Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma Marco Chilya akionyesha sehemu ya mafuta yaliyokamatwa na jeshi hilo kutoka kwenye ujenzi wa mradi wa barabara ya Amanimakolo-Ruanda wilayani Mbinga kufuatia misako mbalimbali inayoendelea kufanyika mkoani humo dhidi ya vitendo vya uharifu na waharifu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Marco Chilya kushoto,akikabidhi sehemu ya mafuta aina ya Dizel kwa meneja mradi wa kampuni ya China Railway Group Ge Guanghua yaliyokamatwa na Jeshi hilo kutoka kwenye ujenzi wa mradi wa Barabara ya lami ya Amanimakolo-Ruanda mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma Marco Chilya katikati,akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa kampuni ya China Railway Group inayojenga mradi wa Barabara ya Amanimakolo-Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilomita 35.
Na Muhidin Amri, Songea
JESHI la polisi mkoani Ruvuma ,limekabidhi jumla ya lita 630 ya mafuta ya Dizel kwa uongozi wa kampuni ya China Railway Group inayojenga mradi wa barabara ya lami ya Amanimakolo -Ruanda yenye urefu wa kilomita 35.
Mafuta hayo yalikamatwa na askari wa jeshi hilo, yakiwa yanasafirishwa kutoka katika mradi huo na baadhi ya watu kwa nia ya kwenda kuyauza.
Akikabidhi mafuta hayo kwa uongozi wa Kampuni hiyo Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma Marco Chilya alisema kuwa,mafuta hayo yalikamatwa siku kadhaa zilizopita ambapo mtuhumiwa wa wizi huo ambaye hakumtaja jina amefikishwa mahakamani na kesi hiyo imemalizika na mtuhumiwa kupata hukumu ya kifungo.
Kwa mujibu wa Kamanda Chilya ni kwamba,baada ya kutolewa kwa hukumu huyo mafuta hayo yameamriwa yarudishwe kwa kampuni inayotekeleza mradi huo wa barabara ili waweze kuyatumia katika shughuli zao.
Kamanda Chilya,ametoa onyo kali kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya wizi,uharifu na kuhujumu mradi huo na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa mkoani Ruvuma kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha linawasaka na kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
Aidha,amewahakikishia raia wa kigeni wanaotekeleza mradi huo kwamba,jeshi hilo linaendelea kufanya misako,doria na operesheni mbalimbali ili kuhakikisha maeneo yote ya mkoa huo yanakuwa salama pamoja na eneo hilo la ujenzi wa Barabara.
Meneja mradi wa kampuni hiyo Ge Guanghua,amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kutokana na jitihada zilizofanikisha kukamatwa na kupatikana kwa shehena hiyo ya mafuta ambayo yaliletwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Ruvuma.
Guanghua,amehaidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa Jeshi la Polisi,na kutoa taarifa za uharifu na waharifu watakaobainika ili mradi huo uweze kumalizika kwa muda uliopangwa.
No comments:
Post a Comment