HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 23, 2022

UPANUZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA TANGA WANUKIA

 


Serikali imesema iko katika hatua za mwisho za kuanza utekelezaji wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Tanga kwa kuboresha miundombinu yake ili kuendelea kufuungua kibiashara mkoa huo.

Akizungumza jijini Tanga Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema nia ya Serikali ni kuufanya Mkoa wa Tanga kukua zaidi kibiashara hasa kwa kuzingatia kuna miradi mikubwa inayotekelezwa mkoani humo ambayo kukamilika kwake kunahitaji njia zote za usafiri.

“Mkoa wa Tanga kwa sasa kuna miradi mikubwa inayotekelezwa mfano upanuzi wa bandari, pia kuna miradi itakayorekelezwa kama ujenzi wa bomba la mafuta likalojengwa kuelekea nchini Uganda, hivyo lazima tuhakikishe miundombinu wezeshi inakuwepo mapema”, amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameutaka uongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Tanga na Mamlaka ya Viwanja vya ndege (TAA), kuhakikisha wanakaa pamoja kwenye kila hatua ili kupunguza changamoto za kiutendaji ambazo zinaweza kujitokeza mara mradi utakapokamilika.

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Tanga, Bw. Mussa Mchola, amesema kiwanja hicho kwa sasa kinahudumia ndege ndogo zenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 5 hadi 12 za ratiba na zisizo za ratiba.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Eng. Eliazary Rwekiza, amesema kwa sasa Serikali imeshalipa fidia kwa wananchi waliopisha eneo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja hicho.

Eng. Rwekiza ameongeza kuwa upanuzi wa kiwanja hicho utaanza wakati wowote ambao utahusisha ujenzi wa barabara 2 za kuruka na kutua ndege ambapo moja itajengwa kwa kiwango cha lami na nyingine kwa kiwango cha changarawe, barabara ya maegesho ya ndege, mifumo ya maji, taa, uzio, jengo la abiria na mnara wa mawasiliano, jengo la zima moto na kituo cha umeme.

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Sekta ya Uchukuzi na utendaji wa taasisi zilizo chini yake.
Muonekano wa moja ya barabara ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa meta 1.268 katika Kiwanja cha Ndege cha Tanga. Serikali iko kwenye mpango wa kuboresha miundombinu ambapo barabara hiyo itarefushwa kutoka meta 1,268 hadi meta 1.800.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akitoa maelekezo kwa Mameneja wa Taasisi zilizopo katika Kiwanja cha Ndege cha Tanga, wakati alipotembelea kiwanja hicho, mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akimsikiliza Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Mkoa wa Tanga Moses Mwalyoga kuhusu utendaji wa Mamlaka hiyo katika kiwanja cha ndege cha Tanga, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kiwanja hicho, mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akimsikiliza Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Mkoa wa Tanga Kurwa Mwambo (mwenye shati nyeupe) kuhusu shughuli za Mamlaka katika kiwanja cha Ndege cha Tanga, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kiwanja hicho, mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akimsikiliza Meneja wa Kampuni ya Ndege ya Auric Air Mkoa wa Tanga, Cornelius Maya (Kulia) kuhusu ratiba za shirika hilo, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kiwanja hicho, mkoani Tanga. Katikati ni Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Tanga Mussa Mchola
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akimsikiliza Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Tanga Mussa Mchola (Katikati) kuhusu uendeshaji wa Kiwanja hicho, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kiwanja hicho, mkoani Tanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad