HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 10, 2023

MKANDARASI WA UJENZI WA JENGO LA TSC, SUMA JKT ATAKIWA KUONGEZA NGUVUKAZI KUKAMILISHA MRADI KWA WAKATI


Mwonekano wa hatua iliyofikiwa katika mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za TSC Makao Makuu unaofanyika katika eneo la Ndejengwa jijini Dodoma.

 

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za TSC Makao Makuu, SUMA JKT wakati wa ziara yake katika eneo la mradi, Ndejengwa jijini Dodoma Machi 9, 2023.
Msimamizi wa Mradi kutoka SUMA JKT, Maj. Samwel Jambo (mwenye sare za jeshi) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za TSC Makao Makuu katika eneo la Ndejengwa jijini Dodoma wakati Naibu Waziri huyo alipofanya ziara katika eneo hilo Machi 9, 2023.


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) akiwasili katika eneo la Ndejengwa jijini Dodoma ambapo ndipo unapotekelezwa mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za TSC Makao Makuu. Katika ziara hiyo iliyofanyika Machi 9, 2023 Naibu Waziri huyo aliambatana na Mejejimenti ya TSC.

Na Mwandishi wetu – Dodoma.
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mkandarasi, SUMA JKT anayejenga jengo la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuongeza nguvukazi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Machi 9, 2023 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya TSC Makao Makuu katika eneo la Ndejengwa jijini Dodoma ambapo alibaini kuwa mradi huo upo nyuma ikilinganishwa na mpango kazi wa utekelezi wa kazi hiyo.

“Hapa ni lazima muone namna ya kufanya ili utekelezaji wa mradi huu uendane na mpango kazi mliokubaliana kwenye mkataba. Kwa mujibu wa mpango kazi ilitakiwa wakati huu mmefikia asilimia 16 ya utekelezaji wa mradi, lakini hadi sasa bado mpo nyuma. Ongezeni nguvukazi ili kuharakisha ujenzi kwa kuwa tunataka kila hatua iendane na mpango kazi wetu na hatimae mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa bila kuongeza muda,” amesema Naibu Waziri huyo.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa jengo hilo ni muhimu sana kwa kuwa kwa sasa TSC inafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na upungufu wa vyumba vya ofisi kwa ajili ya watumishi na uhifadhi wa nyaraka mbalimbali za walimu, hivyo ujenzi huo unatakiwa ukamilike kwa wakati ili kuondokana na adha hiyo.

“Mazingira wanayofanyia kazi TSC kwa sasa hayaendani na uzito wa majukumu waliyonayo, wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya ofisi za watumishi na vyumba vya kutunzia nyaraka mbalimbali. Hivyo, tunawategemea sana mkamilishe mradi huu kwa wakati ili tuwaondolee adha ya kufanya kazi katika mazingira magumu,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri huyo alisema kwamba atafanya ziara katika mradi huo kila baada ya miezi mitatu ili kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa kasi na viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa mkataba.

Akizungumza kuhusu sababu ya mradi huo kuwa nyuma ya mpango kazi, Msimamizi wa Mradi kutoka SUMA JKT, Maj. Samwel Jambo amesema kuwa wakati wa kuchimba mashimo ya nguzo za jengo walikuta mwamba mgumu ambao ulilazimu kutafuta vifaa vya ziada kwa ajili ya kuutoboa, hivyo kupunguza kasi ya ujenzi huo.

Hata hivyo, msimamizi huyo amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Naibu Waziri na watayafanyia kazi kwa haraka ili kuhakikisha ujenzi huo unaendana na mpango kazi wa mkataba na hivyo kufanya mradi ukamilike kwa wakati.

Naye Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama amesema ujenzi ukikamilika utasaidia Tume kutoa huduma kwa walimu kwa ufanisi zaidi huku akieleza kuwa ana imani kuwa mkandarasi huyo atakamilisha kazi kwa wakati.

“Mhe. Naibu Waziri sisi TSC tuna imaini kuwa walichokisema wenzetu SUMA JKT watakwenda kukitekeleza. Kwa kweli tangu tumeanza mradi huu tunakwenda nao vizuri, tunaamini kwamba watakamilisha kwa wakati ili tuweze kuhudumia walimu wetu kwa ufanisi zaidi,” amesema Mwl. Nkwama.

Mradi huo unaogharimu kiasi cha shilingi 6,499,982,353.03 ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 umeanza Desemba 6, 2022 na utakamilika ifikapo Juni 2, 2024. TSC tayari imelipa kiasi cha shilingi 500,000,000 ikiwa ni malipo ya wali ya kuanza utekelezaji wa mradi huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad