya watu wote nchini ni wanawake na asilimia 75 ni vijana hivyo makundi haya mawili kuwa sehemu muhimu ya nguvukazi ya taifa.
“Hata hivyo, wanawake na vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo mila na desturi kandamizi, elimu duni, ukosefu wa mitaji na stadi za ujasiriamali. Serikali imechukua hatua mbalimbali zinazolenga kujenga uchumi jumuishi na shirikishi ili kuwakomboa kiuchumi, ni wakati sasa wa kila mjasiriamali mdogo kuzitumia fursa zinazotolewa na CRDB Bank Foundation na Benki ya CRDB kwani mkizitumia vizuri, itakuwa rahisi kukabiliana na changamoto hizi na kukuza biashara zenu,” amesema Waziri Gwajima. 

Vilevile, Waziri amesema Serikali inafanya kazi usiku na mchana kuwawezesha wanawake kiuchumi hivyo inaendelea kutekeleza mkakati wa kutimiza malengo ya Jukwaa la Kimataifa ya Kukuza usawa wa Kijinsia hususan katika Haki na Usawa wa Kiuchumi.

Uwezeshaji wa wanawake na vijana, amesema ni suala linalotiliwa mkazo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050, na Sera ya Maendeleo na Jinsia ya Mwaka 2000. 
Maonesho hayo ya wajasiriamali yanayofanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Septemba 11 mpaka 13 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja yameandaliwa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Wilaya ya Ilala yakiwakusanya zaidi ya wajasiriamali 3,000 wa halmashauri hiyo, Jiji la Dar es Salaam na Tanzania nzima kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema benki inathamini shughuli za kijasiriamali kwa kutambua kuwa zimekuwa msaada mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa. 
“Tunaamini ili sekta hii itoe mchango wake kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa, kunahitajika huduma na mifumo shirikishi itakayowawezesha wajasiriamali kutimiza malengo yao. Imani hii ndio iliyoishawishi Benki yetu ya CRDB kuanzisha kitengo maalum kwa ajili ya kuhudumia wateja wa kundi hili tangu mwaka 2005,” amesema Nsekela.

Kutokana na jitihada hizo, amesema Benki ya CRDB imekuwa kinara katika uwezeshaji wajasiriamali kwani hadi robo ya pili mwaka huu imetoa mikopo ya zaidi ya Shilingi trilioni 3.4 kwa wajasiriamali 200,000 huku wajasiriamali wengine 50,000 wakinufaika na mafunzo yaliyotolewa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema juhudi za kuwajengea ujasiri wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo pia yanazihusisha mamlaka nyingine za Serikalina sekta binafsi ikiwamo TRA, BRELA, SIDO, VETA, NHIF, NIDA, Wakala wa Ununuzi Serikalini (PPRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), kampuni ya GS1, NSSF, Shirika la Bima la Taifa (NIC) huku Benki ya CRDB ikiwapa elimu ya fedha na fursa za mikopo ilizonazo.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema maonesho hayo ni mwanzo wa safari endelevu ya kuwapa wajasiriamali nchini fursa ya kuonyesha biadhaa zao hivyo kunufaika na soko kubwa la ndani na watakapokuwa tayari watoke nje ya mipaka ya Tanzania.
“Maonesho haya ni sehemu ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa wajasiriamali wetu kwa kuwatengenezea masoko ya huduma na bidhaa zao kupitia programu yetu ya IMBEJU. Katika maonesho wajaisiriamali wanawake na vijana wamepata fursa ya kuonesha huduma na bidhaa zao bure bila kuingia gharama zozote za maonesho. Niwakaribishe watanzania kuwaunga mkono wajasiriamali wetu ili waweze kuku, jambo ambalo litachochea ukuaji wa uchumia wa Taifa letu,” amesema Tully.

Tully amesema hadi sasa, IMBEJU imewafikia zaidi ya biashara changa za vijana 700 kupitia program shindani, na zaidi ya wanawake wajasiriamali 100,000. Kwa upande wa mitaji wezeshi CRDB Bank Foundation imeshatoa Shilingi milioni 250 kwa wajasiriamali kwa zaidi ya 100, na leo hii imekabidhi mitaji wezeshi ya pikipiki 9 na bajaji 4 kwa wajasiriamali wanawake. Aliongezea kuwa zoezi la kutoa mitaji wezeshi linaendelea nchi nzima na kuwa Shilingi bilioni 5 zimetengwa. 
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Martin Warioba alimhakikishia Waziri Gwajima kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha wajasiriamali wanawake na vijana ili kujenga uchumi jumuishi ambao watu wote wanafursa ya kushiriki na kufaniki. “Nikuahidi Mheshimiwa Waziri huu ni mwanzo tu, malengo yetu ni kuyafanya maonesho haya kuwa endelevu hapa Wilaya ya Ilala, lakini matarajio yetu ni kwanda nchi nzima,” amesema.

















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad