HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 1, 2023

LATRA YAONGEZA MUDA USAJILI WA MADEREVA NCHINI

 


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeongeza muda wa usajili wa Madereva nchini kwa miezi mitatu mingine, badala ya agizo la mwisho wa usajili 30 Aprili 2023, zoezi hilo litaendelea hadi Julai 30, 2023 ili kutoa fursa kwa Madereva hao kuendelea kujisajili na kuthibitishwa na Mamlaka hiyo.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Jahansen Kahatano wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Mamlaka hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam, Kahatano amesema hadi sasa Madereva 3,334 wamesajiliwa kwenye Mfumo akibainisha kuwa ni idadi ndogo.

“Tumeona tuongeze muda wa usajili wa Madereva wote nchini kutokana na awali zoezi hili la usajili kuwa na changamoto za Madereva wengi kukosa Vyeti vya Shule za Udereva, wengi wamekosa mafunzo ya Udereva lakini kuwepo kwa hitaji la kupima Afya, suala ambalo kwa sasa tumeliondoa,” amesema Kahatano.

Kahatano amesema ili Dereva aweze kusajiliwa na LATRA anatakiwa kuwa na Leseni ya Udereva, Kadi ya NIDA na Cheti cha Udereva, amesema zoezi hilo linaendelea baada ya kutamatika hivi karibuni baada ya miezi mitatu ya awali kutolewa, amesema Madereva wote wanapaswa kusajiliwa Mamlaka hiyo kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).

Kahatano amebainisha sababu za usajili wa Madereva kuwa na faida nyingi ikiwemo kutambua fani hiyo ya Udereva kama Taaluma rasmi ya Udereva sanjari na Madereva wote kutambuliwa kama Wanataaluma hiyo, pia kuunganisha mifumo ya usafirishaji kwenye Kanda za SADC, Kanda ya Afrika na COMESA ili kuwa na urahisi kufanya shughuli za usafirishaji mipakani.

Aidha, Kahatano amesema Mamlaka ya LATRA imefanya maboresho katika muda wa usafiri wa Mabasi makubwa ambayo yalitakiwa kulala njiani kwa Mabasi yanayotoka Dar es Salaam hadi Kigoma na Katavi ambayo awali yalilazimika kulala njiani kwa sababu ya usalama.

“Kutokana na kauli ya Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni, iliyotolewa bungeni tumefanya maboresho ya muda wa kuondoka Mabasi hayo, kwa sasa yataanza safari zao kuanzia Saa 9 hadi 10 Usiku badala ya Saa 11 Alfajiri,” amesema Kahatano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad