Na Munir Shemweta, WANMM LUDEWA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaelekeza watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha wanakuwa na kliniki za ardhi kama ilivyoelekezwa na wizara yake ili kutatua changamoto za sekta ya ardhi.
Dkt Mabula ametoa maelekezo hayo tarehe 11 Agosti 2023 wilayani Ludewa mkoa wa Njombe kufuatia kupokea malalamiko mbalimbali kuhusu changamoto za sekta ya ardhi katika mkutano wa hadhara akiwa katika ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe.
Katika mkutano huo, wananchi walimlalamikia waziri Mabula kuwa, wamekuwa wakipata usumbufu kutoka kwa watendaji wa sekta ya ardhi katika mambo mbalimbali yanayohusiana na sekta ya ardhi jambo linalowafanya kushindwa kupata huduma stahiki ikiwemo hati milki.
‘’Wananchi wengi katika wilaya ya Ludewa hatuna hati milki za ardhi, tukikosa hati miliki maisha yetu yako hatarini maana tunaweza kunyang’anywa viwanja wakati wowote’’ alisema mkazi wa Ludewa Cosmas Sanga
Mkazi mwingine Herman Luoga alisema, mbali na kupimiwa mashamba kwa ajili ya kupatiwa hati za kimila lakini pamoja na kufuatilia mara kwa mara ofisi za ardhi kwenye ofisi za ardhi katika halmashauri ya wilaya ya ludewa wameshindwa kupata majibu hadi sasa.
‘’Jambo ambalo ningependa watumishi wa sekta ya ardhi wafanye ni kuwa na klinik za ardhi ambazo wizara yake imeziekeleza kufanyika nchi nzima’’ alisema Waziri wa Ardhi Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kupitia klinik za ardhi watumishi wa sekta ya ardhi watatoka ofisini kwenda kwenye kata na kuweka vikao kwa ajili ya kusikiliza hoja, changamoto na kero za sekta ya ardhi kutoka kwa wananchi na wanaposikiliza lazima watoe majibu papo hapo kwa kuwa wao ndiyo wataalamu wa sekta hiyo.
Alisema, katika maeneo hayo wanaweza kukaa siku moja ama mbili kutegemeana na uhitaji wa eneo husika na kuongeza kuwa, kliniki hizo za ardhi zinatakiwa kuzungukia kata zote za halmashauri ambapo alisisitiza kuwa ya watendaji hao kabla ya kwenda eneo husika lazima watangaze ama kutoa taarifa mapema siku watakayokwenda.
‘’Kwa sababu wakati mwingine changamoto hakuna isipokuwa elimu, mtu haelewi kwa nini amiliki ardhi kwa nyaraka, mtu hajui akitaka kupimiwa aanzie wapi na mwingine amevamiwa katika eneo lake hajui afanye nini’’ alisema Dkt Mabula.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemaliza ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe ambapo alitembelea wilaya za Njombe, Makete pamoja na Ludewa ambapo mbali na kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi pamoja na wananchi wa wilaya hizo alikabidhi hati milki kwa wananchi waliokamilisha taratibu za kupatiwa hati.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wilayani Ludewa wakati wa ziara yake katika mkoa wa Njombe tarehe 11 Agosti 2023. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva na kushoto ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba.
Mkuu wa wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe Victoria Mwanziva akizungumza katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara ya Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula (kushoto) tarehe 11 Agosti 2023. Kulia ni Katibu Tawala wilaya ya Ludewa Gilbert Sandagila na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias.
Sehemu ya wananchi wa Ludewa mkoani Njombe wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula uliofanyika wilayani humo tarehe 11 Agosti 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimpongeza mmoja wa wananchi wa Ludewa aliowakabidhi hati katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake katika wilaya hiyo tarehe 11 Agosti 2023. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipokea zawadi ya mbuzi aliyopewa na wananchi wa Ludewa kama zawadi baada ya kufanya ziara katika wilaya hiyo tarehe 11 Agosti 2023. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsalimia mlemavu mara baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi wa Ludewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani humo tarehe 11 Agosti 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
No comments:
Post a Comment