Mkuu wa Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha la Taaluma lijulikanalo kama Career Fair lililoandaliwa na Chuo hicho kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi katika kukabiliana na soko la ajira nchini
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa kushoto na Katibu Mtendaji wa baraza la usafirishaji Meli (TSC), Sallu Johnson wa katikati, wakipata maelekezo kutoka kwa Hellen Ignatus aliyebuni mfumo maalamu wa kuoshea magari kwa muda mfupi na kwa weledi ( automatic car wash system).
Baadhi ya wadau na wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha usafirishaji NIT, wakifuatilia hotuba ya Katibu Mtendaji wa baraza la usafirishaji meli (TSC) Sallu Johnson hayupo pichani, wakati wa ufunguzi wa tamasha la Taaluma lijulikanalo kama Career Fair lililoandaliwa na Chuo hicho kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi katika kukabiliana na soko la ajira nchini
Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Usafirishaji nchini (TSC) Sallu Johnson amekitaka Chuo cha Usafirishaji nchini (NIT) kuendelea kuboresha mitaala ya mafunzo vyuoni kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo ili kuendana na soko la ajira za wataalamu wa sekta hiyo.
Hayo ameyabainishwa leo Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Tamasha la taaluma liitwalo Career Fair lililoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi katika kukabiliana na hali ya soko la ajira nchini.
Amesema malengo ya kujifunza masuala ya kazi yanasaidia kutimiza malengo ya uanzishwaji wa chuo hicho kwa kuboresha taaluma za wanafunzi na kuakisi dira ya maendeleo ya nchi ya kujenga mifumo imara ya sekta ya usafirishaji.
Ameeleza kuwa fursa ya kujifunza kwa vitendo inasaidia wanafunzi kuelewa namna ya kufanya kazi zao vizuri na lengo la kujenga kizazi chenye weledi.
"Naamini kuwa tukio hilo litakuwa chachu ya ushirikiano baina ya chuo na wadau wa sekta ya usafirishaji na kufikia soko la ajira kwa kuboresha mitaala ya mafunzo chuoni na ushirikiano wa wadau," amesema Johnson.
Ametoa rai kwa wawakilishi kutoka sekta za umma na binafsi kuendelea na ushirikiano huo kwa sababu jukumu la kujenga wanataaluma waliobobea sio la chuo pekee.
"Tamasha hili la taaluma unaendana na juhudi ya kuunganisha taasisi za elimu na wadau walipo kwenye soko la ajira, wanafunzi watapata fursa ya kujifunza na kuelewa mabadiliko yaliyopo kwenye soko la ajira duniani na sekta binafsi imepewa nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo hivyo wanafunzi wanajukumu la kuongeza uelewa huku wakiwa na mkakati wa kutosha kukabiliana na soko la ajira," amesisitiza.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Profesa Zakaria Mganilwa amesema tamasha hilo limewakutanisha wadau wa sekta za usafirishaji na wanafunzi wa chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kujifunza kwa vitendo pamoja na kupata uelewa wa soko hali ya soko la ajira nchini.
Profesa Mganilwa amesema kumekuwa na nafasi kati ya wanavyofundisha chuoni na vilivyomo kwenye soko la ajira.
Ameongeza kuwa katika kutengeneza daraja hilo wameona kuwa na tamasha hilo ili walimu na wanafunzi wapate fursa ya kujifunza kutoka kwa waajiri ili kuboresha taaluma zao na kuwajengea uwezo wa kutambua soko la ajira lilivyo.
"Kuwahamasisha vijana wetu kujiajiri na kuajiri wengine. Chuo kimebadilika sana kwani wanaprogramu nyingi shahada za kwanza 15, diploma 25 na jumla ya wanafunzi 14,000," amesema Profesa Mganilwa.
Pia amesema chuo kinajivunia kwamba ndoto za waasisi wao zimetimizwa za kuboresha sekta ya usafirishaji wa maji, reli, anga na kebo na wapo wanafunzi wa kutosha katika kozi zote.
Aidha amesema tamasha hilo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika uboreshaji miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa reli, ujenzi wa bandari pamoja na ujenzi wa meli kwa kuwaandaa wataalamu wazawa waliobobea katika sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment