Rufiji. Tarehe 25 Agosti 2023: Baada ya Benki ya CRDB kufungua tawi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa amewakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania kuja kuwekeza kwenye fursa tele zilizopo wilayani Rufiji.
Mchengerwa amesema Rufiji ambayo ni kati ya wilaya kongwe nchini inazidi kukua kila siku kwa kuimarisha miundombinu ya huduma za jamii kwani tayari serikali imejenga zahanati 24, shule za msingi 45 na sekondari 9 ndani ya vijiji 38 ilivyonavyo zinazotoa nafasi kwa wananchi kutibiwa na watoto kupata elimu itakayowasaidia kujikomboa katika maisha yao hivyo ujio wa Benki ya CRDB inawaongezea fursa za kujiimarisha kiuchumi.
“Uamuzi wa serikali kujenga Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umeleta neema nyingi zitakazowanufaisha wananchi na halmashauri hii yenye utajiri mkubwa wa ardhi, maliasili na utamaduni. Ukiacha bwawa hili, kuna hekta 300,000 limetengwa kwa ajili ya kilimo kitakachoendeshwa kwa mfumo wa umwagiliaji. Ni wakati sahihi sasa kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania kuja kuwekeza wilayani Rufiji kwani kuna usalama wa kutosha kuanzia namna ya kuhifadhi fedha zao mpaka kutekeleza miradi watakayoianzisha,” amesema Mchengerwa.
Ili kutoachwa nyuma, Mchengerwa ambaye ni mbunge wa Rufiji tangu mwaka 2015 amewahimiza wananchi wenzake kulitumia tawi hilo la Benki ya CRDB hivyo kunufaika na huduma zinazotolewa na kujihakikishia usalama wa fedha, kukopa kwa ajili ya miradi na mipango binafsi hata kufanya uwekezaji.
“Rufiji ni kati ya wilaya kongwe nchini lakini kwa muda mrefu haikuwa imefunguka ila leo hii Benki ya CRDB imeonyesha njia. Ili kuwa wilaya ya sita wakati wa mkoloni na ya 13 baada ya uhuru. Mimi ni mteja wa siku nyingi wa Benki ya CRDB hivyo nawasihi wananchi wenzangu nanyi mjiunge kutumia huduma za benki hii.
Benki hii ya CRDB inayo huduma ya imbeju ambayo ni programu maalumu ya kuwawezesha vijana na wanawake. Makundi haya muhimu kwa jamii yetu yapo wilayani Rufiji na kwa kufika kwenye tawi hili ndivyo yataweza kunufaika na programu hii inayotoa mtaji wezeshi kwao. Kwa kuwa Rufiji ina kila kitu kinachohitajika kwa mjasiriamali kujikwamua kiuchumi, mtaji huu unaotolewa na Benki ya CRDB na mikopo ya aina tofauti iliyopo ni msingi mkubwa wa kuwakomboa wananchi kiuchumi,” amesema Mchengerwa.
Mchengerwa amezitaja fursa nyingine zilizopo wilayani humo kuwa ni pamoja na kilomita za mraba 6,500 ambazo ni hifadhi na misitu zinazofaa kwa utalii. Nyingine amesema ni uvuvi, huduma za kijamii na ukarimu zikiwamo hoteli. Kwenye kilimo, amesema ufuta, korosho na mazao mengine mengi ya biashara yanastawi vyema wilayani humo na hivi karibuni kiwanda kikubwa cha sukari kitajengwa wilayani humu.
Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa alisema wamejipanga vyema kukidhi mahitaji ya mtaji kwa ajili ya wateja wao wakiwamo wawekezaji wanaohitaji shilingi hata fedha za kigeni.
“Jana benki yetu imepata kibali za kuorodhesha hatifungani ya kijani yenye thamani ya dola milioni 300 za Marekani ambazo ni sawa na shilingi bilioni 780. Fedha zitakazokusanywa kutokana na mauzo ya hatifungani hii zitaelekezwa kwenye miradi inayolinda na kujali mazingira. Rufiji ni kati ya maeneo yanayostahili kuzitumia hivyo nawakaribisha mje tuwahudumie,” amesema Raballa.
Afisa huyo amesema kupitia tawi hilo, wananchi wa wilaya nzima ya Rufiji wanafunguliwa milango kunufaika na mtandao mpana wa matawi 260 yanayoifanya Benki ya CRDB kuwa na idadi kubwa zaidi ikilinganishwa na benki nyingine nchini.
Licha ya huduma matawini, kupitia mawakala wa benki, mashine za kutolea fedha na zile zinazopokea malipo ya kadi au kupitia simu ya mkononi, amesema Benki ya CRDB inatoa ushauri na elimu kuhusu masuala ya fedha, uwekezaji na namna bora ya uendeshaji wa biashara.
“Watu wengi hudhani benki ni kuweka, kutoa pesa au kuomba mkopo tu lakini ukweli wasioujua ni kuwa tunatoa elimu na ushauri na tumekuwa tukifanya hivyo kwa wateja wetu ingawa wengi hawaitumii huduma hii. Hivyo niwakaribishe katika Benki yenu ya CRDB kupata ushauri.
Na kupitia taasisi yetu ya CRDB Bank Foundation, tunafanya uwezeshaji kwa wanawake na vijana kwa kuwapa mitaji wezeshi kwa masharti nafuu ili kuwapa nafasi ya kuimarisha kipato chao na kushiriki kujenga uchumi wa taifa,” amesema Raballa.
Benki ya CRDB ndio taasisi pekee ya kizalendo yenye matawi nje ya mipaka ya Tanzania ikitoa huduma nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
No comments:
Post a Comment