Na Mwandishi Wetu
SEKTA ya Utangazaji nchini Tanzania imeendelea kukua kwa ongezeko la vituo vya utangazaji wa televisheni na redio, redio na televisheni Mtandao na televisheni za waya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dodoma katika Mkutano ulioratibiwa na Idara ya Habari Maelezo ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo mwaka 2003 jumla ya watoa maudhui 741.
Dkt. Jabiri alibainisha kuwa tangu kuasisiwa kwa Mamlaka hiyo jumla ya vituo vya televisheni 61 vilisajiliwa, televisheni za Mtandao 390, televisheni za waya 65, vituo vya redio 218 na redio za mtandaoni 7.
Alieleza kuwa Mamlaka hiyo imejidhatiti kuhakikisha sekta ya utangazaji nchini inakua na kuleta mchango chanya kwa ukuaji wa Maendeleo ya nchi.
“Utangazaji ni njia pekee ya Mawasiliano inayowafikia watu wengi kwa haraka na wakati mmoja. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya sekta ndogo ya Utangazaji ina wajibu wa kuweka mazingira rafiki ya kusambaza huduma za Utangazaji kwa njia ya redio, televisheni na mitandao nchi nzima ili kumfikia kila Mwananchi,” alisisitiza Jabiri.
Alibainisha kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itahakikisha kuwa maudhui yanayorushwa na vituo vya Utangazaji yanazingatia maadili na weledi wa uandishi wa habari na pia hayakiuki Sheria na Kanuni zinazosimamia sekta ya Utangazaji.
“Ni wajibu wa Mamlaka kuhimiza utengenezaji, uzalishaji na usambazaji wa maudhui ya ndani (local content) na kutangaza urithi, vivutio, mila na desturi za mtanzania,” alibainisha Mkurugenzi Mkuu Jabiri.
Alibainisha kuwa katika kutekeleza majukumu yake TCRA hushirikiana na taasisi za kimataifa na kikanda zinazosimamia mawasiliano na wadhibiti wa mawasiliano katika nchi nyingine ambapo kwa sekta ya utangazaji Tanzania ni mwanachama wa Shirikisho la Utangazaji la Kusini mwa Afrika (Southern African Broadcasting Association - SABA).
Alieleza kuwa takwimu za utangazaji zinaonyesha kwamba visimbuzi 3,326,845 vilikuwa hewani hadi Septemba 2022. Kati ya hivyo, 1,656,460 ni vya dijitali kwa mfumo wa televisheni wa utangazaji wa mitambo ya ardhini (DTT) kulinganisha na 1,670,385 kwa mfumo wa televisheni kwa satelaiti.
Jabiri alibainisha kuwa Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na visimbuzi (1,270,755), ikifuatiwa na Arusha (272,702), Mwanza (261,237) na Mbeya (218,007). Mikoa yenye visimbuzi vichache ni Songwe (1,568) ukifuatiwa na Katavi (16,990).
Televisheni za waya (cable tv) zimeenea kutoka watu 16,786 waliounganishwa 2018 hadi 41,092 Septemba 2022. Huduma ya televisheni kwa waya (yaani cable Tv) imeenea mikoa ya Ziwa; ambapo mkoa wa Simiyu unaongoza; ukiwa na jumla ya waliounganishwa 4,584, ikifuatiwa na Mwanza, yenye 3,480.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambae pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akimshukuru Mkurugenzi Mkuu baada ya kueleza kazi za TCRA alibainisha kuwa Serikali imejidhatiti kusimamia vema sekta ya Mawasiliano nchini ili kuhakikisha inaleta tija zaidi kwa Maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na kujenga mkongo wa taifa utakaowezesha ukuzaji wa sekta ya Mawasiliano ikiwemo sekta ndogo ya utangazaji.
“Mwaka huu tumeweka Bilioni 147. Tunataka tujenge kilomita za mkongo wa Taifa zifike kilomita 15,000 ifikapo 2025,” alibainisha Msigwa.
Akipokea hoja za Waandishi waliohudhuria Mkutano huo wakitaka kujua hatua za TCRA kudhibiti maudhui yasiyofaa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA alibainisha kuwa Mamlaka hiyo kupitia Kamati ya Maudhui itaendelea kuhakikisha sekta ya utangazaji inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya Jamii.
No comments:
Post a Comment