HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, April 23, 2023

NSEKELA ATAJWA VIONGOZI 25 WENYE MCHANGO MKUBWA KIUCHUMI AFRIKA

Portsmouth, Uingereza – Akiwa na takribani miaka mitano tangu alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ametajwa na Jarida la African Leadership Magazine (ALM) la Uingereza kuwa miongoni mwa viongozi 25 wenye mchango mkubwa kwenye uchumi.

Tuzo hizo zilizotolewa na kutangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita zilipitia mchakato mrefu ulioihusisha bodi ya uhariri wa gazeti la ALM kutambua majukumu yanayotekelezwa na viongozi wa Serikali, kampuni binafsi hata mashirika ya kimataifa.

 Mhariri Mtendaji Mkuu wa Jarida la ALM, Kingsley Okeke alisema orodha ya viongozi hao imezingatia mchango wao katika uandaaji wa sera rafiki, uongozi makini na program ziligowagusa na kuwashirikisha wananchi wengi zaidi kwenye uchumi hivyo kusaidia kuviepuka vihatarishi vilivyojitokeza duniani na kusaidia kuufufua na kuukuza uchumi wa mataifa yao.

"Orodha hii inayowajumuisha mawaziri wa fedha, magavana wa benki kuu na wakurugenzi watendaji wa benki pamoja na taasisi kubwa za fedha barani Afrika  imewamulika viongozi waliojitoa kwa upekee kusimamia maendeleo ya mataifa yao hasa kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo kushikiri kujenga uchumi kwa kuwapa fursa za mtaji na nyinginezo licha ya changamoto zinazoshuhudiwa kote duniani," amesema Okeke. 

Kuipata orodha hiyo, Okeke amesema kulikuwa na hatua mbili muhimu. Kwanza ni kutambuliwa kwa viongozi hao kulikofanywa na waandishi nguli wa jarida hilo waliopo katika mataifa tofauti duniani pamoja na wataalamu wa sekta ya fedha Afrika kabla bodi ya ALM haijawachuja na kuwatangaza baada ya kuwapigia kura kwa kuzingatia mambo waliyoyafanya kwenye mataifa yao.

Orodha ya washindi hao imetajwa siku chache baada ya hafla ya viongozi wa uchumi Afrika iliyofanyika jijini Washington DC nchini Marekani pembezoni mwa mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

 Akizungumzia tuzo hiyo, Nsekela alisema inamtia moyo kuona wadau wakubwa Jarida la ALM wanaona anachokifanya hivyo ataendelea kuweka mikakati makini kwa kushirikiana na Bodi na Menejimenti ya Benki ya CRDB kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapa fursa wanazostahili.

Tangu kuibuka kwa janga la Uviko-19, Nsekela amesema benki imebuni program kadhaa zilizotekelezwa nchini na kuwagusa wananchi wa kawaida pamoja na kuinua biashara za wajasiriamali kuanzia wadogo mpaka wakubwa.

"Kwa kipindi chote, Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa imara ikitoa miongozo iliyoturuhusu tufanye biashara kwa umakini licha ya changamoto zilizokuwapo  wakati tukipambana na majanga yote kuanzia Uviko-19, kupanda kwa bei ya mafuta na sasa vita kati ya Russia na Ukraine," amesema Nsekela.

Ndani ya miaka mitano iliyopita, Benki ya CRDB imetekeleza program zilizorahisha upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi na sekta ya umma. Ili kuongeza uwezo wa kuwahudumia wajasiriamali wengi zaidi, Benki ya CRDB imekuwa ikishirikiana na wadau kadhaa wa kimataifa kuimarisha mtaji wake. Mwaka jana Benki hiyo ilikusanya zaidi ya TZS 500 billion kwa ajili ya uwezeshaji wa wajasiriamali nchini huku mkazo mkubwa ukiwekwa kwa wajasiriamali wanawake.

Benki hiyo pia imekuwa ikichukua hatua ya kupunguza riba kama sehemu ya kusaidia jitihada za serikali kuimarisha uchumi. Mwaka jana Benki ya CRDB ilipunguza  riba kwenye mikopo ya kilimo kutoka asilimia 20 mpaka asilimia 9, jitihada ambazo zilienda sambamba na kupunguzwa kwa riba ya mikpo ya wafanyakazi hadi asilimia 13.

Nsekela anaeleza kuwa Benki hiyo pia imekuwa ikishirikiana kwa karibu na serikali katika kuwawezesha wafanyabiashara wago, wamamchinga. Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetenga Shilingi Bilioni 60 kwa ajili ya kusaidia kukukuza uchumi wa buluu kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa wajasiriamali wadogo visiwani humo.

"Bado kuna mengi ya kufanya kuwawezesha wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo kwenye maeneo yao. Benki ya CRDB inaendelea kujitanua Ili iwafikie popote walipo. Hivi karibuni tumefungua matawi mapya; Shirati , Bukombe, Ikwiriri, Mafia, Kilwa Kivinje, Liwale, Kaliua, na Nkasi Ili kufikisha huduma zetu,” amesema Nsekela huku akigusia kuwa upanuzi huo wa matawi unaenda sambamba na upanuzi wa kikanda na kuwa Benki hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuingia nchini Congo.

Alibainisha kuwa Benki hiyo pia inaendelea kuimarisha majukwaa yake ya huduma za kidijitali na mtandao wa CRDB Wakala ambao sasa ina mawakala zaidi ya 25,000 kote nchini. “Tunaamini iwapo kila mwananchi atatumia huduma za benki mahali alipo, itarahisisha kukuza kipato chake hivyo kukuza uchumi wa Taifa," amesema Nsekela.

Mapambano dhidi ya UVIKO-19 yaliposhika kasi zaidi mwaka 2020, Benki ya CRDB ilichukua hatua kadhaa kuwainua wajasiriamali na wafanyabiashara hasa katika sekta ya utalii wasianguke. Juhudi hizo ziliifanya CRDB ikopeshe zaidi ya TZS 6.9 trilioni mwaka 2022, nakushuhudia Benki hiyo ikipata ukuaji wa faida wa asilimia 31 kufikia TZS 351.4 bilioni, kutoka TZS 268.2 bilioni mwaka 2021.

Viongozi wengine waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Ahmed Shide, waziri wa Fedha wa Ethiopia, Rindra Rabarinirinarison, waziri wa Uchumi na Fedha Madagascar na

Mamadou Moustapha Bâ, waziri wa Fedha na Bajeti wa Senegal. Mawaziri wengine ni Zainab Ahmed wa Nigeria,

Dk Renganaden Padayachy wa Mauritius, Samuel Tweah wa Liberia, Matia Kasaija wa Uganda na Adama Coulibaly wa Ivory Coast.

Pia yumo Gavana Lesetja Kganyago wa Benki Kuu ya Afrika Kusini, Johnny Damian wa Benki Kuu ya Sudan Kusini, Dk Patrick Ngugi Njoroge, gavana wa Benki Kuu ya  Kenya, Dkt Ernest Addison wa Benki Kuu ya Ghana, John Rwangombwa wa Rwanda, Caroline Abel wa Benki Kuu ya Seychelles na José de Lima Massano wa Benki Kuu ya Angola pamoja na Dkt John Mangudya, gavana wa Benki Kuu ya  Zimbabwe.

Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfFB), Dk Akinwumi Adesina naye ametajwa pamoja na Dkt Adesola Kazeem Adeduntan, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya First Bank ya Nigeria, Mwenyekiti wa Heirs Holding, Tony Elumelu, na Profesa Benedict Oramah, Rais wa Benki ya African Export–Import (Afreximbank).

Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Rokel, Dkt Walton Gilpin nchini Sierra Leone, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Group, Simphiwe Tshabalala,  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya BMCE, Othman Benjelloun ya nchini Morocco na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara ya Zambia (Zanaco), Mukwandi Chibesakunda.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad