Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Sept 19
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amezitaka, Shule za Msingi kuandaa wanafunzi ambao watashindana kwenye soko la kitaifa na kimataifa kwa faida ya Maisha yao baadae na kuzingatia utamaduni wa Kitanzania.
Aidha amewaasa wazazi na walezi, kuwa karibu na watoto wao kutokana na hali ya sasa ambayo dunia inaenda kasi na maendeleo ya teknolojia,na wasimamie maadili.
Koka aliyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa mahafali ya shule za msingi za Kibaha Independence School (KIPS), Anex na Msangani zote zilizopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Vilevile Koka, alisema sekta binafsi haina sababu ya kupuuzwa kwani inasaidia serikali kubeba jukumu la kutoa elimu ambapo hata Rais Samia Suluhu Hassan anasisitiza ushirikiano huo.
"Naipongeza familia ya Yusuph Mfinanga kwa kuwekeza kwenye sekta ya elimu kwa kuanzisha shule tatu za msingi na mbili za sekondari, kwa hakika wanasaidia serikali kuipunguzia mzigo kwa huduma ya elimu bora na kutoa ajira"alieleza Koka.
Nae Mkurugenzi wa Kampuni ya Njuweni Ltd, Alhaj Yusuph Mfinanga aliahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni tano kwa mwanafunzi atakayefaulu na kuongoza kitaifa kwenye mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutoka shule tatu zinazomilikiwa na kampuni hiyo.
Mfinanga alieleza ,atawasomesha bure wanafunzi 20 watakaofaulu masomo ya kumaliza elimu ya msingi na kupata alama za daraja A kwa masomo yote kwenye shule za sekondari za kampuni hiyo za Vuchama Islamic Secondary School na Mangio Secondary School zilizopo Mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake meneja wa KIPS Nuru Mfinanga alisema kuwa wanashirikiana vizuri na serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye sekta hiyo lengo likiwa ni kutoa elimu bora.
No comments:
Post a Comment