HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 21, 2022

TUNDURU WAFANYA MNADA WA PILI WA KOROSHO

 


Na Muhidin Amri, Tunduru
WAKULIMA wa zao la korosho mkoani Ruvuma wanaohudumiwa na Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(TAMCU LTD),wamekubali kuuza korosho zao zaidi ya tani 1,600 sawa na kilo milioni 1,657,417 kwa bei ya Shilingi 1.859 kwa kilo moja.

Huo ni mnada wa pili wa zao la korosho kufanyika mkoani Ruvuma, ambapo bei ya chini ilikuwa Sh. 1,855 huku bei ya juu ilikuwa Sh.1,890 na katika mnada huo uliofanyika katika viwanja vya Ukumbi wa Sky Way Tunduru Mjini wakulima wamefanikiwa kujipatia zaidi ya Sh.bilioni 3,081,138,203.

Akizungumza na wawakilishi wa wakulima,viongozi wa vyama vya msingi na Chama Kikuu cha Ushirika wilayani humo(TAMCU LTD)Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dkt Benson Ndiege,amewapongeza wakulima wa zao hilo kwa kukubali kuuza korosho kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Alisema,mfumo huo ni mzuri kwani umewasaidia sana wakulima kuwa na sauti ya pamoja,uhakika wa soko na bei nzuri kutoka kwa wafanya biashara na wanunuzi wamepata korosho safi zinazokusanywa kwenye maghala ya vyama vya msingi vya ushirika(Amcos).

Alisema,kupitia mfumo huo serikali inapata taarifa sahihi juu ya idadi ya wakulima wake,kiasi cha fedha na mazao yanayozalishwa,tofauti na mfumo wa zamani ya soko hulia ambao haukuwa rafiki sana kwa wakulima hapa nchini.

Aidha,amewaomba wanunuzi kutoa bei nzuri kwenye minada ya korosho inayoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ili kuwashawishi wakulima kuendelea na uzalishaji wa zao hilo linalochangia pato kubwa la Taifa.

Dkt Ndiege,amevitaka vyama vya ushirika kutenda haki kwa wakulima na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu,dhuruma na wizi ambavyo kwa sehemu kubwa vinawarudisha nyuma na kuwatisha tamaa wakulima.

“viongozi wa ushirika hakikisheni mnasimamia na kuwatendea haki wakulima ambao ndiyo wanachama wenu,acheni tabia ya ujanja ujanja katika uendeshaji wa shughuli zenu”alisema.

Dkt Ndiege,amewahimiza wakulima kujiunga na vyama vya ushirika ili wapate nafasi ya kuuza mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao tangu ulipoanzishwa umeleta tija kubwa.

Alisema, Serikali ya awamu ya sita inawathamini sana wakulima ndiyo maana imeongeza bajeti ya wizara ya kilimo mara tatu zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma,ili wakulima waweze kufanya shughuli za kilimo kwenye mazingira rafiki.

Naye Mkurugenzi mtendaji bodi ya usimamizi wa stakabadhi ghalani Asangye Bangu,amewashukuru wakulima wa wilaya ya Tunduru kuendelea kuonyesha imani kwa Serikali kwa kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

Alisema,serikali itaendelea kusimamia na kufanya kazi na vyama vya msingi vya ushirika na waendesha maghala waaminifu na wanaofuata sheria na hatokuwa tayari kufanya kazi na watu ambao hawataki kusimamia misingi na taratibu za nchi.

“tukikubaini umekiuka taratibu na maagizo ya serikali hatutosita kukufutia leseni yako na kukuchukulia hatua za kisheria,tunahitaji watu makini wanaofuata sheria na taratibu katika uendeshaji wa kazi zetu”alisema Bangu.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro alisema,serikali itaendelea kuwasaidia wakulima kwa kutoa elimu na ushauri kuhusu kilimo cha kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani na hatimaye wapate maendeleo kupitia shughuli zao za kilimo.

Mtatiro,amewashauri wakulima,kuanza kulima mazao mengine ya biashara kama soya,ambalo lina soko la uhakika na bei nzuri,badala ya kung’ang’ania zao moja la korosho.

Mtatiro amewahimiza wakulima katika wilaya hiyo, kwenda kujiandikisha kwenye ofisi za serikali za vijiji na mitaa ili waweze kupata mbolea za ruzuku zinazouzwa kwa bei rahisi katika vituo na maduka yaliyoteuliwa.
Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dkt Benson Ndiege wa kwanza kushoto,akimsikiliza mtunza ghala la kukusanya na kuhifadhi korosho la Zuma Cargo Edson Kitiga wa kwanza kulia, wakati wa ziara yake ya kukagua na kuzungumza na watunza maghala katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wa pili kulia ni Mkurugenzi mtendaji bodi ya usimamizi wa stakabadhi ghalani Asangye Bangu,
Baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya Ushirika wilayani Tunduru,wakimsikiliza Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika(TAMCU)Imani Kalembo(hayupo pichani)wakati wa mnada wa kwanza wa zao la korosho uliofanyika katika viwanja vya Sky Way mjini Tunduru.
Waandishi wa vyama vya msingi vya Ushirika wlayani Tunduru wakifungua barua za maombi kutoka kwa makampuni yaliyojitokeza kununua korosho katika mnada wa pili wa zao hilo.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu)Mussa Manjaule akitangaza matokeo ya mnada wa pili wa zao la Korosho ambapo katika mnada huo korosho zimeuzwa shilingi 1859 kwa kilo moja,kushoto Meneja Mkuu wa Tamcu Iman Kalembo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad