Na. Edward Kondela
Wataalamu wa mifugo nchini wametakiwa kuhakikisha wanatumia vyema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwafikia wafugaji wengi na kutatua changamoto zao.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha hayo katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, wakati akifunga mafunzo rejea ya baadhi ya wataalamu wa mifugo kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita yaliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akisema kuwa idadi ya wataalamu wa mifugo waliopo nchini kwa sasa haitoshelezi kila mfugaji kufikiwa na mtaalamu kwa wakati.
Naibu Waziri Ulega ameongeza kuwa kutokana na ukuaji wa tekonolojia wafugaji wengi wanatumia simu za mkononi hivyo zikitumika vyema kwa kushirikiana na wataalamu wa mifugo kupitia mfumo wa M-Kilimo kwa ajili ya huduma za ugani itakuwa ni njia rahisi kwa wafugaji kutatuliwa changamoto zao kwa haraka zaidi na kupata ushauri wa ufugaji bora na kisasa.
“Lazima wataalamu wetu muwe watumiaji wazuri wa hii mitandao ya kitaaluma ili kupeleka teknolojia kwa wafugaji wetu kwa kuwa hatuna uwezo wa kutosheleza wataalamu kila kijiji upungufu ni mkubwa.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha, amewataka wataalamu hao kuhakikisha wanajiwekea malengo kwa kuwa na wafugaji wachache kila baada ya muda ambao wanawafuatilia kwa karibu kuhakikisha wafugaji hao wanakuwa na maeneo yao wenyewe wanayoyamiliki na kuwapatia elimu na huduma bora za mifugo.
Amesema kwa kufanya hivyo wataalamu wa mifugo wataweza pia kuwafikia wafugaji ambao nao watatoa elimu kwa wenzao juu ya huduma bora za mifugo na kuwahamasisha kumiliki maeneo na kuwa na hatimiliki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa amesema jukumu la wizara ni kusambaza tekonolojia sahihi na zenye ubora ili kuleta mabadiliko chanya kwa wadau mbalimbali wa mifugo na kuwafikia wafugaji kwenye maeneo yao ya kazi kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa.
Ameongeza kuwa katika mafunzo hayo mada mbalimbali zimewasilishwa ikianza na mabadiliko makubwa ambayo sekta ya mifugo inatekeleza pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye Sera ya Mifugo ya Mwaka 2006 kuhakikisha wataalamu wa mifugo wanajengewa uwezo na kuainisha maeneo muhimu ya mpango mkubwa wa mabadiliko.
Pia, amesema mafunzo hayo yamegusia juu ya uendelezaji wa malisho ya mifugo na maji ambapo wafugaji wamekuwa wakipata changamoto hususan nyakati za kiangazi na kuwafanya kuhamahama kutafuta malisho na maji pamoja na namna wafugaji wanavyoweza kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo rejea, wamesema mafunzo hayo yamewakumbusha mambo muhimu ya kufanya kwa wafugaji ili waweze kufuga kisasa na kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiendeleza mafunzo rejea kwa wataalamu wa mifugo kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha inawakumbusha mambo muhimu ya kuzingatia katika taaluma ya mifugo ili wafugaji waweze kufuga kisasa na kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza wakati wa kufunga mafunzo rejea kwa baadhi ya wataalamu wa mifugo (hawapo pichani) kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita yaliyofanyika katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza ambapo amewataka kuhakikisha wanatumia vyema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwafikia wafugaji wengi na kutatua changamoto zao.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza Mhe. Veronika Kessy akizungumzia hali ya sekta ya mifugo katika wilaya hiyo na kuishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna inavyohakikisha inatoa mafunzo rejea kwa wataalamu wa mifugo. Mhe. Kessy amezungumza hayo wakati wa kufungwa kwa mafunzo rejea kwa baadhi ya wataalamu wa mifugo (hawapo pichani) kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita yaliyofanyika katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa akizungumza wakati wa kufunga mafunzo rejea kwa baadhi ya wataalamu wa mifugo (hawapo pichani) kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita yaliyofanyika katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza ambapo amesema jukumu la wizara ni kusambaza tekonolojia sahihi na zenye ubora ili kuleta mabadiliko chanya kwa wadau mbalimbali wa mifugo na kuwafikia wafugaji kwenye maeneo yao ya kazi kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa.
Baadhi ya wataalamu wa mifugo kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita waliohudhuria mafunzo rejea ya siku mbili yaliyofanyika katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza ili kuwakumbusha juu ya taaluma ya mifugo na kubadilishana ujuzi wa namna bora ya kuwahudumia wafugaji.
No comments:
Post a Comment