HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 9, 2023

ELIMU YA KODI YA MLANGO KWA MLANGO YAWANUFAISHA WAFANYABIASHARA WA MBAGALA

 




Wafanyabiashara wa Mbagala jijini Dar es Salaam wakipata elimu juu ya Kodi kutoka kwa maafisa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

WAFANYABIASHARA wa Mbagala wamenufaishwa baada ya kutembelewa na maafisa wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao walifika katika muduka kwa lengo la kuwapa elimu juu ya Kodi sambamba na kusikiliza changamoto zao ili kuweza kuzifanyia kazi kwa wakati na kuepusha usumbufu.

Hayo yamejiri wakati maafisa hao wakiendelea na kampeni ya elimu ya mlango kwa mlango kwaajili ya kuwaelimisha wafanyabishara wa Mbagala juu ya mambo mbalimbali yanayohusu ukusanyaji wa kodi sambamba na kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo katika masula ya ulipaji kodi na upatikanaji wa huduma za TRA.

Akielezea mwenendo kwa kampeni hiyo, Afisa wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa Mkoa wa kodi Temeke wa TRA, Hamisi Sanze amefafanua kuwa kampeni hiyo iliyoanza februari 27 mwaka huu, amesema kuwa zoezi hili linafanyika kwa wiki mbili ambapo linatarajiwa kukamillika Machi 12, 2023.

Pia, Sanze ameeleza kuwa, zoezi hilo limelenga kutoa elimu kwa Mlipakodi Mlango kwa Mlango juu ya mambo mbalimbali yanayohusu kodi pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa eneo la Mbagala.

“Tupo kwenye zoezi la elimu la mlango kwa mlango pamoja na kuchukua mrejesho wa kero mbalimbali kutoka kwa walipakodi kwa lengo la kuboresha Zaidi.”

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Victoria Mushi ameelezea kufurahishwa kwake na ujio wa Maafisa wa TRA katika eneo lao kwa sababu kufika kwao kumewanufaisha sana sio tuu kupata elimu lakini wameweza kuelezea changamoto zao na kupatiwa muongozo namna ya kutatua changamoto hizo.

Aidha, Victoria amewashauri maafisa hao kuendelea kuwatembelea ili kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi sambamba na kuendelea kuwapa elimu ya kodi kwa sababau kuna wafanyabishara wengi hawajui kazi za TRA na kodi wanazokusanya pamoja namna ya ulipaji kodi, pia itasaidia watu kulipa kodi kwa hiari bila ya usumbufu wowote.

“Mimi nashauri TRA waendelee na huduma hiyo ya kuwatembelea maofisini (katika biashara zao) kwa sababu sisi wafanyabiashara tunamalalamiko mengi kwa vile tukiwaeleza wanatuelewa na wanatushauri nini cha kufanya.”

Kwa upande wa Julius Mberwa ambae ni mfanyabiashara wa Chamanzi ameipongeza TRA kwa kusikiliza changamoto zao na kuzifanyiakazi akitolea mfano wa upatikanaji wa TIN (namba ya utambulisho wa Mlipakodi) kwa sasa umekuwa ni rahisi sana tofauti na ilivokuwa awali walivyokuwa wakipata changamoto kuzipata.

Kampeni ya elimu ya mlango kwa mlango kwa mlipakodi inafanyika mara kwa mara mikoa mbalimbali nchini kulingana na uhitaji wa kampeni hiyo katika eneo husika kampeni inalenga kutoa elimu ili kuongeza ulipaji kodi kwa hiyari.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad