Na Albano Midelo,Namtumbo
SEKONDARI ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyojengwa
katika kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma kwa gharama
ya shilingi bilioni nne imeanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano.
Mkuu wa Shule hiyo Mwl.Dafrosa Chilumba amesema ili kutekeleza mradi
wa ujenzi wa sekondari hiyo serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika awamu ya kwanza ilitoa shilingi
bilioni tatu.
Ameyataja majengo ambayo yalijengwa katika awamu ya kwanza ya
ujenzi ulianza Aprili 2022 kuwa ni ujenzi wa jengo moja la
utawala,madarasa 12 na maabara nne za Jiografia,Kemia,Fizikia na
Biolojia.
Majengo mengine ameyataja kuwa ni nyumba mbili za walimu zenye
uwezo wa kuchukua familia tatu,mabweni Matano yenye uwezo wa
kuchukua wanafunzi 120 kila bweni,mfumo wa maji safi wenye matanki
mawili na mitaro yenye urefu wa mita 1050,vyoo matundu 16,bwalo kubwa
la chakula,chumba cha jenereta,njia za kutembea na uzio.
Hata hivyo amesema utekelezaji wa ujenzi katika awamu ya kwanza
umefikia zaidi ya asilimia 95 na kwamba serikali imeleta shilingi bilioni 1.1
kuanza kutekeleza mradi kwa awamu ya pili.
Ameitaja miundombinu ambayo inajengwa katika awamu ya pili kuwa ni
ujenzi wa madarasa kumi,nyumba mbili za walimu zenye uwezo wa
kuchukua familia nne,jengo la TEHAMA, maktaba,mabweni manne yenye
uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kila moja.
“Wanafunzi wa kidato cha tano ambao tumepangiwa na serikali kuanza
masomo ni 249 wengi wameshafika,wanafunzi hao wanasoma michepuo
mitano ,wanafunzi wanafurahia mazingira ya kuvutia yenye huduma zote
muhimu,walimu wapo wa kutosha,hakuna mwanafunzi anayewaza
kuhama’’,alisisitiza.
Stella Magaho ni Mwanafunzi wa Kidato cha Tano katika sekondari ya
Wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan mchepuo wa PCB amesema
wanafunzi walioripoti katika shule hiyo wanafurahia mazingira rafiki ya
kusoma na kwamba hakuna changamoto yoyote .
Mwanafunzi huyo ambaye ni Kiranja Mkuu kwa niaba ya wenzake
anaishukuru serikali kwa kuwajengea sekondari bora kwa Watoto wa kike
ambapo ameahidi watafanya vizuri katika masomo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema sekondari ya
wasichana ya Namtumbo ni miongoni wa sekondari mpya 11 ambazo Rais
Dkt.Samia ametoa zaidi ya shilingi bilioni 7.7. kujenga sekondari hizo
mkoani Ruvuma katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Kanali Thomas amezitaja shule hizo mpya kuwa zimejengwa katika
Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma na kwamba shule
zimejengwa kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari nchini
(SEQUIP).
Hata hivyo amesema katika Halmashauri ya Tunduru zimejengwa shule
tatu za sekondari kupitia mradi wa SEQUIP na kwamba katika Halmashari
ya Namtumbo pia zimejengwa shule mbili ikiwemo shule ya wasichana ya
Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Deogratias
Ndejembi amesema serikali ya Awamu ya sita katika mwaka 2022/2023
imetoa zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za
sekondari 176 za kata kupitia program ya SEUIP.
“Fedha hizo zimetolewa kujenga shule za sekondari za kata katika kata
zisizo na shule na kata zenye wanafunzi wengi zaidi ukilinganisha na
miundombinu ya shule zilizopo’’,alisisitiza Ndejembi.
Hata hivyo amesema katika Mkoa wa Ruvuma kupitia program hiyo mwaka
huu,serikali imetoa shilingi bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya
saba za sekondari za kata.
Sekondari ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyopo Namtumbo
mkoani Ruvuma ni miongoni mwa sekondari kumi mpya za wasichana za
mikoa zilizojengwa na serikali ya Awamu ya Sita.
Baadhi ya majengo ya sekondari mpya ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akiwa ofisini kwake mjini Songea.
Mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyopo kata ya Rwinga wilaya ya Namtumbo mkoanii Ruvuma ambayo serikali imetoa shilingi bilioni nne kujenga shule hiyo iliyoanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu.
Stella Magaho mwanafunzi wa kidato cha tano sekondari ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ameanza masomo hivi karibuni.
Jengo la utawala na madarasa katika shule ya sekondari ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment