HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 15, 2022

BILIONI 6.01 KUTEKELEZA MRADI WA MAJI KATIKA VIJIJI VITANO MUFINDI,WANANCHI WAIPONGEZA RUWASA KWA KAZI NZURI

Na Muhidin Amri,
Mufindi

KERO ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji vitano vya Mabaoni,Makungu,Lugema,Isaula na Kiyowela  katika Halmashauri ya wilaya Mufindi mkoani Iringa inakwenda kuwa historia baada ya serikali kutoa Sh.bilioni 6.01ili kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa Mgololo.


Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mufindi Mhandisi Irine Sengiwa alisema, fedha hizo zitatumika kumaliza kabisa tatizo la muda mrefu la huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 14,740 wa vijiji hivyo.

Alisema,ujenzi wa mradi ulianza kutekelezwa mwezi machi 2022 na unatarajiwa kukamilika mwezi machi mwaka 2023 kwa fedha za mfuko wa maji(NWF)na unajengwa na mkandarasi kampuni ya  M/S Kings Bulders Limited ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 65.

Sengiwa alisema,katika mradi huo kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ununuzi na ulazaji mabomba(bomba kuu na bomba  la usambazaji),uchimbaji na ufukiaji wa mitaro umbali wa km 75 na ujenzi wa mtego wa maji.

Alitaja kazi nyingine ni ujenzi wa matenki  manne ya kuhifadhia maji katika vijiji vya Makungu,Isaula, Kiyowela yenye ujazo wa lita 75,000 kila moja na tenki moja katika kijiji cha Mabaoni la lita 20,000, ujenzi wa vituo 50 vya kuchotea maji na ofisi ya chombo cha watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) katika kijiji cha Mabaoni.


Kwa mujibu wa Sengiwa,kazi zilizofanyika ni ujenzi wa mtego wa maji,tenki zote nne za kuhifadhia maji,vituo vya kuchotea maji na kuchimba mtaro umbali wa km 18.


Alisema,serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilayani Mufindi,itahakikisha  inamsimamia mkandarasi kwa karibu ili mradi uwe na ubora na unakamilika kwa muda uliopangwa.

Alitaja faida za mradi  huo pindi utakapo kamilika,ni kupunguza muda wa wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji na kupata nafasi kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine za kiuchumi ikiwamo kilimo,ufugaji na biashara ndogo ndogo.

Kwa upande wake mwakilishi wa  mkandarasi  Miliki Mlindoko alisema, ujenzi wa mradi  unaendelea vizuri ambapo matenki yote manne yamekamilika na kazi inayoendelea kwa sasa ni ulazaji wa mabomba.


Mlindoko,amehaidi kukamilisha kazi zote zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo,kwani wako ndani ya muda wa mkataba na kuwaomba wananchi kuwa subira na kutunza miundombinu ili mradi uweze kudumu kwa muda mrefu.


Mwenyekiti wa kijiji cha Isaula Isdory Kipapi,ameishukuru wizara ya maji kupitia Ruwasa kuanza ujenzi wa mradi huo kwani utamaliza  kero ya muda mrefu ya huduma za maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji hicho.


Pia amemuomba mkandarasi,kuanza ujenzi wa vituo vya kuchotea maji ili wananchi waanze kupata huduma huku kazi nyingine zikiendelea kutekelezwa kwani wana hamu kubwa na maji ya bomba na  wamechoka kusubiri.

Mmoja kati ya vijana wanaofanya kazi  katika mradi huo Petro Msaula alisema,mradi umewasaidia kupata ajira za muda ambazo zinawaingizia fedha na kupunguza baadhi ya changamoto zilizopo kwenye familia zao.
Moja kati ya matenki manne yaliyojengwa kupitia mradi wa maji wa Mgololo lenye uwezo wa kuhifadhi lita 75,000 za maji.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Mhandisi Irene Sangiwa,akijaribu kufungua maji kutoka kwenye tenki lililojengwa kwenye mradi wa maji wa Mgololo.
Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Mhandisi Irene Sangiwa katikati na mwakilishi wa kampuni ya King's Builders Ltd inayojenga mradi wa maji wa Mgololo wilayani humo Miliki Mlindoko wa tatu kushoto wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Ruwasa na wa kampuni hiyo.
Mwakilishi wa kampuni ya King's Builders Ltd inayojenga mradi wa maji wa Mgololo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Miliki Mlindoko,akimweleza jambo Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mufindi Mhandisi Irene Sangiwa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambao hadi sasa umefikia asilimia 65 ya utekelezaji wake. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad