Na Mwandishi Wetu
Uhusiano wa kufanya kazi kwa karibu kati ya Benki ya Biashara Tanzania (TCB) na Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT Taifa) umeanza kwa kishindo kiuwezeshaji na ahadi za kushirikiana kibiashara ili kuisaidia serikali kulijenga taifa na kuwahudumia vyema wananchi.
Wiki hii, taasisi hizo mbili zimesema zimejipanga vizuri kuunganisha nguvu zao kutimiza azma hiyo na ziko tayari kuhakikisha zinafanya kila linalowezekana kusaidia kuboresha maisha ya Watanzania na kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini.
Na kwa mara ya kwanza, TCB imeshiriki mkutano mkuu wa mwaka wa ALAT ambao mara hii umefanyika kwa siku mbili jijini Arusha kuanzia Jumatatu. Mbali na ushiriki huo, benki hiyo pia ilikuwa mmoja wa wadhamini wake kwa ufadhili wa TZS 100 milioni.
Benki ya TCB ilitumia fursa hiyo kujinadi si tu kwa washiriki zaidi ya 500 wa mkutano huo lakini pia hata kwa wajumbe wa ALAT na viongozi wa wanachama wa jumuiya hiyo ambao ni halmashauri zote 184 nchini.
Wakitoa maoni yao kuhuss ushirikiano huo, wana ALAT walisema hilo ni jambo ambalo jema na wako tayari kufanya kazi kwa karibu na TCB kwani kufanya hivyo si tu ni jambo la kimaendeleo kwa taifa lakini pia la kizalendo.
“Kwa namna ya kipekee niwashukuru TCB kwa uhusiano huu na tunawahakikishia mchango mkubwa wa kibiashara kutoka kwetu kama taasisi pamoja na wanachama wetu wote kwa ujumla,” Meya wa Mwanza, Bw Sima Constantine ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa alisema.
Hiyo ilikuwa ni kwenye hafla iliyoandaliwa na TCB kama sehemu ya udhamini wake wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 37 wa ALAT uliofanyika katika ukumbi wa AICC na kufunguliwa rasmi Jumatatu na Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango.
Wajumbe wa mkutano huo, akiwemo Bi Halima Mchoma, diwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Mtwara, alisema kufanya kazi na TCB ni kusaidia kuiwezesha serikali hasa kimapato.
Wengine, kama Bw Bahati Heneriko, mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ya Kagera, walisema kufanya biashara na TCB pia kuna tija kimaslahi ya taifa kwa sababu ndiyo benki pekee inayomilikiwa kwa kiasi kikubwa na serikali.
“Kwa jinsi muundo wa umiliki wake ulivyo, hii ndiyo benki yetu Watanzania wote ambayo kila mtu anapaswa kuiunga mkono izidi kushamiri na kuchangia kikamilifu maendeleo yetu,” Mwenyekiti wa Hamashauri ya Wilaya ya Kibondo, Bw Habili Charles Maseke, aliliambia gazeti hili.
“TCB ni benki ya taifa na ya kizalendo kutokana na serikali kumiliki asilimia 83 ya hisa zake. Kwa hilo, tuipe ushirikiano stahiki,” kiongozi huyo kutoka Kigoma aliongeza na kuichagiza TCB kujitanua zaidi kwa kupeleka huduma zake katika maeneo ambayo haipo kwa sasa kama Kibondo.
Awali kwenye wasilisho lake siku ya Jumatatu, Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Bw Sabasaba Moshingi, alisema wao ndiyo wenye mtandao wa tatu mpana wa matawi ambayo ni 82 nchi nzima yanayosaidiwa na ATMs 86 na zaidi ya mawakala 5000 kulihudumia taifa.
Mbali na serikali, Bw Moshingi alisema wamiliki wengine wa TCB ni Shirika la Posta lenye hisa asilimia nane, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (3%), Posta na Simu Saccos (3%), PSSSF (2%) na Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi (WCF) (1%).
Lililomvutia zaidi kiongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini A ya Zanzibar, Bw Mchano Fadhil Babra, ni pale CEO Moshingi aliposema siku si nyingi TCB itafikisha miaka 100. Sasa hivi benki hiyo ina uzoefu wa kuwepo sokoni kwa miaka 97 ikichangia ujenzi wa taifa kupitia huduma mbalimbali hususani zile za mikopo kwa makundi maalumu.
“Tuko vizuri hasa katika makusanyo ya fedha na kuyakopesha makundi maalumu kama yale ya akina mama na vijana ambayo hadi sasa tumeyapatia mikopo yenye thamani ya zaidi ya TZS bilioni 60,” Bw Moshingi alisema wakati akieleza faida ambazo halmashauri zitapata kwa kufanya kazi na TCB.
Aidha, alibainisha kuwa benki hiyo pia ina sifa ya kuanzisha huduma mbalimbali nchini kama zile za benki wakala na benki mtandaoni ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika ajenda ya taifa ya ujumuishaji kifedha.
Nyingine kuybwa ni ile ya kuwakopesha wastaafu.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Tanzania Commercial Bank Tawi la Arusha-Meru
Selestine Mteta alipotembelea banda la benki hiyo wakati wa mkutano mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania - ALAT unaofanyika jijini Arusha. Benki ya TCB ilikuwa ni mmoja wa wadhamini wa mkutano huo
No comments:
Post a Comment