Naibu Waziri wa maji Maryprisca Mahundi akimtua Mama ndoo kichwani katika kata ya Oldonyosambu kitongoji cha Masusu Wilaya Ngorongoro.
Maryprisca Mahundi Naibu Waziri wa maji katikati,akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa maji katika kuhakikisha wanasimamia fedha zinazotolewa na wizara hiyo.
Moja ya tenki la maji ambalo litakuwa likishusha maji kwenye mabomba ili wananchi wapate maji ya uhakika.
Na Jane Edward, Arusha
SERIKALI kupitia wizara ya Maji inaendelea kutekeleza miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 19 ambazo zinalenga kutatua changamoto ya Maji ya muda mrefu iliyokuwa inawakabili Wananchi wa vitongoji na vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Ngorongoro.
Akizungumza katika ziara ya Naibu Waziri wa maji Maryprisca Mahundi alipotembelea moja ya miradi ya maji inayotekelezwa katika kata ya Oldonyosambu kitongoji cha Masusu Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Raymond Mangwala amesema ujio wa Naibu waziri huyo umekuwa Neema kwa wanakijiji hao.
Amesema fedha hizo zinalenga kutatua changamoto ya maji kwa kuzingatia kijiji hicho hakijawahi kuwa na maji toka kupatikana kwa Uhuru wa nchi ya Tanzania.
Aidha amesema kuwa katika Wilaya ya Ngorongoro miradi 25 iko katika mchakato wa kukamilika ili Wananchi wapate maji ya uhakika kwani Wananchi walikosa maji kwa muda mrefu .
Kwa upande wake Naibu Waziri wa maji Maryprisca Mahundi amesema fedha nyingi zimetumika katika mradi huo wa Masusu na kwamba kwa kuanza wamepata vichotea maji vichache lakini Serikali kupitia Wizara ya maji itahakikisha ukosefu wa maji unakuwa historia katika Wilaya hiyo.
"Sera ya maji inatutaka kutotembea umbali wa zaidi ya Kilometa 14 kutafuta maji na sisi tupo kuunga jitihada za Rais Samia kumtua Mama ndoo kichwani "Alisema
Amefafanua kuwa katika miradi hii inayotekelezwa na Serikali ya Rais Samia inapaswa itunzwe na wananchi na sio kuharibu miundombinu ya maji kwani itarudisha nyuma maendeleo ya upatikanaji wa maji.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo alitembelea miradi ya maji katika kata ya Sale,enguserosambu,magaiduru pamoja na kijiji cha Wasso ambapo huduma ya maji kwa Wilaya ya Ngorongoro inatajwa kufikia zaidi ya asilimia 72.
No comments:
Post a Comment