HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 19, 2023

Jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi lafunguliwa


Baadhi ya wadau mbalimbali wa masuala ya uwezeshaji wanawake waliohudhuria uzinduzi wa Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa ajili ya kuwafikia wanawake katika sekta mbalimbali za uchumi na kuunganisha nguvu zao pamoja zitakazowasaidia kutambua fursa zinazowazunguka na kufaidika kiuchumi. JUKWAA la kitaifa la kuwawezesha wanawake kiuchumi limezinduliwa ili kuliwezesha kundi hilo kufikia fursa zinazowazunguka. 


Uzinduzi huo umefanywa hivi karibuni jijini Dodoma na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kwa kushirikiana na Taasisi ya Legal Services Facility.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amesema jukwaa hilo limeanzishwa ili kuongeza uelewa kwa wanawake kuhusu masuala ya Biashara, upatikanaji mitaji na Sheria za nchi katika masuala ya uchumi.

Amesema mbali na jukwaa hilo la kitaifa, Serikali imeunda majukwaa ngazi ya mkoa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

“Kupitia maazimio ya mkutano wa wanawake Beijing 1995, Tanzania iliamua kujikita katika maeneo manne ambayo ni: kuwawezesha wanawake kiuchumi; wanawake na haki za kisheria; usawa katika elimu, mafunzo na ajira; na wanawake katika nafasi za uongozi na ngazi za Maamuzi.”

Waziri huyo wa maendeleo ya Jamii amesema “pia, mwaka 2021, Tanzania ilishiriki Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Kizazi chenye Usawa (Generation Equality Forum) uliofanyika Jijini Paris – Ufaransa, ambapo Tanzania iliwasilisha ahadi za nchi, ambazo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ni kinara katika utekelezaji wa eneo linalohusu haki na Usawa wa Kiuchumi.”

Katika hatua nyingine, Dk. Gwajima ameyaagiza majukwaa hayo nchi nzima kuwaunganisha wanawake katika fursa za kibenki, masoko na utaalamu wa kuboresha uzalishaji wa bidhaa zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala, amesema Shirika hilo imeamua kushirikiana na Serikali katika uzinduzi wa jukwaa hilo, kwa kuwa linagusa moja ya maeneo muhimu ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki kwa watu wote.

“Ni matumaini yetu kuwa Jukwaa hili la kitaifa litajikita katika kusghulikia changamoto mbalimbali za wanawake kwenye masuala ya kiuchumi, masuala ya kisera, kitaaluma, kirasilimali pamoja na haki nyingine za msingi za kiuchumi. Sisi kama LSF tutaendelea kushirikiana na Jukwaa hili kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii,” amesema Ng’wanakilala.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ikiwa ni sehemu ya Serikali kuendelea kutekeleza mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa kuhusu kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, ambayo imewezesha Serikali kuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuanzisha jukwaa hilo nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambalo litasaidia kushughulikia changamoto mbalimbali za wanawake kwenye masuala ya kiuchumi, sera, taaluma, rasilimali pamoja na haki nyingine za msingi za kiuchumi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, ambapo amesisitiza Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Majiji kuendelea kutenga fedha za ndani ili kuwawezesha Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kukopa na hatimaye kuweza kujiendeleza kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad