HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 3, 2023

WATEJA ZAIDI YA 30,000 WAJIUNGA NA CRDB AL BARAKAH, WANUFAIKA NA UWEZESHAJI WA SHILINGI BILIONI 73 NDANI YA MWAKA MMOJA

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Mudrick Soraga (wapili kushoto) na Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile (wanne kulia) wakikabidhi msaada wa futari kwa vituo vya kulelea watoto vya Jukumakhe kilichopo Melitano, na Sebleni Masjid Jumma wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB mwishoni mwa wiki katika hoteli ya Verde, Zanzibar. Wengine pichani ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Kikwajuni, Mhe. Nassoro Salim Ali, (wapili kulia), Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredricck Nshekanabo (wakwanza kushoto), na Mkuu wa Kitengo cha CRDB Al Barakah, Rasid Rashid (wakwanza kulia). 
 
=============   ============   ============ 

Benki ya CRDB imesema kuwa wateja zaidi ya 30,000 wamejiunga na huduma za benki hiyo zinazofuata misingi ya sharia za “CRDB Al Barakah” katika kipindi cha mwaka mmoja tokea kuzinduliwa kwa huduma hizo.

Taarifa hiyo imetolewa na Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Verde iliyopo mkoa wa Mjini Magharibi, iliyohudhuriwa na zaidi ya wateja 500.
Akitoa salamu maalum za mwezi mtukufu, Mwile aliwashukuru wateja kwa imani ambayo wameionyesha katika huduma za Benki ya CRDB zinazopatikana kupitia “CRDB Al Barakah”, akieleza kuwa hiyo inaonyesha ni kwa namna huduma hizo zimekidhi mahitaji ya wateja.

“Idadi hii ya wateja ni ndani ya mwaka mmoja kuanzia 2021 tulipozindua kwa mara ya kwanza hadi tunafunga mwaka 2022. Haya ni mafanikio makubwa sana kwetu, lakini tunajivunia pia kufanya uwezeshaji wa zaidi ya Shilingi Bilioni 73 kwa watu binafsi, na biashara,” alisema.

Akiwahimiza wale ambao hawajajiunga na mfumo huo wa CRDB Al Barakah, Mwile alisema mfumo huo una huduma zinazogusa makundi yote ya wateja, ikijumuisha akaunti binafsi na za biashara, na huduma za ufadhili binafsi na biashara kupitia mfumo usioambatana na riba, ambao kitaalamu unajulikana kama Murabaha.

Mwile alibainisha kuwa huduma za CRDB Al Barakah zinapatikana kupitia mtandao wa matawi ya Benki ya CRDB kote nchini, lakini pia katika hali ya kusogeza huduma kwa wateja baadhi ya huduma ikiwamo zile za kufungua “Al Barakah Account” na ukataji wa bima sasa hivi zinapatikana kupitia CRDB Wakala waliosambaa nchi nzima.
Akizungumza kwa niaba ya wateja wa Benki hiyo, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Mudrick Soraga aliipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio ambayo imeyapata kupitia mfumo wa CRDB Al Barakah.

Waziri Soraga alibainisha kuwa mfumo huo umesaidia kuchochea kwa kiasi kikubwa ujumuishi wa kifedha visiwani humo. Aliwataka Watanzania ambao wamekuwa nje ya mfumo rasmi wa kibenki kutokana na kukosa huduma zinazoendana na imani yao kuchangamkia fursa ya CRDB Al Barakah kujijenga kiuchumi.
Akielezea juu ya umuhimu wa kujitoa kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Waziri Soraga aliipongeza Menejimenti ya Benki ya CRDB kwa kuendeleza utamaduni wake wa kuuandaa  na kushiriki futari na wateja, wadau na wenye uhitaji katika jamii katika kipindi cha mwezi huu.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kujikita katika ibada kwa kuishi kwa matendo mema katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na baada ya mwezi mtukufu kwani matendo mema hayana ukomo wala kipindi maalum.

Katika hafla hiyo ya futari, pia ilitoa msaada wa futari vituo vya kulelea watoto yatima visiwani humo vya Jukumakhe kilichopo Melitano,  na  Sebleni Masjid Jumma, ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia watoto wetu kufanikisha funga ya Ramadhani.
Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na uwezeshaji kwa wajasiriamali wadogo.

Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moody’s Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji. Moody’s imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara. 
 
Benki ya CRDB imepata utambuzi wa Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UN Green Climate Fund) tangu mwaka 2019 na pia imetambuliwa kama benki bora Tanzania na jarida la Global Finance kwa mwaka 2020.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad