HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 5, 2023

SERIKALI IMEPOKEA MATOKEO YA UFUATILIAJI NA TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KUKABILIANA NA UVIKO-19

 Na Joseph Mahumi na Farida Ramadhani

SERIKALI imepokea Matokeo ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa Kukabiliana na Madhara ya Kijamii na Kiuchumi ya UVIKO-19 yaani (Tanzania Covid-19 Socio-Economic Response and Recovery Plan - TCRP) kupitia fedha za mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Matokeo hayo yamewasilishwa jijini Dodoma na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. William Mwegoha, kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamadi Hassan Chande.

Akizungumza katika hafla ya kupokea taarifa ya ufuatiliaji na tathimini ya matokeo hayo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamadi Hassan Chande, alisema matokeo hayo yana umuhimu mkubwa kwa kuwa tukio hilo linadhihirisha dhana muhimu za uwajibikaji, ushirikishwaji na uwazi katika utekelezaji wa miradi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo inasimamiwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema manufaa yanayotokana na Mpango wa Kukabiliana na Madhara ya Kijamii na Kiuchumi ya UVIKO-19 nchini ni ya kudumu na yanagusa wananchi wote Bara na Visiwani kwenye sekta za afya, elimu, maji, utalii, kusaidia kaya maskini, makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye walemavu.

“Katika Sekta ya Maji, tumenunua mitambo 25 seti tano (5) za mitambo ya uchimbaji na ujenzi wa mabwawa, na seti nne (4) za vifaa vya uchunguzi wa maji chini ya ardhi na kwenye Sekta ya Elimu tumejenga madarasa 12,000 katika shule za sekondari na madarasa 3,000 ya shule za msingi shikizi, ununuzi wa madawati na ujenzi wa mabweni 50 kwa ajili ya wanafunzi wa kike wenye mahitaji maalum”, alisema Mhe. Chande.

Aliongeza kuwa katika elimu pia kulikuwa na ujenzi wa vyuo vinne (4) vya VETA vya mikoa ya Rukwa, Geita, Simiyu na Njombe na ujenzi wa vyuo 25 vya VETA vya wilaya.

Mhe. Chande alisema Serikali imeimarisha taasisi za Sekta ya Utalii zilizoathiriwa kwa kiasi kikubwa na UVIKO-19, ikiwemo TANAPA, TAWA na NCAA na kubainisha mapato ya taasisi hizo yameshaanza kurejea katika viwango vya awali vya kabla ya UVIKO-19.

“Mafanikio mengine ni kununuliwa kwa mitambo mitano (5) kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya hifadhi 13 za Taifa; na Kuimarishwa kwa mifumo ya utangazaji wa fursa za utalii ikiwemo Royal Tour”, alisema.

Alisema Serikali imefanikiwa kujenga na kukarabati miundombinu ya vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali 70, miundombinu ya kutolea Huduma za Dharura (EMD) katika hospitali 101 na kununua magari 663 yakiwemo magari 373 ya huduma ya kwanza (basic ambulance).

Mhe. Chande alisema pia kuwa Serikali imenunua magari 20 ya kutolea huduma ya kwanza ya kisasa (advanced ambulance) na magari ya kawaida 270 kwa ajili ya huduma za chanjo katika mikoa na halmashauri pamoja na kampeni za kuhamasisha uchomaji wa chanjo na ununuzi wa vifaa tiba zikiwemo mashine za X-ray, CT-Scan, mashine za huduma za uchunguzi wa moyo (Echo Cardiography) na MRI.

Kwa upande wake Naibu Katibu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaabani alisema kuwa Serikali ilipata mkopo usio na riba kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kiasi cha shilingi trillion 1.3, ambazo ziliekezwa kutatua changamoto zilizotokana na athari za UVIKO-19.

Alisema kuwa kiasi halisi kilichopokelewa kilikuwa shilingi trilioni 1.29130.18 kutokana na mabadiliko ya thamani ya kubadilisha fedha za kigeni, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 1.061 kilitumika kutekeleza miradi upande wa Tanzania Bara na kiasi cha shilingi bilioni 230.1 kilipelekwa Zanzibar na kwamba Serikali imekwisha toa zaidi ya shilingi trilioni 1.242 sawa na utekelezaji wa zaidi ya asilimia 96.

Bi. Amina Khamisi Shaaban alisema kuwa majukumu ya Wizara ya Fedha na Mipango katika utekelezaji wa mradi huo lilikuwa kusimamia mgawanyo wa fedha za mkopo, utoaji wa fedha kwa sekta husika, utoaji wa misamaha ya kodi, kufanya ufuatiliaji na tathimini (M&E) ya utekelezaji wa miradi, kufanya ukaguzi wa ndani na kufuatilia uzingatiaji wa makubaliano ambayo Serikali iliingia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Alisema Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifanya zoezi la kuchakata na kutoa misamaha ya kodi iliyopokelewa kutoka sekta zinazotekeleza miradi inayogharamiwa na fedha za UVIKO-19 ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi haikwami.

“Katika kipindi cha utekelezaji, TRA ilipokea jumla ya maombi ya misamaha kwa miradi 152. Kati ya miradi iliyowasilishwa, miradi 148 ilipata hati za msamaha wa kodi na miradi minne (4) kutoka RUWASA ilikosa msamaha kutokana na mapungufu yaliyobainika ya kusainiwa kwa mkataba ukiwa na kipengele cha kulipa kodi (Tax inclusive)” Alisema Bi. Amina.

Naye Mwenyekiti wa Bunge, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya bajeti, Mhe. Daniel Baran Sillo, alitoa rai kwa Serikali kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa kufuata mfumo wa ufatiliaji na tathmini ili kuongeza ufanisi na kuepusha hoja za kikaguzi.

Akiwasilisha matokeo hayo, Prof. Henny Moleli alisema tahmini hiyo ilifanyika kuanzia mwezi Novemba 2021 hadi June 2022 na madhumini yake ni kuboresha utekelezaji wa mradi huo ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Alisema katika utafiti huo wamejifunza kuwa uratibu makini na ufuatiliaji wa karibu wa miradi iliyokusudiwa viliongeza uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wake huku akibainisha kuwa force accounts na manunuzi ya kimkakati zimekuwa na ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Aidha, alibainisha kuwa baadhi ya changamoto zilizobainika ni mchakato wa manunuzi, ardhi kwa ajili ya kujengea miundombinu, hali ya hewa, kuongezeka kwa gharama za ujenzi na kusahaulika kwa baadhi ya miundombinu wakati wa ujenzi kama vila miundombinu ya vyoo, mifumo ya maji na gasi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akipokea matokeo ya ufutiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Kukabiliana na Athari za Kijamii na Kiuchumi zitokanazo na UVIKO-19, kutoka kwa Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) (Katikati walioketi), Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamisi Shaaban na Mwenyekiti wa Bunge na Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge, Mhe. Daniel Sillo, wakiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na baadhi ya wabunge wengine walioshiriki wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mpango wa kukabiliana na athari za kijamii na kiuchumi zitokanazo na UVIKO-19, iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad