Na Mwandishi wetu
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata watu watano kwa tuhuma za kosa la kuharibu mali na kufanya mkusanyiko usio halali katika ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kishiri ‘A’ Wilaya ya Nyamagana.
Katika Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi (M) Mwanza, SACP Wilbrod W Mutafungwa imesema kuwa Tarehe 27.04.2023 majira ya saa 20:00 huko katika kiwanja cha Ofisi ya Serikali za Mtaa wa Kishiri ‘A’, Kata ya Kishiri, Wilaya ya Nyamagana, msanii wa nyimbo za asili aitwaye Mateso Julius, miaka 27, msukuma, mjasiliamali na mwanamziki akiwa na wenzake wa 04, waliandaa tamasha la muziki katika kiwanja hicho bila kuwa na kibali cha kufanya tamasha hilo.
Baada ya kusikia kelele za muziki huo, Afisa Mtendaji wa kata hiyo John Mwakalasya, Miaka 33, Mnyakyusa alifika katika eneo hilo na kuwaomba kibali cha kufanya tamasha hilo ambapo alibaini kuwa wanamziki hao hawakuwa na kibali hivyo, aliwataka waache kuandaa tamasha hilo hadi watakapopata kibali.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Wasanii hao walikaidi maelekezo hayo na kuendelea kuandaa tamasha huku wakipiga mziki kwa sauti ya juu wakiwa na spika zilizokuwa ndani ya Gari lao aina ya Canter namba T. 235 DFK. Afisa mtendaji aliwasisitiza tena kuacha mara moja kufanya tamasha hilo na kuondoka eneo hilo ndipo wasanii hao walianza vurugu za kurusha mawe kwenye ofisi ya mtendaji kata ambapo walivunja vioo vya madirisha ya ofisi hiyo.
Taarifa hizo ziliripotiwa kituo cha Polisi Nyakato kwa haraka Askari walifika eneo la tukio na kuwaamuru wanamziki hao kuacha kuendesha tamasha hilo bila kibali ambapo walikaidi, ndipo Askari walitawanya mkusanyiko huo usio wa halali na kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni:-
1. Mateso Julius, miaka 27, msukuma, mjasiliamali na mwanamziki
2. Samson Sylvester, Miaka 30, Msukuma, Mjasiliamali Na Mkazi Wa Kalemela,
3. Magereza Lazaro. Miaka 30, Msukuma Na Mkazi Wa Geita,
4. Lucas Samson, Miaka 21, Msukuma, Mkulima, Mkazi wa Geita Pamoja na
5. Emmanuel Ntambi, Miaka 30, Msukuma, Mkulima, Mkazi Wa Kanindo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa rai kwa wananchi kufuata sheria na taratibu za kufanya tamasha na kupiga muziki katika maeneo yenye makazi ya watu. Pia, linawasihi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu ili ziweze kufanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment