Na.Mwandishi Wetu
Serikali inatarajia kutoa ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640 kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu kwa asilimia 100 kupitia mpango wa Samia Skolashipu kwa Mwaka wa masomo 2023/24.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesisitiza kuwa ufadhili huo ni kwa masomo ya Shahada ya Kwanza kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika Mitihani ya Kidato cha Sita mwaka 2023 inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika tahasusi za Sayansi na kuchaguliwa kujiunga na Programu za Sayansi Teknolojia, Elimu Tiba na Hesabu katika Vyuo vikuu nchini.
Ameongeza kuwa kwa mwaka wa masomo 2023/24 Wizara imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 6 kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.
Ameeleza kuwa Maombi ya Samia Scholarship yatawasilishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa https://olas.heslb.go.tz kuanzia Jumatatu, Septemba 25, 2023.
Amesisitiza kuwa Skolashipu hizo zitaendelea kutolewa kwa haki na kwa uwazi , kwani vigezo vinafahamika na vitafuatwa na kwamba lengo ni kuongeza chachu ma idadi ya wanasayansi nchini.
“Samia Skolashipu inalenga kuongeza idadi ya wanasayansi nchini ambao watachangia moja kwa moja katika maendeleo ” amesisitiza waziri huyo.
Aidha, Prof. Mkenda amesema kuwa kwa mwaka wa masomo 2022 /23 shilingi bilioni tatu zilitengwa na kunufaisha wanafunzi 636 ambapo Kati ya wanafunzi hao, wa kike walikuwa 261 (41%) na wa kiume 375 (59%) na kwamba wanafunzi hao walidahiliwa na kusajiliwa katika taasisi 18 za Elimu ya Juu kikiwemo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS),
Amesema Idadi ya wanafunzi watakaokuwa wamefadhiliwa na Scholarship hiyo katika miaka miwili itakuwa imefikia wanafunzi 1276.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa ufadhili utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na utagharamia maeneo ya ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, Vitabu na Viandikwa, utafiti,Bima ya Afya, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo na vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kwamba Orodha ya majina ya wanafunzi wenye sifa za kuomba itapatikana kupitia www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi Agosti, 2023.
Prof. Nombo amesisitiza kuwa Mwanafunzi atakaepata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIP atapaswa kuzingatia masharti ambayo ni pamoja na Kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili wa Masomo kati yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Masharti mingine ni pamoja kuwa mnufaika hataruhusiwa kubadilisha programu ya masomo aliyopatia ufadhili bila barua ya idhini ya maandishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; na hataruhusiwa kuahirisha masomo, isipokuwa kwa sababu za kiafya, na kuthibitishwa na chuo husika.
Katibu Mkuu ameongeza kuwa Iwapo kiwango cha ufaulu wa mnufaika kitashuka chini ya GPA 3.8 katika mwaka wa masomo, ufadhili utasitishwa mnufaika ataendelea na masomo kupitia mkopo wa Elimu ya Juu.
Aidha ameongeza kuwa ina mfumo wa kufuatilia maendeo ya wanufaika hao ambapo kila mmoja wao apaswa kujiandikisha katika mfumo kupitia https:schlarshis.moe.go.tz
Mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Dina Giga ameishukuru Serikali kwa ufadhali huo ambao umeondoa gharama kwa wazazi, lakini pia imeleta hamasa kwa wanufaika kusoma kwa bidii na pia kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kujiunga na programu za Sayansi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 27,2023 jijini Dar es Salaam kuhusu ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640 kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu kwa asilimia 100 kupitia mpango wa Samia Skolashipu kwa Mwaka wa masomo 2023/24.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo,akizungumzia ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akiwa katika picha ya pmoja mara baada ya kuzungumzia ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640 kupitia mpango wa Samia Skolashipu kwa Mwaka wa masomo 2023/24.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
No comments:
Post a Comment