HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 4, 2023

HATI ZA HAKIMILKI ZA KIMILA 70,000 KUTOLEWA TANGANYIKA

 Na. Magreth Lyimo, WANMM

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Kuboresha Usalama wa Milki za Ardhi imejipanga kutoa hati za hakimilki za kimila 70,000 kwa wananchi katika Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi ambapo katika awamu ya kwanza ifikapo Juni 2023 hati za hakimiliki za kimila takriban 20,000 zitakuwa zimetolewa.

Hayo yalisemwa na Mratibu wa Mradi huo Bw. Joseph Shewiyo wakati timu ya wataalam kutoka Benki ya Dunia pamoja na timu ya wataalam wa Mradi ilipotembelea Vijiji vya Ikaka na Kamsanga vilivyopo katika Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi tarehe 03/04/2023 kwa lengo la kujionea maeneo ambayo mradi huo utatekelezwa kwa upande wa Vijijini.

Bw Shewiyo alisema ‘‘Wilaya ya Tanganyika itaanza moja kwa moja na zoezi la utoaji hati za hakimilki za kimila kwa kuwa tayari Wilaya hiyo ina Mpango wa Matumizi ya ardhi ya Wilaya ambapo jumla ya Vijiji 29 katika Wilaya hiyo vina Mipango ya Matumizi ya ardhi ya Vijiji na vyeti vya ardhi vya vijiji’’.

Mratibu wa Mradi huo alifafanua kuwa katika wilaya hiyo hatua itakayofuata ni kutoa elimu kwa wananchi katika vijiji hivyo ili kuwa na uelewa wa pamoja wa namna zoezi hilo litakavyokuwa shirikishi kuanzia hatua ya upimaji hadi ugawaji wa hati hizo.

Katika ziara hiyo Meneja mradi upande wa Vijijini Bw. Osena Joseph alisema kuwa mradi umejikita kutoa jumla ya hati za hakimilki za kimila 500,000 katika wilaya saba ambapo alifafanua kuwa mpaka sasa wilaya sita ambazo ni Mbinga, Songwe, Chamwino, Maswa, Mufindi, Longido zinakamilisha uandaaji wa Mpango wa Matumizi ya ardhi ya Wilaya.

Aidha Bw. Osena amewaomba Wananchi katika Wilaya ya Tanganyika kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaokuwa wanatekeleza mradi huo ili zoezi hilo liweze kwenda kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa na kuwashauri kumaliza migogoro ya mipaka ya maeneo yao mapema ili wataalamu watakapofika katika maeneo yao wawe na kazi nyepesi ya kutambua mipaka na kuwapimia ili wapate Hati zao ndani ya muda uliopangwa.

Kwa upande wake Bw. Martin Msungwi ambae ni mkazi wa Kijiji cha Ikaka amesema kuwa wanamshukuru Mungu pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu kwa kuwapelekea mradi huo kwani taratibu za kupimiwa na kupata Hati zilikua ndefu na ngumu ila mradi huo umewafuata mpaka Vijijini hivyo wapo tayari kutoa ushirikiano muda wowote utekelezaji utakapoanza.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji kutoka Kijiji cha Kamsanga Bi. Edina Kadyege amesema kuwa ujio wa mradi huo ni ukombozi kwao kwani hapo awali walikua wanashindwa kukopesheka au kuwekeana dhamana kutokana na kutokua na Hati lakini wanaamini baada ya utekelezaji wa mradi huo watakua wanamiliki maeneo yao kisheria ambapo itawawezesha kufanya shuguli za kimaendeleo na ulinzi wa kudumu wa maeneo yao.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ni mradi unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa muda wa miaka mitano (2022/2027) ukiwa na lengo la kuboresha usalama wa milki za ardhi nchini lakini pia kuzingatia haki za umiliki wa ardhi kwa makundi maalum kama vile wafugaji na wakulima, wanawake, vijana, walemavu, wazee na watoto.
Meneja Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kwa upande wa Vijiji Bw. Osena Joseph akiwa pamoja na Mtaalam kutoka Benki ya Dunia Bw. Camille Bourguignon walipokuwa wanatembelea baadhi ya vijiji ambavyo vitanufaika na mradi huo katika Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.
Wataalam kutoka Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi pamoja na wataalam kutoka Benki ya Dunia wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Katavi wakati walipokuwa katika ziara ya kutembelea maeneo ya mradi katika Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad