HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 2, 2023

WANACHAMA BONDE LA MTO NILE WAKUTANA KUJADILI CHANGAMOTO

 Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

SEKRETARIETI ya Bonde la Nchi za Mto Nile imekiri kuwepo changamoto mbalimbali, Mei 2-4, 2023 wanakutana kwenye mafunzo kutatua changamoto hizo ili kuhakikisha rasilimali zilizopo kwenye Bonde hilo zinalindwa, sanjari na kuomba nchi wanachama kuweka mkazo kwenye Sera ili kulinda mazingira na vyanzo vya maji.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kwenye mafunzo maalum kuhusu masuala ya pamoja ya nchi za Bonde hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde hilo, Mhandisi Sylvester Matemu amesema changamoto hizo ni ongezeko la idadi kubwa ya watu katika nchi hizo wanachama hali inayopelekea kushindwa kulinda ipasavyo rasilimali za Bonde.

“Kwenye Bonde la Mto Nile, mwaka 2012 kulikuwa na watu zaidi ya Milioni 238 na sasa kuna watu zaidi ya Milioni 272, idadi ya watu inaongezeka na ardhi haiongezeki na watu wanahitaji maji kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji umeme, shughuli za viwandani na kijamii,” amesema Mhandisi Matemu.

Aidha, Mhandisi Matemu amesema changamoto nyingine ni uharibifu wa mazingira katika Bonde hilo, amesema hali ya uharibifu wa mazingira inachangia rasilimali za Mto Nile kushindwa kulindwa ipasavyo.

“Suala la uharibifu wa mazingira ni changamoto nyingine kwenye Bonde la Mto Nile, watu waliopo kwenye Bonde wanashindwa kulinda mazingira na vyanzo vya maji ili kulinda Mto kwa ujumla na rasilimali zake,” ameeleza Mhandisi Matemu.

Pia, Mhandisi Matemu amesema hali ya mabadiliko ya tabia nchi, hali ya uwepo wa Mvua nyingi kunapelekea mafuriko kwenye Bonde na hali ya Ukame inapelekea kukauka kwa Maji katika Bonde hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde hilo amewapongeza Viongozi wa juu wa Serikali ya Tanzania kuonyesha mfano mzuri katika kusisitiza kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya Maji ili kunusuru Bonde hilo la Mto Nile.

Bonde la Mto Nile linaundwa na nchi 10 ambazo ni Burundi, DR Congo, Misri, Ethiopia, Kenya, Sudan Kusini, Sudan, Rwanda, Tanzania na Uganda.


Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Mto Nile, Mhandisi Sylvester Matemu akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kwenye mafunzo yaliyowakutanisha nchi wanachama wa Bonde hilo kujadili masuala mbalimbali yakiwemo, masuala ya Demokrasia kwenye mambo ya maji, majadiliano kwenye masuala mbalimbali na namna ya kutatua migogoro.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad