HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 25, 2023

MHE. KAIRUKI ASISITIZA VYOMBO VYA HABARI KUTANGAZA UTALII DUNIANI




Na John Mapepele


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amevitaka Vyombo Vya Habari kutangaza vivutio vya utalii ili watalii wengi waweze kuvifahamu na kuja nchini hatimaye kuinua uchumi wa nchi yetu.


Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea Televisheni ya TBC jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Kituo hicho kabla ya kufanya kipindi maalum kwa ajili ya kutoa ujumbe maalum wa Tanzania katika maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani ambapo kauli mbiu ya siku hiyo kwa mwaka huo ni Utalii na Uwekezaji Unaojali Mazingira.


Aidha, amelitaka Shirika la Utangazaji Tanzania TBC kupitia chaneli yake ya utalii ya “Safari Channel” kufanya tafiti za kuboresha matangazo vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali duniani na kujifunza kwa nchi zenye teknolojia ya juu ya utangazaji wa vivutio hivyo ili iweze kutangaza vivutio vya utalii duniani.




“Ninawataka mtoke mwende duniani mkajifunze wenzetu wanaendeshaje chaneli za utalii ili na sisi tuweze kuendesha kituo chetu vizuri zaidi kiweze kutangaza vivutio vyetu vya utalii duniani na kutuletea wageni wengi zaidi” amefafanua Mhe. Kairuki



Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa tunatangaza vivutio vya utalii watu wengi waweze kufahamu hazina ya vivutio vya Tanzania tulivyonavyo ili waweze kuja kutembelea na kuliingizia taifa mapato zaidi.




Aidha, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini kusimamia Sekta za Maliasili na Utalii na kumhakikishia kuwa ataendelea kushirikiana na menejimenti ya wizara yake na wadau mbalimbali kutekeleza maono ya Serikali na ya Mhe. Rais kutangaza utalii wa Tanzania.


Maazimisho ya Siku ya Utalii duniani yanafanyika jijini Riadhi Saudi Arabia ambapo Tanzania pia inashiriki.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad