MKAZI wa Simanjiro Mkoani Manyara Joshua Kanunga ameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo.
Shukrani hizo amezitoa wakati akiongea na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipofika ofisini kwake jana kwaajili ya kumshukuru kutokana na Taasisi hiyo kumsamehe gharama ya matibabu ya mke wake aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo hivi karibuni.
Kanunga alisema mke wake aliyekuwa na matatizo ya moyo amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika Taasisi hiyo bila malipo kutokana na hali yao ya kiuchumu kutomudu kulipia gharama za matibabu hayo.
“Naushukuru sana uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kumpokea mke wangu anayesumbuliwa na maradhi ya moyo na kukubali kumsamehe gharama za matibabu ambazo zilikuwa ni shilingi 5,294,000”, alisema Kanunga
Kanunga alisema mke wake alianza kuumwa tangu mwaka 2017 na kumtafutia tiba tofauti tofauti hadi ilipofika mwaka 2021 alipompeleka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na kugundulika kuwa na magonjwa ya moyo hivyo kupewa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu.
“Namshukuru Mungu mke wangu katibiwa na sasa kaambiwa amepona tatizo lililokuwa likimsumbua, sasa hivi tunajiandaa kwa ajili ya kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kuhangaika kwa miaka sita bila ya mafanikio”, alisema Kanunga
Kanunga aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kubuni mbinu ya kuanzisha Hospitali inayotibu magonjwa ya moyo hapa nchini ili kuwasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata matibabu hayo.
“Watanzania wengi hatuna uwezo wa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta tiba, naipongeza sana Serikali kwa kuanzisha Taasisi hii, pia nawapongeza madaktari waliomhudumia mke wangu kwa upendo bila ya kuangalia uwezo wetu mdogo wa kiuchumi”, alisema Kanunga
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Taasisi hiyo itaendelea kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wote wenye uwezo wa kulipa na wasio kuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu.
“Katika Taasisi yetu tunapokea wagonjwa wanaolipa gharama za matibabu wao wenyewe, wagonjwa wanaolipiwa na bima za afya, wagonjwa wanaolipia sehemu ya huduma na sehemu inayobaki Taasisi inawalipia na wagonjwa ambao hawalipi kabisa huduma za matibabu” alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kuna taratibu za ustawi wa jamii ambazo wagonjwa wasio na uwezo wa kulipa wanatakiwa kuzifuata na kama watakidhi vigezo Taasisi inawachangia au kuwalipia gharama za matibabu.
Dkt. Kisenge aliwaomba wananchi wajiunge na bima za afya ili ziwasaidie kulipa gharama za matibabu ikiwemo ya moyo kwani matibabu yake ni ya gharama kubwa.
No comments:
Post a Comment