SHAMBA LA MITI RUBYA WAJENGA KITUO CHA POLISI KWA GHARAMA YA MILIONI 54/- - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 6, 2023

SHAMBA LA MITI RUBYA WAJENGA KITUO CHA POLISI KWA GHARAMA YA MILIONI 54/-

 

-Wananchi wafurahia kusogezewa kituo karibu na makazi yao, waishukuru Serikali

Na Said Mwishehe, Michuzi TV –Ukerewe

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kupitia Shamba la Miti Rubya lililopo wilayani Ukerewe mkoani Mwanza wamekamilisha ujenzi wa kituo cha polisi Serema ambacjo kimegharimu Sh.milioni 54 hadi kukamilika kwake.

Ujenzi wa kituo hicho unatokana na uchakavu wa kituo cha polisi ambacho kimekuwepo katika shamba la Rubya kwa muda mrefu, hivyo TFS iliona iko haja ya kutoa fedha kujenga kituo cha polisi kipya, lengo likiwa kuimarisha usalama wa msitu pamoja na mali za wananchi wanaozunguka shamba hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari PCO Mhifadhi Mkuu Shamba la Miti Rubya Festo Chaula amesema Shamba hili ni miongoni mwa mashamba yanayosimamiwa na TFS na kati ya mwaka 1986 mpaka mwaka 2004 kulitokea wimbi kubwa la uhalifu mkubwa wa rasilimali zitokanazo na misitu.

“Hivyo Serikali iliamua kuleta kituo cha polisi eneo hili ili kukabiliana na uhalifu, hata hivyo hakukua na jengo ,kwa hiyo shamba la miti Rubya liliamua kutoa jengo lake kwa niaba ya Serikali ili kuwe na kituo hicho cha polisi.

“Hata hivyo kituo hicho kimekuwepo kwa muda mrefu na kusababisha majengo yake kuwa chakavu ,kutokana na uchakavu wa kituo hicho ,shamba la miti Rubya kupitia TFS kwa niaba ya Serikali tuliamua kukiboreha,”amesema PCO Chaula .

Aidha amesema ilipofika nwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali kupitia shamba la miti Rubya ilitoa Sh.milioni 54 kujenga kituo kipya polisi ambacho kimejengwa eneo la Serema kwasababu pale kilipokuwepo awali lilionekana ni eneo la hifadhi ya barabara lakini pia ni eneo la linalohistahili kuachwa kwasababu za uhifadhi wa mazingira.

“Faifa ya kituo hiki kitasaidia wananchi kupunguza uhalifu hasa kwenye shamba lenyewe pamoja na wannchi wote wanaozunguka hili shamba,”amesema na kuongeza mbali ya kujenga kituo hicho wamekuwa wakisaidia katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema shamba la miti Rubya pia lilishajenga Zahanati ambayo inahudumia wananchi wanaozunguka shamba hilo huku akifafanua pia wamesaidia ujenzi wa madarasa,wametoa bati 96 kwa ajili ya Shule ya Msingi Rubya pamoja na mifuko ya saruji 100 katika kijiji cha Serema.

“Kazi za uhifadhi zinaendelea kama kawaida lakini pia kituo hiki kuwepo hapa jirani tunapata usalama mkubwa na hata wananchi wanafurahi kwa kuamini watakuwa salama zaidi kwasababu kipo karibu,”amesisitiza .

Kwa upande Mkaguzi Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo cha Polisi Rubya amesema wanaishukuru Serikali kupitia TFS kwa ujenzi wa kituo kipya cha polisi Rubya na baada kukamilika kwa kituo hicho matumaini yao wananchi watapa huduma karibu na makazi yao.

“Kwa kituo hiki cha Rubya tunakwenda kuhudumia kata zima ya Bwiro yenye vijiji vinne lakini pia baadhi ya vijiji vya Kata ya Mriti na kata ya Igala, kwa hiyo tunatoa huduma kwa kata tatu.Kituo cha polisi Rubya kimekuwa ni msaada muhimu katika kukabiliana na wahalifu na kwa sasa hali ni nzuri sana,”amesema huku akisisitiza wamekuwa na ushirikiano mkubwa na TFS pamoja na vijiji vyote vinavyozunguka msitu.

Wakati huo huo Mtendaji wa kijiji cha Rubya Justinian Emmanuel ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa TFS kwa kushirikiana na Serikali ya Kijiji kwa kujenga kituo hicho ambacho tayari kimekamilika.

“Kwa kipekee tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa msaada wa ujenzi wa kituo hiki kwani kule kilipokuwepo awali tulikuwa tunatumia gharama kubwa kwenda kufuata huduma , sasa huduma imesogea karibu kabisa na wananchi,”amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji Serema Mkama Mjaya Mkama ametoa shukrani kwa shamba la miti Rubya kwa kutoa ushirikiano na kujenga kituo hicho.

“Shamba la miti Rubya walituandikia barua ya kuomba ardhi kwa ajili ya kujenga kituo cha polisi, Serikali ya kijiji tuliona tunao uhitaji wa kuwa na kituo cha polisi hivyo tulikubali kwa kutoa ardhi bila malipo yoyote,”amesema.

Muonekano wa juu wa shamba la miti Rubya

Jengo la utawala la Shamba la Miti Rubya ambalo kama linavyoonekana katika picha

Mmoja ya wakazi wanaozunguka shamba hilo akikaokota kuni baada ya uongozi wa shamba hilo kuruhusu wananchi kuokota kuni

Muonekano wa jengo la zamani la kituo cha Polisi ambacho kilikuwa kinatumiwa kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi wanaozunguka shamba la miti Rubya .Kutokana na kuchaa kwa kituo hicho shamba hilo kwa niaba ya Serikali wamejenga kituo kipya cha Polisi Serema


Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Rubya wilayani Ukerewe mkoani Mwanza PCO Festo Chaula( wa tatu kutoka kushoto waliosimama mbele) akiwa na baadhi ya viongozi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Serema ambako kimejengwa kituo kipya cha polisi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad