Mamlaka ya usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeadhimisha Siku ya Usafiri wa Anga Duniani (ICAD) mwaka 2023 kwa maandamano yaliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Banana-Ukongo jijini Dar es Salaam.
Maandamano hayo yaliyohusisha watumishi wa Mamlaka na wanafunzi wanachama wa ‘aviation club’ kutoka shule mbalimbali za sekondari yamefanyika leo Disemba 7 na kauli mbiu isemayo “Kuendeleza Ubunifu kwa Maendeleo ya Dunia”, hivyo kufanya siku hiyo kuadhimishwa kwa mara ya 79, na miaka 79 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).
Akizungumza mara baada ya maandamano hayo, Mkurugenzi wa Huduma wa Mamlaka TCAA, Teophory Mbilinyi amesema Mamlaka inazidi kuboresha mifumo yake na ili kuzidi kulifanya anga la Tanzania kuwa salama na kutoa huduma bora za urambazaji wa anga.
“Lengo hasa la siku hii ni kukumbushana majukumu yetu ya kuhakikisha kwamba tunasimamia shughuli za usafiri wa anga na kuhakikisha kwamba anga letu na hata anga jirani linakuwa salama,” amesema Mbilinyi.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Uongozaji Ndege TCAA, Flora Mwanshinga amesema kwa sasa wanatekeleza mradi mpya na mkubwa wa kubadilisha mitambo ya sauti ya analojia na kugeukia mitambo ya kidigitali itakayowasaidia marubani na waongoza ndege.
“Kusimika ile mitambo hasa itaanza mwezi Januari, tunategemea ndani ya miezi mitano, mradi utakuwa umekamilika,” amesema Mwanshinga.
Sherehe hizo hufanyika Desemba 07 ya kila mwaka, iliyoasisiwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), Tanzania ni nchi mwanachama. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Ubunifu endelevu kwa Maendeleo ya Usafiri wa Anga Duniani’.


Mkurugenzi wa Huduma wa Mamlaka TCAA, Teophory Mbilinyi akipandisha Bendera ya hirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani (ICAD) yaliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Banana-Ukongo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma wa Mamlaka TCAA, Teophory Mbilinyi akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani (ICAD) yaliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Banana-Ukongo jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Huduma wa Mamlaka TCAA, Teophory Mbilinyi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani (ICAD) yaliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Banana-Ukongo jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment