Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani COREFA, Robert Munisi akizungumza mara baada ya kuthibitishwa na wajumbe kuwa Mwenyekiti
Mwenyekiti wa COREFA Robert Munisi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe waliomthibitisha ambao wametokea Mafia, Kibiti, Rufiji ,Chalinze,Mkuranga Bagamoyo.na Kibaha
Pichani ni baadhi ya wajumbe wa COREFA wakifuatilia neno kutoka kwa Mwenyekiti hayupo pichani.
Na Khadija Kalili, Michuzi Tv
CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), jana kwa kauli moja
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uliofanyika jana Agosti 13 2023 wamemthibitisha Robert Munisi kuwa Mwenyekiti wao kupitia mkutano huo ambao awali ulitakiwa uwe wa uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo ya Mwenyekiti
Munisi amethibitishwa baada ya mgombea mwenzake Hassan Othuman 'Hasanoo' kutangaza kujitoa kabla ya uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Msomi Kiomoni Kibamba amewaambia wajumbe kuwa, kulitakiwa kuwe na uchaguzi wa nafasi moja tu ya Mwenyekiti wa COREFA ambao ungewashirikisha wagombea wawili Hassan almaarufu kwa jina la 'Hassanoo' na Munisi lakini mgombea Hasanoo amejitoa kwa barua aliyoiwasilisha katika Kamati hiyo.
"Kwa kuwa mgombea ni mmoja na kwa mujibu wa kanuni ya 19, kanuni ndogo ya 8 ya kanuni ya uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mnachotakiwa kufanya hapa ni kumthibitisha tu huyu mgombea aliyepo mbele yenu je mnamthibisha ndugu Robert Munisi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani COREFA?" Wakili Msomi Kibamba amewauliza wajumbe wa mkutano huo na wote kwa pamoja wamemthibitisha.
Akijibu swali aliloulizwa na Michuzi Tv kuwa hivi sasa amekua akihodhi kofia mbili ambapo kabla ya kutwaa kiti cha Uenyekiti COREFA pia ni Mwenyekiti aliyechaguliwa kwa kupigiwa kura na Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kibaha (KIBAFA).
Munisi amesema kuwa ataendelea kushikilia kofia zote mbili huku akisema Katiba haijambana japo kwa hapo baadaaye anaweza kuachia kofia mojawapo ili aweze kutenda kazi kwa ufanisi zaidi.
Amesema kuwa anashukuru Mungu ndoto yake aliyokua akiiota zaidi ya miaka saba nyuma ya kuwa kiongozi wa COREFA , imetimia hivyo amewaomba Kamati tendaji ya COREFA , wajumbe wake na wadau wote wa soka ndani ya Mkoa wa Pwani kushirikiana ili kuweza kupeleka mbele soka la Mkoa wa Pwani ambao lilikua limedorora.
"Tunachopaswa kufanya kwa sasa ni kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha soka ndani ya Mkoa wa Pwani katika kila eneo inasonga mbele", amesema Munisi.
Mohammed Lacha ametangazwa kuwa Makamu Mwenyekiti COREFA huku nafasi ya Katibu COREFA ikibaki kwa Mohammed Masenga ambaye alikua katika nafasi hiyo kweye kipindi kilichopita.
Wakati huohuo Munisi amemtangaza Christina Mwagala kuwa Meneja Masoko COREFA ikumbukwe kuwa Christina alikua Msemaji Mkuu wa timu ya watoto wa Mjini Manispaa ya Kinondoni (KMC).
No comments:
Post a Comment