HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, September 16, 2023

RAIS SAMIA AFURAHISHWA UTENDAJI KAZI BANDARI YA MTWARA,AAHIDI KUONGEZA BAJETI KUBORESHA MIUNDOMBINU

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na ufanisi wa kiutendaji katika Bandari ya Mtwara hasa baada ya maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika Bandari hiyo.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Maboresho wa Bandari hiyo, Rais Dkt. Samia amesema Maboresho makubwa yaliofanyika Bandarini hapo yameleta ufanisi zaidi na kuufungua Kiuchumi Mkoa wa Mtwara na Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Ameongeza kuwa Serikali yake itaendelea kuongeza Bajeti ya kuboresha miundombinu ya Bandari ili kuvutia zaidi Wateja, Wadau Wafanyabiashara wa Usafirishaji kuzitumia Bandari zetu.

Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema Serikali yake imejiandaa kusafirisha korosho kupitia Bandari ya Mtwara, hivyo ametoa wito kwa Wananchi kujiandaa kuiunga mkono Serikali kwa kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za Bandari.

Rais Dkt. Samia pia ametoa rai kwa Watumishi wa Bandari ya Mtwara kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili Bandari hiyo ifikie kiwango cha Bandari ya Dar es Salaam.

Miradi iliyotekelezwa kama sehemu ya maboresho ya utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara ni pamoja na ujenzi wa Gati moja la nyongeza lenye urefu ww mita 300, ujenzi wa mita ya kupimia mafuta ili kuhakikisha mafuta yanayoshushwa katika Bandari ya Mtwara yanapimwa, ujenzi wa sehemu ya kuhifadhi Makasha na ukarabati wa ghala na vifaa vya kuhudumia mizigo Bandarini.

Katika mwaka wa Fedha wa 2022/2023 TPA kupitia Bandari zake zote Nchini imehudumia Jumla ya Shehena Tani Milioni 24.899 ambapo Bandari ya Dar es Salaam ni Kinara kwa kuhudumia Shehena Tani Milioni 21.461 ikifuatiwa na Bandari ya Mtwara iliyohudumia Shehena Tani Milioni 1.62.

📍Bandari ya Mtwara

🗓️ 15 Septemba,2023




 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad