Pichani ni Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani wakisikiliza mada iliyokuwa inatolewa na Mwezeshaji katika Mafunzo Elekezi yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama LushotoNa Yusufu Ahmadi IJA Lushoto
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 12/6/2023 amefungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji sita(6) wapya wa Mahakama ya Rufani na mwingine mmoja ambae hakupatiwa mafunzo hapo awali.
Mafunzo hayo yatachukua siku tano hadi tarehe 16/6/2023 na yameandaliwa na Mahakama na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na yanafanyika hapa IJA Lushoto.
Katika hotuba yake, Jaji Mkuu Prof. Juma amewatoa wito Majaji hao wa Mahakama ya Rufani kufanya kazi katika majopo ili maamuzi yao yasitofautiane..
“Maamuzi yetu yawe na uhakika wa mambo, tunafanya kazi katika majopo, jopo moja lisitoe maamuzi ambayo ni tofauti kabisa na majopo mengine, na hii imetuletea changamoto kubwa sana, Jaji mmoja wa Rufani akiamua tofauti na ule utaratibu wa kisheria, sisi wengine tunajua amekosea, kwa kinatufanya sisi wengine tukwepe uamuzi, sasa ile inakuwa sio vizuri,” amebainisha Jaji Mkuu Prof. Juma.
Pia Mhe. Jaji Mkuu Prof. Juma amewaasa Majaji hao kutafakari kwa kina maamuzi wanayoyatoa kwa kuwa Katiba ya Tanzania imewapa nafasi ya mwisho ya utoaji wa tafsiri ya haki hapa nchini.
“Jambo langu kwenu ni kwamba, ni vizuri siku zote kutafakari uzito wa maamuzi katika nafasi yenu kama Jaji wa Mahakama ya Rufani, kila siku unaposimamia shauri lolote, chukua muda mfupi kidogo, tafakari, kwa sababu Katiba imekupa nafasi ya mwisho katika tafsiri ya haki, ukikosea yale makosa yanakuwa ni makubwa sana na yanachukua muda mrefu kurekebishika,” amesema Jaji Mkuu.
Kwa upande mwingine, Jaji mkuu amewatolea wito Majaji hao kusoma masuala mbalimbali yanayoendelea duniani yakiwemo ya teknolojia badala ya kusoma tu mambo yanayohusu majalada ya Mahakamani, ili wawe na ufahamu mpana utakaowasaidia katika kushughulikia majalada.
Katika mafunzo hayo, Jaji Mkuu ameendesha mada juu ya utamaduni wa Mahakama ikiwa na lengo la kuwafanya Majaji hao wapya watambue taratibu na sheria mbalimbali zinazotumika katika uendeshaji wa mashauri katika Mahakama ya Rufani.
Majaji hao sita wapya waliyoteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hapo Mei 18 mwaka huu ni Mhe.Sam Mpaya Rumanyika, Mhe. Zainab Goronya Muruke, Mhe. Leila Edith Mgonya, Mhe. Amour Said Khamis, Mhe.Dkt Benhajj Shaaban Masoud, Mhe. Gerson John Mdemu na Mhe.Agnes Zephania Mgeyekwa.
Kwa upande wake Jaji wa Mahakama ya Rufani na mwezeshaji wa mafunzo hayo, Mhe. Augustine Mwarija amewaambia Majaji hao kuwa nafasi hiyo waliyopewa waitumie vema kuleta maboresho katika Mahakama ya Rufani.
“Natambua kuwa mlistahili kupata uteuzi huu, sina shaka mtaitumikia kwa uthabiti nafasi hiyo ambayo mmeaminiwa na kupewa, na kama mlikuwa mkiona changamoto yoyote katika mahakama ya Rufani, kwa lengo la kuendeleza maboresho, tambueni sasa ninyi ni sehemu ya kukabiliana na changamoto hizo,” amesema Jaji Mwarija.
Nae Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) Dkt. Paul F. Kihwelo ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, amesema kuwa hayo ni mafunzo Elekezi ya tatu kutolewa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, ya kwanza yakifanyika mwaka 2019 kwa Majaji nane, ya pili mwaka 2021 kwa Majaji sita na ya tatu ni ya mwaka huu 2023 kwa Majaji saba.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa pia na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Tanga, Latifa Mansoor, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Wilbert Chuma na Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 12/6/2023 yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) Dkt. Paul F. Kihwelo ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani akitoa neno ya utangulizi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yanayoendeshwa na Chuo cha Uongzo wa Mahakama Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani alipokuwa anafungua Mafunzo Elekezi leo tarehe 12/6/2023 yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
No comments:
Post a Comment