
Dar es Salaam 14 Januari 2023 - WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amezitaka taasisi zinazohusika na maendeleo ya vijana, wanawake na makundi maalum kuanza kuhamasisha makundi hayo kuwekeza kwenye mfuko wa faida fund.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mfuko huo uliopo chini ya Watumishi Housing, Waziri Mhagama amesema Serikali isingependa kuona Watanzania wanaachwa nyuma katika shughuli za uwekezaji na ukuzaji wa mitaji.
Waziri
huyo alitoa pongezi nyingi kwa shirika la uwekezaji katika makazi la
Watumishi Housing kwa kuja na ubunifu huo ambao si tu unatoa fursa ya
wananchi kuwekeza kwa faida nzuri, bali pia unasaidia shirika hilo
kupata mtaji wa utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dkt. Fred Msemwa amesema uanzishwaji wa mfuko huo unatokana na maoni ya wawekezaji ambao wamekuwa wakipendelea kuwekeza mitaji yao kwa muda mfupi.
Dkt. Msemwa amesema
pamoja na mafanikio makubwa ya mfuko wa awali wa uwekezaji katika sekta
ya makazi (WHC-REIT) uliozinduliwa mwaka 2014 na kukusanya zaidi ya
bilioni 59, baadhi ya wawekezaji hususan wawekezaji binafsi wamekuwa
wakiomba kuanzishwa kwa mfuko utakaotoa fursa kwa wawekezaji wengi
zaidi.
“Kwakuwa hili ni shirika la kizalendo tuliazimia kuyafanyia
kazi maoni ya wawekezaji wetu. Leo hii tunajivunia kuzindua mfuko huu wa
uwekezaji wa pamoja wa ‘FAIDA FUND’. Mfuko huu haubagui kiwango cha
chini cha uwekezaji hivyo unatoa fursa Kwa mtanzania yoyote kujiunga,”
alisema Dkt. Msemwa.
Mkurugenzi huyo wa Watumishi Housing
aliwashukuru Benki ya CRDB ambao ni wasimamizi wa mfuko huo, pamoja na
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, kampuni ya sharia ya Abenry
Advocates, na Solomon Brokers kwa namna ambavyo wameshirikiana katika
kuanzishwa kwa mfuko huo.
Akizungumza kwa niaba ya washirika wa mfuko
huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela aliishukuru
Watumishi Housing kwa kuipa benki hiyo fursa ya kuwa msimamizi wa mfuko
huo, na kubainisha kuwa benki hiyo imejipanga kuhakikisha Watanzania
wote wanafiukiwa na kunufaika na fursa hiyo.
Akielezea faida ya mfuko
huo, Nsekela amesema kuwa ni wa kipekee kwani umezingatia sera mahususi
ya huduma jumuishi za kifedha zinazomjali Mtanzania wa rika zote ikiwa
ni pamoja na kuweza kununua vipande kwa shilingi elfu 10 jambo ambalo
linaenda sambaba na sera ya benki hiyo ya kuongeza ujumuishi wa kifedha.
Aidha
amefafanua kwamba, mfuko wa faida fund unakuwa mfuko wa saba katika
mifuko ya uwekezaji wa pamoja ambayo Benki ya CRDB. Hata hivyo amesema
kuwa benki hiyo imejipanga kusimamia mfuko huo kikamilifu na kuhakikisha
maslahi ya wawekezaji yanalindwa.
Nsekela alimweleza Waziri Mhagama
kuwa benki hiyo inajivunia kuwa kinara katika huduma bora za uwekezaji
katika masoko ya mitaji. Alibainisha kuwa Benki ya CRDB inachangia
zaidi ya asilimia 70 ya wateja wote wanaoshiriki katika masoko ya mitaji
na dhamana.
Mwaka jana Benki ya CRDB ilitunikiwa tuzo na Soko la
Hisa la Dar es Salaam kwa kuitambua benki hiyo kama kinara wa huduma
bora kwenye masoko ya mitaji. Benki ya CRDB ndio benki pekee nchini
ambayo inatoa huduma ya kuuza na kununua bidhaa zote za masoko ya mitaji
kupitia mtandao wa matawi yake kote nchini.

Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mfuko wa Faida (Faida Fund), uliofanyika kwenye ukumbi wa
Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es salaam,
Januari 14, 2023.


No comments:
Post a Comment