HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 2, 2023

SERIKALI HAIJASITISHA MATUMIZI YA TAA ZA SOLA KATIKA UVUVI WA DAGAA ZIWA VICTORIA

 


Na Mbaraka Kambona, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema haijatoa agizo la kusitisha matumizi ya Taa za Sola katika uvuvi wa Dagaa kwenye Ziwa Viktoria ifikapo Januari Mosi, 2023, huku ikiwataka wavuvi kuendelea na shughuli zao kwa kuzingatia Sheria, Taratibu, Kanuni Miongozo inayosimamia shughuli za uvuvu nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi wakati akiongea na Waandishi wa Habari jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Alisema usimamizi wa raslimali za uvuvi nchini unazingatia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 2015; Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2018, 2019, 2020 na 2022. Aidha, Kwa upande wa uvuvi wa dagaa vigezo na masharti ya uvuvi huu yapo katika Kanuni ya 66 ya Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009 na Marekebisho yake kuhusu matumizi ya taa za sola katika shughuli za uvuvi.

“Serikali haijatoa agizo la ukomo wa matumizi ya Taa za Sola kama ilivyodaiwa. Hata hivyo, Wizara kupitia Mkutano wa wadau wa Sekta ya Uvuvi uliofanyika mwezi Novemba 2022 mkoani Mwanza pamoja na masuala mengine ulijadili suala hili na kuazimia kuanza kutolewa kwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Taa za Sola kwa kushirikiana na wadau. Azimio hili limeanza kutekelezwa na ni suala endelevu hata hivyo kumekuwepo na upotoshaji wakati wa zoezi hili,”aliongeza

Bw. Bulayi alitumia fursa hiyo kuwahimiza wavuvi wote hususan wa Dagaa katika Ziwa Victoria na wananchi kwa ujumla kuendelea na shughuli zao za uvuvi kwa kutumia zana na njia rafiki ili kulinda raslimali za uvuvi, Ikolojia na mazingira kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo iliyopo,”aliongeza

Kuhusu masuala ya msamaha wa kodi kwenye zana za uvuvi, Bulayi alisema kuwa Serikali ina utaratibu wa wazi kuhusiana na masuala ya msamaha wa Kodi na Ruzuku. Hivyo, Wizara itaendelea kufuata utaratibu huo ili kuona uwezekano wa kutekeleza hoja husika. Aidha, nitumie fursa hii kuhimiza wadau wote wa suala hili wakiwemo watoa huduma wa Taa za Sola kufuata utaratibu uliopo kuhusu masuala ya kikodi.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na kwamba kila mdau mwenye nia ya kuwekeza katika fursa mbalimbali zinazojitokeza kwenye Sekta ya Uvuvi kufanya hivyo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Aidha, alifafanua kuwa Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ilifanya utafiti kwa kutumia taa za aina zote zinazotumika kwenye uvuvi husika, ikijumuisha na zile zinazoendeshwa na betri za pikipiki na zinazoendeshwa na mafuta ya taa( karabai) ambapo ilipendekeza kutumika kwa taa za sola zenye jumla ya Watt 90 kwa chombo cha uvuvi, kwa maana ya kwamba kila taa moja isizidi Watt 10.

“Taarifa za kitafiti zimethibitisha kwamba betri zenye kutumia teknolojia ya ‘lead-acid’ (betri za pikipiki) zinasababisha uchafuzi wa mazingira, hasa zinapotumika vibaya na kutupwa kwenye maji hivyo kuwa na uwezekano wa kuharibu ikilojia na mazingira ya ziwa,”alibainisha

Bw. Bulayi aliwahimizia wadau wa uvuvi kuendelea kufanya uvuvi endelevu na kwa wavuvi wa Dagaa kuzingatia Sheria zilizopo ili kuepuka uharibifu wa mazingira, athari kwa bioanuai na Ikolojia kwa mazalia ya samaki na mazingira kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi (katikati) akiongea na Waandishi wa Habari(hawapo pichani) wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizosambaa kuwa Serikali imetoa agizo la kusitishwa kwa matumizi ya Taa za Sola katika Uvuvi wa Dagaa kwenye Ziwa Viktoria. Akiongea na Waandishi hao jijini Dodoma Leo Disemba 31, 2022 alisema taarifa hizo sio za kweli huku akiwataka wavuvi kuendelea na shughuli zao kama kawaida. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Uendelezaji wa Raslimali za Uvuvi, Bw. Didas Mtambalike. Kulia ni Mteknolojia wa Samaki, Bw. Masui Munda.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad