HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 10, 2023

Wagonjwa 310 kutoka nje ya nchi watibiwa JKCI kwa kipindi cha miaka miwili

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati za utalii tiba kutoka Hospitali za Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Mifupa Muhimbili (MOI), na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) uliofanyika leo katika Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es Salaam.


 Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

WAGONJWA 310 kutoka nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Visiwa vya Comoro, Ethiopia, Burundi, Armenia, Norway na Uingereza wamepata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati za utalii tiba zilizopo katika Hospitali za kibingwa hapa nchini Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema wagonjwa hao wamepata matibabu hayo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema JKCI katika kuhamasisha utalii tiba mwaka jana imeshiriki maonyesho ya huduma inazozitoa katika visiwa vya Como, wiki hii wataalamu wa Taasisi hiyo wako nchini Malawi kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo na baadaye inatarajia kwenda nchini Burundi na Jamhuri ya watu wa Congo kutoa huduma hizo.

Dkt. Kisenge alisema katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaotoka nje ya Tanzania, kwa mwaka 2022 waliona wagonjwa zaidi ya 200 na mwaka huu wa 2023 hadi sasa wametoa huduma kwa wagonjwa 110.

“JKCI imetengeneza mpango mkakati ambao unafuata malengo yaliyowekwa na kamati ya kitaifa ya utalii tiba kuhakikisha kwamba kupitia sekta ya afya utalii unaongezeka hapa nchini”,.

“Ninaipongeza kamati ya kitaifa ya utalii tiba kwa kuwa chachu ya kufanikisha malengo ya Rais wa Serikali ya awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ninaahidi Taasisi yetu imejipanga kutangaza utalii tiba kwa vitendo”, alisema Dkt.Kisenge.

Aidha Dkt. Kisenge amesema kuwa JKCI inatarajia kufanya mkutano mkubwa mwaka 2024 utakaoonyesha nini kinafanywa na Taasisi hiyo na matarajio yao ni kuhakikisha kuwa zaidi ya nchi 40 zinashiriki katika mkutano huo.

Akizungumza mara baada ya kuzindua kamati za utalii tiba Mratibu wa matibabu nje ya nchi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita alisema hospitali za kibingwa zinatakiwa kujenga uaminifu na ukarimu kwa wagonjwa wanaowahudumia ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kutibiwa kwani huduma zote za kibingwa sasa hupatikana hapa nchini.

Dkt. Asha alisema dhana ya utalii tiba nchini ilikuwa bado haijaeleweka vizuri hapo awali lakini tangu kuanza kwa kamati maalum ya utalii tiba mabadiliko makubwa yametokea kwani sasa wagonjwa kutoka nchi nyingi za Afrika wanakuja Tanzania kupata huduma za matibabu ya kibingwa yanayotolewa na Hospitali zetu.

Dkt. Asha alisema lengo kubwa la utalii tiba ni pamoja na kuongeza pato la nchi lakini pia mtu mmoja mmoja katika nchi kufaidika kupitia utalii tiba kwani wagonjwa wanaofika watahitaji malazi na huduma nyingine hivyo wote kwa pamoja kukuza uchumi wa nchi na uchumi binafsi.

“Kuzindua kamati za utalii tiba ni tukio kubwa katika sekta ya tiba utalii hapa nchini, nawapongeza kwa niaba ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo kamati ya kitaifa ya utalii tiba imefanya tangu walipoteuliwa mwaka 2021 hadi sasa”, alisema Dkt. Asha

Aidha Dkt. Asha amezitaka Hospitali zote nchini kujitathmini na kuamua zinataka kufanya nini ili kuendana na malengo ya wizara inapojiandaa kutengeneza muongozo ambao utaleta majukumu ya kada zilizopo katika Hospitali kuwezesha kila mfanyakazi kuchukua nafasi yake na kutekeleza majukumu yake.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya utalii tiba Prof. Mohamed Janabi alisema kupitia kamati ya kitaifa ya utalii tiba wameweza kuujulisha umma nini maana ya utalii tiba hivyo kupunguza idadi ya watu waliokuwa wanakwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.

Prof. Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema kufikia mwaka 2030 Tanzania inatarajia kuwa na watalii milioni tano waonafika hapa nchini kwa mwaka na kupitia watalii hao wapo baadhi ambao watahitaji huduma za matibabu hivyo ni vyema Hospitali zikaendelea kuboresha huduma na kuvitunza vizuri vifaa tiba kwani ni vya gharama.

“Dhumuni letu kubwa kama kamati tunataka tupate angalau asilimia 10 ya wagonjwa wanaokwenda nchi za ulaya kwaajili ya matibabu kutibiwa katika nchi yetu kwasababu sasa vifaa tunavyo na wataalam kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa wapo wakutosha”, alisema Prof. Janabi.

Mratibu wa matibabu nje ya nchi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge kitabu chanye mpango mkakati wa utalii tiba kilichoandaliwa na kamati wa kitaifa ya utalii tiba leo wakati wa uzinduzi wa kamati za utalii tiba kutoka Hospitali za Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Mifupa Muhimbili (MOI)na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es Salaam.
Wanakamati wa utalii tiba kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja na Mratibu wa matibabu nje ya nchi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita na viongozi kutoka Taasisi mbalimbali mara baada ya uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika leo katika Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad