MTOTO WA BIBI TITI: MAMA ALIJITOA MUHANGA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 16, 2022

MTOTO WA BIBI TITI: MAMA ALIJITOA MUHANGA

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

MTOTO pekee wa Hayati Bibi Titi Mohammed, Bi. Halima Mzee amesema kuwa Mama yake alijitoa muhanga katika kuhakikisha taifa linapata uhuru sanjari na kushirikiana na Waasisi wengine, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akizungumza katika Kongamano la Kumbukizi yake mkoani Pwani, Bi. Halima amesema Mama yake hakuwa na hofu katika kufanikisha malengo ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa huru na kung’atuka mikononi mwa mkoloni.

Bi. Halima amesema Mama yake angekuwa hai, angefurahi kuona Wanawake wanashika nafasi mbalimbali za uongozi katika kada mbalimbali katika nchi na hata kushika nafasi za juu za uongozi kuliongoza taifa huru la Tanzania.

“Enzi za uhai wake, Mama yetu alihamasisha sana harakati za kujikomboa, haswa alihimiza Wanawake kuwa mstari wa mbele katika ukombozi huo, mfano kwa sasa angefurahi sana kuona Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, amesema Bi. Halima, Mtoto wa Bibi Titi.

“Sisi Wanafamilia tunafurahi kuona tunaungana pamoja na watu wengine wa kada mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya kumuenzi Mama yetu, Hayati Bibi Titi Mohammed kwa kutambua mchango wake katika taifa hili”, ameeleza Bi. Halima.

Hayati Bibi Titi Mohamed alizawaliwa mwaka 1926, Wilayani Temeke, ni Mwanamke pekee ambaye alikuwa Mwanaharakati wa kuhamasisha ukombozi wa taifa la Tanzania ili lipate uhuru wake kutoka mikononi mwa wakoloni, Bibi Titi alimsaidia sana Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika harakati hizo.
Mtoto pekee wa Hayati Bibi Titi Mohammed, Bi. Halima Mzee akizungumza katika jopo lililoundwa kuelezea yaliyofanywa na Bibi Titi enzi za uhai wake, jopo hilo liliundwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Dar es Salaam, Bi. Kate Kamba, Nguli wa lugha ya Kiswahili, Prof. Aldin Mutembei na  Prof. Shani Omari wote kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kongamano la Kumuenzi Mwanaharakati huyo wa ukombozi wa taifa la Tanzania lilifanyika Rufiji mkoani Pwani.
Viongozi waliohudhuria mdahalo ulioandaliwa kwenye Kongamano la Kumuenzi Hayati Bibi Titi Mohammed, kutoka kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Bi. Zainabu Shomari, wa pili ni Mwenyekiti wa Umoja huo, Bi. Mary Chatanda, wa tatu ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji, ambaye ni Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mohammed Mchengerwa na wa nne ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Pauline Gekul.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad