NA MWANDISHI WETU, DODOMA
Kampeni
ya Benki ya NMB ya kuongeza miti milioni moja katika ajenda ya serikali
ya kuyatunza mazingira na kupambana na athari za tabia nchi imewakosha
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakiongozwa
na Spika Dkt Tulia Ackson, wawakilishi hao wa wananchi bungeni wameisifu
taasisi hiyo kwa mradi huo mkubwa na wa kipekee nchini wengi wakisema
ni wakizalendo na wenye manufaa makubwa kwa maendeleo ya taifa na maisha
ya viumbe hai kwa ujumla.
Bunge limeahidi kushiriki kikamilifu
katika utekelezaji wake na kuhakikisha kampeni hiyo ya kuikijanisha
Tanzania inazaa matunda yaliyokusudiwa.
Wabunge hao walibainisha
azma hiyo mwishoni mwa wiki jana baada ya kuvutiwa na uwekezaji huo na
kuobwa na uongozi wa NMB kusaidia kuipeleka kampeni hiyo majimboni mwao.
Benki
hiyo iliomba ushirikiano wa Bunge na wajumbe wake kwenye hafla ya Iftar
ambayo iliiandaa Ijumaa bungeni ikiwa ni mwendelezo wa utamaduni wake
wa kushirikiana na waumini wa dini ya Kiislamu kwenye Mfungo wa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani.
NMB imekuwa na utaratibu wa kuwafuturisha
wadau na washirika wake likiwemo Bunge ambalo mara hii limetumia fursa
hiyo kuipongeza taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini kwa ukarimu huo na
pia kuimwagia sifa kwa ushirki wake mkubwa katika ujenzi wa taifa na
maendeleo ya Watanzania.
Mara baada ya futari hiyo ya kukata
na shoka, Dkt Tulia aliipongeza NMB sio tu kwa kudumisha utamaduni wa
kufuturisha bungeni, bali pia kwa kubuni kampeni endelevu ya upandaji
miti na kuona umuhimu wa ushiriki wa wabunge kuifanikisha.
Kiongozi
huyo alisema wameipokea kampeni hiyo iliyozinduliwa kitaifa Machi 27 na
Makamu wa Rais, Dkt Philip Isidor Mpango, jijini Dodoma na kwa niaba ya
wabunge wote kuahidi kuifanyia kazi.
Aidha, Dkt Tulia
aliishukuru NMB kwa kutambua umuhimu wa kufanya ibada ya kufuturisha kwa
kushirikisha wabunge, na kwamba kwa kufanya hivyo, benki inakuwa
imeshirikisha wananchi wao, ambao wanawawakilisha bungeni.
"Sisi
kama Bunge tumefurahishwa na mipango yenu yote iliyoelezwa na Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu , ambayo ni chanya na yenye manufaa makubwa kwa
jamii na taifa kwa ujumla wake. Mipango hiyo ni muendelezo, kwani nina
uhakika kila mbunge hapa jimboni kwake NMB imeacha alama kupitia
uwajibikaji wake kwa jamii (CSR).
"Vitabu vyenu vya mapato
vinaonesha mko vizuri na vinaakisi mchango mkubwa mnaoutoa kwa maendeleo
ya taifa kutokana na kodi kubwa mnazolipa. Na kama haitoshi mnakuja na
mipango muhimu kila uchao, ukiwemo huu wa upandaji miti milioni moja
kote nchini mwaka huu,” alibainisha na kuongeza kuwa:
"Jambo hili
ni la heri sana kwa ustawi wa mazingira yetu na kuwezesha vita ya
kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi. Nashukuru mmewataka
wabunge kushirikiana nanyi kwa kuipeleka kampeni majimboni, nasi
tunaahidi kufanya hivyo, tunaomba tu uwepo wepesi wa kutufikia kila
tutakapowahitaji.”
Kwenye mahojiano baada ya kufuturu, baadhi ya
wabunge, mbali na kuishukuru NMB kwa futari na kuisifu kwa ajenda yake
ya kuchangia maendeleo endelevu, pia walisema benki hiyo ni kinara wa
kulihudumia taifa kupitia ubunifu wa kidijitali na suluhisho za kifedha
za viwango vya kimataifa.
Wabunge hao ambao ni pamoja na Mbunge
wa Nyangwale, Bw Nassor Ammar, Mbunge wa Viti Maalujm, Bi Hawa Mchafu,
na Mbunge wa Sengerema, Bw Hamis Tabasamu, walibainisha pia kuwa NMB
inaongoza kwa kuwekeza katika miradi ya kijamii.
Aidha, walisema
bajeti zake za CSR ni kubwa sana na ambazo ni mfano wa kuigwa kwa
kusaidia kununua maelfu ya madawati kote nchini, kujenga madarasa na
vyoo mashuleni, kuchangia vitanda mahospitalini, mashuka na vifaa
vingine vya kuboresha utoaji wa huduma za afya.
NMB hutumia
asilimia moja ya faida yake baada ya kodi kila mwaka kwa ajili ya
kurudisha fadhila kwa jamii na kusaidia kutatua changamoto za wananchi,
kiasi ambacho kwa mwaka huu, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Filbert Mponzi
alisema kimeongezeka hadi TZS bilioni 6.2.
Akifafanua, Bw Mponzi
alisema hii ni kutokana na Bodi ya Wakurugenzi kuidhinisha TZS bilioni 2
zaidi kwa ajili ya ajenda ya uendelevu yakiwemo masuala ya mazingira
ambayo mradi wa kupanda miti milioni moja ni sehemu ya ufadhili huo mpya
wa maendeleo endelevu wa NMB iliyopata faida ya TZS bilioni 429 mwaka
2022..
"Tumejipanga kupanda miti milioni moja kote nchini na hapa
tutoe ombi kwa wabunge watusapoti kwa kupeleka kampeni hii katika
maeneo yenu. Kwahiyo nawaomba wabunge wachangamkie fursa hii ili kuunga
mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia na Makamu wake Dkt Mpango za
kuboresha na kuhifadhi mazingira," alibainisha
Afisa huyo
mwandamizi pia akaeleza ya kuwa, yote hayo kwa mwaka huu yanaenda
sambamba na sherehe zao za kutimiza miaka 25 ya kutoa huduma za kibenki
nchini huku Bunge likichangia mafanikio makubwa waliyopata.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dkt Edwin Mhede, alitumia nafasi hiyo
kuihakikishia Serikali na wanahisa wengine, kwamba pesa za hisa zao na
mali ziko salama NMB, kwani wanajivunia uimara wa mtaji, thamani na
faida wanayopata mwaka baada ya mwaka.
Spika wa Bunge ,Dk Tulia Ackson (katikati) akikaribishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB - Dk Edwin Mhede (kulia) walipokutana kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na benki ya NMB kwa Wabunge mwishoni wa wiki Bungeni Jijini Dodoma. kushoto ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki ya NMB - Filbert Mponzi
Spika wa Bunge ,Dk Tulia Ackson (kulia) akikaribishwa na Afisa Mkuu wa Wateja wa Binafsi na Biashara wa benki ya NMB - Filbert Mponzi (katikati) walipokutana kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na benki ya NMB kwaajili ya Wabunge mwishoni wa wiki Bungeni Jijini Dodoma. kushoto kabisa ni Shekhe wa Mkoa wa Dodoma Shekhe Mstafa Rajabu.
Spika wa Bunge ,Dk Tulia Ackson (katikati) akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya NMB ,Dk Edwin Mhede pamoja na Afisa Mkuu wa Wateja wa binafsi benki ya NMB Makao makuu ,Filbert Mponzi walipokutana kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na benki ya NMB kwa Wabunge mwisho wa wiki Bungeni Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment