Naibu Waziri Wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Nadir Abdul-latif Yussuf (aliyesimama) akizungumza na wawakilishi wa wafanyakazi wa ATCL wakati wa Kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa ATCL liliofanyika Visiwani Zanzibar. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi na kushoto ni Mwenyekiti COWTU (T) Tawi la ATCL Airport, Bw. John Kimario.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi (aliyesimama) akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa ATCL. Wengine pichani ni Naibu Waziri Wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Nadir Abdul-latif Yussuf (katikati) na Mwenyekiti COWTU (T) Tawi la ATCL Airport, Bw. John Kimario (kushoto).
Baadhi ya wawakilishi wa wafanyakazi wa ATCL wakifuatilia kwa makini ajenda mbalimbali wakati wa Kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa ATCL liliofanyika Visiwani Zanzibar.
Naibu Waziri Wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Nadir Abdul-latif Yussuf (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa wafanyakazi wa ATCL wakati wa Kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa ATCL liliofanyika Visiwani Zanzibar.
Serikali imetaka Wafanyakazi wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kuendeleza nidhamu kwenye utendaji wake ili kuleta matokeo chanya zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa ufunguzi wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa ATCL Mhe. Nadir Yussuf amesema wanatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi wa Kampuni hii lakini bado wanapaswa kuongeza juhudi ili kuiletea nchi sifa na kukuza uchumi wa Taifa letu kwa ujumla.
“Niwapongeza kwa uwezo na kasi ya kufanya mabadiliko kulingana na mahitaji ya biashara, ubunifu pamoja na mahusiano mema kwa jamii ikiwemo kuweza kurudisha kwa jamii ikiwa ni sehemu ya kujali wadau wenu lakini ongezeni juhudi”, alifafanua Mhe. Yussuf.
Amewataka Wafanyakazi hao kutumia mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mitano (5) iliyopita kama chachu na fursa ya kujitathmini kwa kina ili kujipanga kimkakati katika nyanja zote kitaifa na kimataifa kwa kuongeza umiliki wa soko ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema ATCL imefanikiwa kuongeza ndege na vituo vya safari za ndani na nje ya nchi tangu lianze kutekeleza mpango maalum wa ufufuaji wa Kampuni hiyo. Ametaja ndege hizo ni Dash 8 Q300 -1, Dash 8 Q400 -5, B787 –2 na A220-300 –4.
Kwa upande wa vituo vya safari, Mhandisi Matindi amesema vituo vimeongezeka kutoka vituo vinne (4) hadi kufikia vituo kumi na nne (14) kwa safari za ndani ya nchi na kwa safari za nje ya nchi kutoka kituo kimoja (1) hadi vituo kumi (10).
Katika utekelezaji wa Mpango wa ufufuaji, ATCL pia imefanikiwa kuongeza watumishi kutoka mia mbili (200) mwaka 2016 hadi kufikia mia sita thelathini na sita (636) mwaka huu.
No comments:
Post a Comment