HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 8, 2022

CMSA WAZINDUA SHINDANO LA MASOKO YA MITAJI KWA WANAFUNZI VYUO VIKUU, TAASISI JIJINI DAR ES SALAAM

 

 

Na Mwandishi, Wetu Michuzi TV


MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imezindua Shindano la Masoko ya Mitaji kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu pamoja na kutunuku vyeti kwa wahitimu wa kozi ya watendaji katika Masoko ya Mitaji wanaokidhi viwango vya Kimataifa katika ukumbi wa Mikutano

Akizungumza mbele ya wageni waalikwa na wadau mbalimbali wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Desemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA Nicodemus Mkama amesema Katika kutekeleza moja ya mikakati ya Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha CMSA inatekeleza mkakati wa utoaji wa elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji.

Amesema katika utekelezaji wa mkakati huo CMSA inaendesha Shindano kwa Wanafunzi wa Vyuo vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Yaani the Capital Markets Universities and Higher Learning Institutions Challenge, kwa lengo la kuongeza uelewa na kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika masoko ya mitaji kwa kutumia njia ya mitandao ya kielektroniki yaani simu za mikononi na intaneti.

"Shindano hili linahusisha wanavyuo wa elimu ya juu kote nchini - Bara na Visiwani kushirki na kujifunza kwa vitendo na nadharia fursa mbali mbali za uwekezaji katika masoko ya mitaji.Mhe. Mgeni rasmi, shindano hili utakalozindua leo tarehe 7 Desemba 2022 linatarajiwa kufungwa tarehe 31 Machi 2023 ili kutoa muda wa kutosha kwa wanafunzi kushiriki bila kuathiri ratiba za masomo.

"Limegawanyika katika sehemu kuu mbili, ambazo ni (shindano la maswali na majibu - Quiz Competition) na (Shindano la kuandika Insha - Essay Competition).Kupitia shindano la Maswali na Majibu (Quiz Competition), wanafunzi wanatakiwa kujibu maswali 100 kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa njia ya simu za mkononi, tovuti

"Ambapo mshiriki alitakiwa kujisajili kwa kuandika taarifa zake muhimu, ikiwa ni pamoja na majina matatu; jinsia; chuo; na kozi anayosoma, na kisha kufuata maelekezo mengine.Kupitia shindano la pili la Kuandika Insha (Essay Competition), wanafunzi watatakiwa kuandika insha kuhusu “Namna masoko ya mitaji yanavyotumika kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na kuchochea ujenzi wa uchumi shindani kwa maendeleo ya watu”.

Ameongeza isha hiyo inatakiwa isizidi kurasa nne (4), maneno 1,500 na kisha kuituma insha hiyo kwa barua pepe ambayo ni challenge@cmsa.go.tz. Washindi katika mashindano hayo ni wale ambao watapata alama za juu kuliko washiriki wengine na ambao pia wataweza kujibu kwa ufasaha maswali ya usaili utakaofanyika mbele ya jopo la majaji ili kudhihirisha kuwa wao ni washindi

Aidha amesema katika mwaka huu, CMSA imeweka lengo la kuwafikia wanafunzi wapatao 18,000 ikilinganishwa na wanafunzi 16,275 walioshiriki shindano hili katika mwaka wa fedha 2020/2021, ikiwa ni matarajio ya ongezeko la asilimia 10.6 na kwamba ili kufikia lengo hio wameweka mikakati mbalimbali ya kurahisisha ushiriki wa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kutumia njia ya simu za mkononi, tovuti, na barua pepe

Ambapo mwanafunzi kwa kutumia bando lake la kifurushi cha kawaida ana uwezo wa kuingia kwenye tovuti ya shindano na kupata taarifa na taratibu za ushiriki na kuajiandikasha kushiriki katika shindano la maswali na majibu na hali kadhalika kuwasilisha inshia yake. Kwa wanafunzi ambao wako maeneo ambayo yana changamoto za mtandao wa kieletroniki bado wataweza kushiriki shindano hili kwa kutumia barua pepe na simu za mkononi kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi yaani “SMS”.

"Hivyo basi, wanafunzi wanaweza kutumia simu janja (Smartphone) au kiswaswadu (USSD). Mhe. Mgeni rasmi, ili kuwezesha washiriki wa shindano hili kutumia elimu ya nadharia watakayoipata kwa vitendo, CMSA imeandaa utaratibu wa kuwawezesha washiriki wa shindano hili kuwa wawekezaji halisi.

"Kupitia mpango huu washindi 80 watakaopata alama za juu kwenye shindano, watatumia theluthi moja ya zawadi ya fedha taslimu watakazopata ili kuwekeza kwenye masoko ya mitaji kwa kununua hisa na hatifungani za kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam; au vipande katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

"Mpango huu unatarajia kuongeza wawekezaji wapya katika masoko ya mitaji.Mhe. Mgeni rasmi, miongoni mwa zawadi watakazopata washindi wa shindano hili ni kama zifuatavyo:Washindi wa kwanza kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana watapata Sh.1,800,000

"Washindi wa pili kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana watapata Sh.1,400,000);Washindi wa tatu kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana watapata Sh.800,000

Washindi wa nne kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana watapata Sh.400,000); Washiriki waliobaki katika 10 bora watazawadia Sh 200,000 .Washiriki wote waliofika fainali na kuwa miongoni mwa washindi 20 walioshika nafasi za juu watapatiwa vyeti (certificate of recognition); fulana zenye nembo ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana;

Pia Washiriki 6 wavulana; na 6 wasichana wenye alama za juu zaidi watagharamiwa ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ili kujifunza zaidi maswala ya masoko ya mitaji ikiwa ni pamoja na masoko ya hisa na kampuni kubwa zinazohusika na utoaji huduma katika masoko ya mitaji hapa nchini na nje ya nchi.

"Aidha hapa tunao baadhi ya wanafunzi washindi wa shindano la mwaka 2020/2021 ambao wameweza kuendeleza ndoto zao za kushiriki kwenye soko la mitaji na hivyo kutumia sehemu ya fedha zao walizopata kama zawadi kununua hisa za kampuni mbalimbali zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa.

"Hawa sasa wamekuwa wawekezaji halisi na sio kwa nadharia tu. Hawa pia, leo utawakabidhi vyeti vya umiliki wa hisa zao walizonunua kwa kutumia fedha za zawadi ya ushindi na wengine wameongezea fedha zaidi ya hizo na kununua hisa, ambapo uwekezaji wao umekua kwa zaidi ya asilimia 300.Katika jitihada za kuongeza idadi, ueledi na ufanisi wa wataalamu wa masoko ya mitaji wanaokidhi viwango vya kimataifa wenye lengo la kukuza na kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini,"

Ameongeza kwamba Mamlaka imekuwa ikishirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Uwekezaji na Dhamana (Chartered Institute for Securities and Investment - CISI) ya nchini Uingereza, katika kuendesha mafunzo yanayotambulika kimataifa yanayolenga kujenga uwezo na ufanisi kwa watendaji w"a masoko ya mitaji.


MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) Dk.John Mduma (wa tatu kulia) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa   shindano linalohusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo Mamlaka ya Masoko  wanatarajia washiriki wapatao 18,000 watashiriki Shindano hilo.

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) Dk.John Mduma akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua shindano linalohusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo Mamlaka ya Masoko  wanatarajia washiriki wapatao 18,000 watashiriki Shindano hilo.

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Dk.John Mduma akipongezwa na Ofisa  Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama mara baada ya kuzindua shindano linalohusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo Mamlaka ya Masoko  wanatarajia washiriki wapatao 18,000 watashiriki Shindano hilo.

 Ofisa  Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama akizungumza huku akimkaribisha mgeni rasmikwa ajili ya  kuzindua shindano linalohusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo Mamlaka ya Masoko  wanatarajia washiriki wapatao 18,000 watashiriki Shindano hilo.

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad