HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 29, 2023

TUGHE- TCAA WAASWA KUTUMIA VIKAO KUZALISHA HOJA ZENYE KULETA MABADILIKO CHANYA KATIKA TAASISI

 


Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wametakiwa kutumia mikutano ya vyama vya wafanyakazi kujadili na kuja na mapendekezo yatakayoleta mabadiliko chanya katika taasisi.

Hayo yameelezwa leo Aprili 29, 2023 na Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa TCAA Bw. Daniel Malanga alipomuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari wakati wa kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

"Tunatambua umuhimu wa chama cha Wafanyakazi katika kuchagiza mafanikio ya mamlaka, rasilimali watu ni muhimu kwa maendeleo ya taasisi kwahiyo TUGHE ina wajibu wa kuhakikisha inazungumza vyema na watumishi pamoja na kuwa na semina za mara kwa mara kwaajili ya kuwajengea uwezo chanya wanachama wake ,"amesema Bw. Malanga

Kiongozi huyo amepongeza uongozi na wanachama wa TUGHE kwa kuandaa vyema mkutano huu wa mwaka jambo linalowapa fursa ya kujadili kwa mapana taarifa mbalimbali za kiutendaji ndani ya chama na hatimaye kuandaa mapendekezo yatakayoleta tija ndani ya taasisi.

Pia amesema vikao hivi ni muhimu kwa kuwa vinaleta mshikamano na umoja kwa wafanyakazi ikiwemo kujadili changamoto wanazozipata wafanyakazi na kuzitafutia ufumbuzi kwani wao ni kama daraja kati ya utawala na wafanyakazi.

Mbali na hayo, Bw. Malanga aliwataka watumishi wa TCAA kuwasilisha changamoto wanazokumbana nazo kwa mamlaka husika badala ya kusubiri vikao vya TUGHE kueleza changamoto wanazopitia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la TCAA Jackline Ngoda, amesema lengo la kufanya kikao hicho ni kuwakumbusha watumishi wajibu wao katika utendaji ikiwa na kauli mbiu isemayo kuchaguza wafanyakazi wa usafiri wa Anga kufanya kazi kwa ufanisi na juhudi kwani hilo ndilo lengo la kuweza kuipaisha mamlaka hiyo.

Akitoa mada katika mkutano huo, Katibu wa TUGHE mkoa wa Morogoro Bw. Anthelmus Tarimo ametoa wito kwa wanachama wa TUGHE tawi la TCAA kuwa mfano wa kuigwa katika eneo la kazi kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia miongozo na taratibu za kazi.

“Inapendeza sana kuona wewe mwanachama wa TUGHE unakuwa ndio kioo kinachoonesha taswira njema pale pale kwenye eneo la kazi, ifike mahali watumishi wenzako watamani kuwa wanachama wa TUGHE kwa vile wanavyosadifu mienendo yako” alisema Bw. Tarimo.
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa TCAA Bw. Daniel Malanga akizungumza wakati wa kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bi. Jackline Ngoda akizungumza kuhusu namna wanavyoshirikiana na viongozi wa TCAA pamoja na kumkaribisha Mgeni rasmi.
Katibu wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),Bw. Shukuru Mhina akifanywa utambulisho wa wajumbe wa mkutano mkuu wa mwaka wa TUGHE tawi la TCAA kwa Mgeni rasmi.
Katibu TUGHE mkoa Morogoro Anthelmus Tarimo akitoa mada wakati wa mkutano wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa TCAA Bw. Daniel Malanga na Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la TCAA, Bi. Jackline Ngoda wakifuatilia mada katika.
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakifuatilia mada wakati wa mkutano wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad