Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware (kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa Strategis, Dkt. Flora Minja (katikati) na Afisa Mtendaji Mkuu-Bima za Mali na Majanga, Jabir Kigoda wakipiga makofi kuashiria uzinduzi rasmi wa Bima ya Kilimo ya Strategis Insurance uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware (kulia) akibofya kitufe kuzindua rasmi bidhaa mpya ya Kampuni ya Bima ya Strategis ijulikanayo kama Bima ya Kilimo ya Mtetezi Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Strategis, Dkt. Flora Minja na Afisa Mtendaji Mkuu-Bima za Mali na Majanga, Jabir Kigoda.
KAMPUNI ya bima ya Strategis, ambayo ni moja ya makampuni ya bima yanayoongoza nchini, leo imezindua rasmi bima ya Kilimo ijulikanayo kama Mtetezi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bima hiyo ya Mtetezi Jijini Dar es Salaam, Kamishina wa bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, ameipongeza kampuni ya Strategis kwa kuendelea kuzindua huduma mbali mbali za bima ambazo zinaendana na mahitaji ya soko.
’Kampuni ya Strategis ni moja ya makampuni ambayo yamekuwa yakiwekeza katika uvumbuzi wa bidhaa ambazo zinakwenda na mahitaji ya soko. Nakumbuka miezi miwili iliyopita, kampuni hii ilizindua bima ijulikanayo kama ‘’container insurance’’ na leo tuko hapa kushuhudia uzinduzi mwingine wa bima ya kilimo ijulikanayo kama Mtetezi’’. Amesema Dk. Saqware.
Aidha Pamoja na kuwapongeza kwa hatua hii, Dkt. Saqware amewaomba pia Strategis kuangalia uwezekano wa kutoa bidhaa nyingine za bima kwenye upande wa mifugo na misitu.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Strategis, Dkt. Flora Minja, amesema Strategis inaamini kwamba kuna nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo na hivi karibuni, tumeona jitihada mbali mbali zilizochukuliwa na Serikali yetu ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kuboresha sekta hii.
Uwekezaji na mipango iliyofanyika na inayoendelea kufanyika imewapa wadau wa sekta hii matumaini makubwa ya uwezo wa sekta hii kuendelea kukua zaidi.
“Bima hii mpya itawalinda wakulima dhidi ya majanga mbalimbali yanayoathiri mavuno ya mazao nq wakulima watapata fidia endapo watakumbana na majanga ambayo yanaweza kuathiri mavuno yao kama vile hali ya hewa, wadudu, magonjwa na majanga mengine,” amesema Dkt. Minja.
Pamoja na hayo, wadau wote waliohudhuria walipata muda wa kuelimishwa kuhusu huduma hiyo mpya ya bima kutoka Strategis. Akitoa maelezo kuhusu huduma hiyo, Afisa mkuu Mtendaji wa Strategis upande wa bima za mali na ajali, Jabir Kigoda amesema kuwa bima hii ya Mtetezi ina faida kubwa kwa wakulima na wadau wote katika sekta ya kilimo. ‘’Huduma hii ya bima inatoa kinga ili kuhakikisha mkulima anapata mavuno anayostahili kutoka eneo lake husika kwa kuangalia historia ya uzalishaji wa eneo hilo.
Vile vile bima hii inampa nafasi mteja kuweza kukinga mazao yake kutokana na athari za hali ya hewa kama vile ukame na mafuriko. Hivyo basi, utofauti mkuu wa bima hii na nyingine ni kumpa mteja chaguo ili kuweza kupata bima sahihi kwa mazao yake. Hii ni moja ya faida kubwa ya bima hii kwasababu kuna baadhi ya maeneo ambayo ni vigumu kuweza kutumia bima inayo angalia zaidi kiasi cha mavuno yaliyopatikana kwa kulinganisha na historia ya uzalishaji wa eneo hilo’’. Amesema Kigoda.
"Tumeona juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya kilimo kwani kuna mikakati mizuri sana ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali na hivyo basi kuwapa matumaini wananchi ".
Hata hivyo, wakati tunafurahi jitihada hizi, basi ni lazima pia tujue kuna majanga pia ambayo yanaweza kuja na kuharibu uwekezaji huo uliofanywa kwenye sekta hii. Hivyo basi tunaamini, bima ya kilimo ya Mtetezi toka Strategis itakuja kulinda uwekezaji huo uliofanywa.
No comments:
Post a Comment