HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 14, 2022

Dkt. Kisenge: Jiendelezeni kielimu ili muendane na teknolojia ya matibabu

  

Na  Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

 

14/12/2022 Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kujiendeleza kielimu ili waweze kutoa huduma bora zinazoendana na teknolojia za kisasa zinazotumika duniani kwa ajili ya kutoa matibabu kwa wagonjwa.

 

Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na viongozi wa JKCI katika kikao cha kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24.

 

Dkt. Kisenge alisema kutokana na maendeleo na teknolojia kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya afya jambo ambalo linawalazimu wafanyakazi wa sekta hiyo kutafuta namna ya kuongeza ujuzi ili huduma wanazozitoa ziweze kuendana na kasi ya maendeleo duniani.

 

“Kwenda kuongeza elimu katika fani zetu ni sehemu ya kuongeza ujuzi katika utendaji wetu wa kazi lakini pia kunatusaidia kubadilisha mazingira tuliyoyazoea na kutupa motisha ya kujifunza vitu vipya ambavyo katika mazingira yetu havikuwepo hii yote ikiwa ni kwa maslahi ya huduma tunazozitoa kwa wagonjwa wetu,” alisema Dkt. Kisenge.

 

 Aidha Dkt. Kisenge aliwataka wafanyakazi wa Idara ya Ununuzi na Ugavi kuyatembelea  makampuni yanayotengeneza bidhaa zinazotumiwa na Taasisi hiyo zikiwemo dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama kwa kununua bidhaa hizo kwa watu ambao nao wanaziagiza kutoka katika makampuni hayo.

 

“Bajeti hii ya mwaka wa fedha 2023/24 tutaitekeleza kwa asilimia 100 kama wafanyakazi wa Idara ya Ugavi na Ununuzi wataangalia namna ya kubana matumizi kwa kuzifikia kampuni zinazozalisha dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama kubwa tunazotumia kununua bidhaa hizo kwa wadau ambao nao wanachukua vifaa hivyo katika makampuni mengine,” alisema Dkt. Kisenge.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi hiyo CPA. Agnes Kuhenga alisema katika bajeti ya mwaka 2022/23 JKCI imefanikiwa kuongeza duka la dawa linalohudumia wagonjwa wote wanaohitaji dawa (Community Pharmacy), pamoja na kupanua eneo la kutakatisha vifaa tiba (Sterilization unit).

 

CPA. Agnes alisema kupitia hela ya mradi wa uviko 19 JKCI imeweza kukarabati na kuweka vifaa vya kisasa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo (ICU) pamoja na chumba maalum cha kuwahudumia wagonjwa wa moyo wanaohitaji uangalizi wa karibu (Coronary Care Unit - CCU)

 

“Katika mafanikio tuliyoyapata kupitia huduma tunazozitoa kwa wagonjwa wetu tulijiwekea kwa mwaka wa fedha 2022/23 tufanye upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa 1700 hivyo ukichukua miezi mitano ya Julai hadi Novemba 2022 tumeshafanya upasuaji huo kwa wagonjwa 889 haya ni mafanikio makubwa kwetu”,.

 

“Kwa upande wa upasuaji wa kufungua kifua  tulijiwekea malengo ya kufanya upasuaji kwa wagonjwa 700 ambapo ukigawa kwa miezi 12 kwa kipindi hiki cha miezi mitano yaani Julai hadi Novemba 2022 tumeshafanya upasuaji kwa wagonjwa 278”,  alisema CPA. Agnes.

 

Naye mkuu wa kitengo cha watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Sulende Kubhoja alisema kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 JKCI iangalie namna ya kuongeza vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum pamoja na vifaa vyake ili itakapotokea janga linalohitaji huduma za ICU kama lile la UVIKO 19 Taasisi hiyo iweze kupokea wagonjwa hao na kuwahudumia.

 

“Wakati wa UVIKO 19 tuliona ambavyo huduma za ICU pamoja na mashine za kusaidia kupumua (Ventilator) zilivyokuwa zinahitajika kwa wagonjwa wa hivyo sasa ni wakati wetu kupitia bajeti hii na ili na sisi tuongeze mashine hizo pamoja na vyumba hivyo ili kama Taasisi ya Umma tuwe msaada kwa wagonjwa kipindi linapoibuka janga la kitaifa,” alisema Dkt. Kubhoja.

Mkurugenzi wa  Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Agnes Kuhenga akiwasilisha rasimu ya bajeti ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24 wakati wa kikao na viongozi wa JKCI cha kupitia na kujadili bajeti ya Taasisi hiyo ya mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akielezea namna ambavyo JKCI itatekeleza  majukumu yake wakati wa kikao cha viongozi wa Taasisi hiyo cha  kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya JKCI kwa  mwaka wa fedha wa 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Vida Mushi akiwasilisha baadhi ya vifungu vilivyopo katika bajeti ya Taasisi hiyo wakati wa kikao cha viongozi wa Taasisi hiyo cha kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya Taasisi ya mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mawasilisho mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa wakati wa kikao cha viongozi wa Taasisi hiyo kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya Taasisi ya mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi hiyo mara baada ya kumaliza kikao cha kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya Taasisi ya mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Picha na JKCI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad