HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 4, 2023

RUWASA YATUMIA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 2.5 KUTEKELEZA MIRADI MITATU YA MAJI MBINGA

 

Na Albano Midelo,Mbinga

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma imetumia zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kutekeleza
miradi mitatu ya maji.

Meneja wa RUWASA wilayani Mbinga Mhandisi Mashaka Sinkala ameitaja
miradi hiyo kuwa ni Pamoja na mradi wa maji Kitai ambao hadi kukamilika
unatarajia kutumia shilingi milioni 560.

Amesema mradi huo utahudumia jumla ya wakazi 1,468 kati yao wakazi
1,204 wanatoka katika Gereza la Kitai,shule ya msingi Kitai na zahanati ya
Kitai na kwamba wakazi 264 wanatoka katika kitongoji cha Ngembambili.

Mhandisi Sinkala ameutaja mradi mwingine ambao unatekelezwa na
RUWASA kuwa ni mradi wa maji kata ya Matiri ambao unagharimu zaidi ya
shilingi bilioni 1.4

Ameutaja mradi wa maji Matiri kuwa unahusisha vijiji vya Matiri na Kiyaha
na kwamba mradi unatarajia kuhudumia wakazi zaidi ya 9870.

Hata hivyo amesema mradi huo hadi sasa umefikia asilimia 60 ya
utekelezaji na unatarajia kukamilika Novemba 17 mwaka huu ambapo
amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza adha kubwa ya
upatikanaji wa maji iliyokuwepo kabla ya kuanza kutekelezwa mradi huo.

“Wananchi wa Matiri kwa muda mrefu wamekuwa wanasumbuliwa na
magonjwa ya milipuko kutokana na kutumia maji ambayo sio salama,mradi
huu pia utasaidia watu kupata muda mwingi wa kushughulika na kazi
zingine za kiuchumi kwa kuwa maji yatakuwa karibu na makazi’’,alisisitiza.

Mradi mwingine ambao unatekelezwa na RUWASA wilayani Mbinga
kulingana na Meneja huyo ni mradi wa maji Kitanda unaohusisha vijiji vya
Kitanda na Magwangala na kwamba mradi unatarajia kuhudumia jumla ya
wakazi 3,600.

Amesema mradi huo unatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 473 na
kwamba mradi umekamilika kwa asilimia 100 na unakwenda kupunguza
adha kubwa ya upatikanaji wa maji kwenye vijiji husika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RUWASA
Tanzania Mhandisi Ruth Koya ameitaja azma ya Rais Dkt Samia Suluhu


Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani inakwenda kutimia miaka
michache ijayo.

Amesema anaamini kufikia mwaka 2025 asilimia 85 ya wananchi
wanaoishi maeneo ya vijijini watakuwa wanapata maji safi na salama.
Ameiagiza Menejimenti ya RUWASA kuhakikisha kwamba wakandarasi
wanaoidai serikali fedha walipwe mara moja kwa kuwa serikali imeshatoa
fedha za kutekeleza miradi hiyo kilichobakia ni taratibu za kuwalipa
zikamilike haraka ili wakandarasi wakamilishe kazi zao.

Kaimu Mkurugenzi wa RUWASA Bwai Biseko amesema RUWASA haitaki
kujisifia kwa kuhesabu miradi mingapi imetekelezwa badala yake
wanapenda kuona namna walivyowagusa wananchi kuhakikisha mradi
umekamilika na wananchi wanapata huduma.

Stella Mhagama Mkazi wa Matiri amesema anamshukuru Rais Samia kwa
kutoa fedha za kutekeleza mradi huo ambapo amesema kwa miaka mingi
wanawake na Watoto wamekuwa wanapata kero ya kusafiri kilometa nne
kufuata maji mtoni na kubeba kichwani.

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan
imetoa zaidi ya shilingi bilioni 58 katika Mkoa wa Ruvuma kutekeleza miradi 36 ya maji hadi kufikia Juni 30 mwaka huu.

Mradi wa maji katika kijiji cha Kitai  wilaya ya Mbinga unaogharimu shilingi milioni 560  ambao umeanza kuwanufaisha  wananchi wanaozunguka eneo la Gereza la Kitai.Pichani  kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RUWASA Mhandisi Ruth Koya alipokagua mradi wa majji Kitai hivi karibuni akimtiwsha maji mmoja wa akinamama katika kijiji hicho.
Mradi wa maji wa kata ya Matiri wilayani Mbinga  unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.4 ,mradi huo unatarajia kukamilika Novemba mwaka huu.
Mradi wa maji katika kijiji cha Kitanda wilayani Mbinga mkoani Ruvuma ambao unagharimu shilingi  473 ambao umekamilika kwa asilimia 100.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad