HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 22, 2023

Jamii yahimizwa kuchangia damu

 






Na Salome Majaliwa – Dar es Salaam
WADAU wa afya nchini wameitaka jamii kuona umuhimu wa kuchangia damu ili kuwezesha huduma za matibabu ikiwemo upasuaji wa moyo kufanyika kwani changamoto ya upatikanaji wa damu imekuwa ikipelekea wagonjwa kukosa huduma za matibabu kwa wakati.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa chama cha wachangia damu kwa hiyari Tanzania Dominick Mkane alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuona huduma zinazotolewa pamoja na kupata taarifa ya uhitaji wa damu uliopo katika Taasisi hiyo.

Mkane alisema kila mtu anaweza kuumwa na kuhitaji damu wakati wowote hivyo ni muhimu jamii ikaelewa kuwa zoezi la kuchangia damu ni la mzunguko kwani ipo siku mchangia damu naye atahitaji damu kutoka kwa mtu mwingine.

“Sisi kama wachangia damu wa hiyari tunapenda kuungana na wataalam wa afya wa JKCI kuifikia jamii na kuielezea umuhimu wa kuchangia damu mara kwa mara kuwezesha matibabu ya wagonjwa wakiwemo wa moyo wanaopatiwa matibabu hapa JKCI”, alisema Mkane.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya upasuaji wa JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema damu nyingi uhitajika katika upasuaji mkubwa wa moyo, mgonjwa mmoja ili afanyiwe upasuaji anahitaji chupa tatu za damu na endapo itatokea dharula mgonjwa anaweza kutumia hadi chupa kumi za damu kufanikisha upasuaji huo.

“Ili upasuaji mkubwa wa moyo ufanyike damu ya kutosha inatakiwa kuwepo kwani katika upasuaji mkubwa wa moyo tunasimamisha moyo na kuipeleka damu katika mashine ya kuusaidia moyo na mapafu kufanya kazi (Heart Lung Machine)”,

“Mashine hii ni ya mipira hivyo damu inapoingia kwenye mashine inapoteza uhalisia wake na kuna kiwango cha damu kitakuwa hakifai tena baada ya upasuaji kufanyika ndio maana hata baada ya upasuaji mgonjwa atahitaji kuongezewa damu tena”, alisema Dkt. Angela

Naye mgonjwa aliyelazwa katika Taasisi hiyo Mariam Selemani alisema alimchukua mwezi mmoja kukaa wodini kusubiria damu ili aweza kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na baada ya kufanyiwa upasuaji huo kutokana na damu yake kuwa ndogo kidonda chake kimechelewa kupona kwa haraka.

“Damu yangu ni ya kundi “O+” na upatikanaji wake umekuwa wa shida lakini nashukuru ilipatikana kidogo na kuniwezesha kufanyiwa upasuaji lakini hadi sasa sijaruhusiwa kwenda nyumbani kutokana na damu yangu kuwa ndogo nahitaji kuongezewa damu nyingine ili kidonda kipone kabisa”, alisema Mariam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad