HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 24, 2023

DART yahitaji wanawake madereva wa kuendesha mabasi yaendayo haraka

 


*Takwimu zinaonyesha ajali nyingi zimesababishwa na wanaume

Na Chalila Kibuda, Michuzi TV
WANAWAKE wametakiwa kuchangamkia fursa kwa kusoma kozi ya udereva ili waweze kuajiriwa na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwani wameonekana kumudu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuendesha magari yaendayo haraka bila kusababisha uharibifu wowote.

Wanawake hao wanatakiwa kuwa na leseni C kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili waweze kujipatia ajira hiyo kutokana uhitaji wa kundi hilo.

Akizungumza Mkoani Dodoma katika semina maalam ya kuwajengea uwezo waandishi habari, Meneja wa Mipango na Usafirishaji Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Mohamed Kuganda, alisema kuwa DART imefanikiwa kuajiri madereva 360 kati yao wanawake 18.

Mhandisi Kuganda alisema kuwa madereva wanawake 18 ambao wamefanikiwa kufanya nao kazi katika kuendesha magari yaendayo haraka wapo makini na kuwa tofauti na wanaume.

"Tuna madereva wanawake 18 na wapo makini kwani hawajawahi kusababisha ajali katika utekelezaji wa wanajukumu yao barabarani wakati wanaendesha mabasi yaendayo haraka, ajali nyingi za DART zimesababishwa na madereva wanaume " alisema Mhandisi Kuganda.

Mhandisi Kuganda alisema kuwa madereva wengi wanawake wapo makini katika kuendesha magari kutokana na kuwa na nidhamu Katika kazi na wanafanya kwa uweledi mkubwa mpaka abiria wanafurahia.

Alisema kuwa madereva wanapaswa kuwa na nidhamu katika kuendesha magari ili kuepukana na ajali ambazo asilimia kubwa zinasababishwa na madereva wasiokuwa makini.

"Tunaomba wazazi waweze kuwapeleka vijana wao wa kike kusoma fani ya udereva, Kwa sababu sisi kama DART tuna uhitaji mkubwa wa madereva na kwa sababu wanawake wapo makini na kazi tunawahitaji sana" amesema Mhandisi Kuganda.

Amebainisha kuwa katika kuhakikisha wanaongeza idadi ya madereva wa kike wamekuwa na programu maalam ya kuwajengea uwezo madereva wa kike 100 iliyofanyika katika Chuo Cha Usafirishaji Tanzania (NIT).

"Kati ya madereva wanawake 100 ambao tuliwajengea uwezo ni madereva 18 walifanikiwa kujiunga na Kwa Sasa wanafanya kazi na DART wengine waliendelea kufanya kazi katika Kampuni na taasisi nyengine za usafirishaji" amesema Mhandisi Kuganda

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad